06 February 2006

Onyesho la sanaa : Mchina amtwanga hadi kumuua Mtanzania..Tanzania.

Hivi majuzi Dennis Londo na MtiMkubwa walituletea kisa cha Mchina kumtwanga Mtanzania hadi kumuua. Leo katika kidirisha cha maoni nimekutana na onyesho kamili la jinsi hali ilivyokuwa, nimeona niwaletee wote tushirikiane kuona hali halisi ya Watanzania tulivyo. Kwa mtindo huu tusije shangaa kukuta 'Mti' kaamua kututengenezea kabisaa filamu yake. Haya onyesho lenyewe hili:-

SEHEMU YA KWANZA:
Mchina mfupi, mdogo kwa umbo, na sura yake kama paka anaonekana anamkimbiza Mtanzania. Mtanzania anakimbia kwa mbio zake zote huku anageukageuka nyuma kuangalia kama atadakwa. Mchina anaongeza kasi. Mtanzania maskini wa MUNGU kasi inapungua kadri anavyozidi kukimbia. Hatimaye Mchina anamkamata Mtanzania.
Wakati huo huo wa kumkimbiza Watanzania wengine wanakimbilia nyuma. Siyo kwamba wanakimbilia kumdhibiti Mchina isipokuwa wanakimbilia kuona kibano atakachopewa Mtanzania na Mchina.

SEHEMU YA PILI:
Mchina kamkamata mwizi wake (Mtanzania). Wote wawili wanahema kwa nguvu kwa sababu ya kukimbia. Mchina anamkunja shati Mtanzania. Watanzania wengine wamefika kwenye tukio wanasubiri kuona cha mtema kuni atakachokipata Mtanzania mwenzao. Mchina anaanza shughuli ya kumuadabisha Mtanzania kwa vibao. Kwa kila kibao anachopokea Mtanzania analia "..mama!.." "..ang'i!.." "..mama!.."
Wakati huo Watanzania wengine wanashabikia "..Kula eeeh.." "..kula eeeh.." "..k...mae wallai Wachina siyo mchezo cheki anavyopiga kunfuu.." Mchina anaona anaumiza mkono wake kwa sababu jamaa ni sugu sana anachukua chuma anaanza kumbonda nalo kichwani kama anaua nyoka. Mtanzania damu zinamchuruzika kwa majeraha. Watanzania wengine wanaacha kuangalia wengine wanaangalia huku wakisema "..Mchina akikasirika hatari.." "..hawa jamaa huwa hawaongei lakini 'usiwauzi'..Maanake wakikasirika jasho litakutoka.." Mchina anaendelea kubonda kichwa na nondo. Paa la uso linapasuka. Mtanzania sasa halii tena bali anaguna tu kila pigo la nondo likitua "..mmgh.." Pigo jingine "..mmmgh.." na jingine tena "..mmgh.." na jingine tena "..mmgh.." na jingine tena hakuna sauti inayotoka Mtanzania kishapoteza fahamu. Mikono, viatu na nguo za Mchina vimetapakaa damu ya Mtanzania. Mchina anamuangalia mtuhumiwa wake anaridhika na kisago alichompa.

ONYESHO LA TATU
Mchina na wenziye wanachumpa ndani ya gari yao kwenda kunawa na kubadilisha nguo. Watanzania waliokuwepo kwenye tukio wanaondoka wasije wakakutwa na polisi wakatakiwa kutoa ushahidi. "..haroo, yaani yule Mchina arikuwa kakasirika bwana..Maanake arikuwa anampiga kwa nguvu kama nini.." "..Mshikaji tukijikate mandata wasije wakatukuta hapa tukaitwa kwenye ushahidi.." "..Lakini jamaa kajitakia mwenyewe sasa kwa nini aliiba?.." ".unajua mimi nilianza kuwaona tangu wanamkimbiza, nikajua tu leo jamaa ataipata.." "..Hivi arifikiri anaweza kumshinda mbio Mchina..Wachina wanafanya mazoezi ware tangu wadogo.." "..Mimi nirikuwaga nawaonaga wakati wanajenga reri ya tazala, tujamaa tudogo rakini tunabeba mataruma ya reli kama kanabeba rura ya kupigia mistari.."

ONYESHO LA NNE
Mtanzania mmoja mzalendo aliyekereheshwa na kitendo kizima anakwenda kuita polisi baada ya tukio kuisha. Polisi wanakuja na mwandishi wa habari mmoja. Polisi wanampinduapindua maiti. Halafu wanawaamrisha watu "..Hebu sogeeni mbali mnatunyima nafasi.." Polisi mmoja anachapa chapa virungu watu wanasogea mbali kidogo. Wengi wa watazamaji wa tukio ni wanaume vijana na watoto wadogo. Watoto wengine wanamtazama maiti huku macho yamewatoka kama wanatazama sinema ya dracula. Polisi wanampindua marehemu kutoa kitambulisho mfukoni ili kumjua jina lake. Kwa bahati nzuri ana kitambulisho. Wamemtambua jina. Halafu wanampasia mwandishi wa habari kitambulisho. Mwandishi anachukua jina halafu anamrudishia ofisa. Maiti anaokotwa anawekwa nyuma ya Land Rover anapelekwa hospitali. Watanzania wanatawanyika. Eneo la tukio linaachwa na damu halafu polisi wamesahau kuokota nondo iliyotumika kumpigia marehemu. Msamaria mwema anaiokota anaitupa jalalani huku akisema "..Isije ikaua mwingine.."

MWISHO
Mchina anapigiwa simu aende kituoni akatoe maelezo ya tukio. Kituo yupo ofisa upelelezi kesi za jinai. Kiingereza chake siyo kizuri sana kwa hiyo stetimenti ataiandika Kopla Masanja kwa sababu anaongea Kiingereza kizuri zaidi. Mchina anafika kituoni masaa kadhaa baada ya tukio. Stetimenti inaandikwa. Mchina anaambiwa itabidi alale ndani jioni ya leo. Baada ya siku mbili tatu suala linakuwa kati ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa China nchini Tanzania. Kwa sababu za kidiplomasia Mchina anakuwa 'dipotedi' Kesi imekwisha.

Watanzania hivi sivyo inavyokuwa? Kama nimekosea kutengeneza onyesho niambieni! Sawa?

7 Comments:

At Tuesday 7 February 2006 at 12:14:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

Onyesho hili sijui niseme nini. Kwanza nimecheka sana. Pili nimesikitika sana. Tatu ninampongeza Mti kwa onyesho hili lenye sehmu nne. Nakubaliana naye kabisa. Ila nadhani kuna mahali amekosea kidogo, yule ndugu aliyetoa taarifa polisi asingeachiwa. Naye angetiwa ndani kusaidia polisi!

Ukisoma onyesho hili utajua kuwa Mti anatufahamu Watanzania vizuri sana. Kwa mfano, mtazamo wa Watanzania kuhusu Wachina. Huwa tunadhani Wachina wote au Wajapani wanajua kung fu au karate.

Inasikitisha kuona Watanzania wale kwenye onyesho walivyokuwa wakitazama Mtanzania na mwanadamu mwenzao akiuawa. Ajabu ni kuwa ingekuwa ni Mtanzania anampiga Mchina, Watanzania wangeingilia kati kumuokoa Mchina.

Ile habari aliyoandika Mti Mkubwa kuhusu wimbo wa taifa kumuoma mola awabariki viongozi wetu (pamoja na kuwa wezi au wazembe) niliitumia kwenye moka ya makala zangu gazetini (nilitaja chanzo cha habari yenyewe kwa heshima yake). Nitamuomba ruhusu nitumie mchezo huu. Mchezo mfupi lakini unatoa picha kubwa sana ya taifa letu. Tulipo na tunapokwenda.

 
At Wednesday 8 February 2006 at 07:14:00 GMT, Blogger Reggy's said...

Da Minja ongera kwa kutufikishia huu mchezo wa kuigiza. nadhani si wa kuigiza, bali ni tukio halisi ambalo limetokea, bali hii ni namna ya kuliripoti. Lakini, kasoro ni kwamba, polisi wa hapa Tanzania hawawezi kushirikiana na mwandishi wa habari namna ile. Mwandishi angekuwa miongoni mwa waliopigwa virungu ili wasogee wasiingilie 'uchunguzi wa polisi', na baadaye waitwe kwa Kamanda wa Polisi wa Mkoa husika (RPC) kuchukua taarifa (ambazo kwa vyovyote zaweza zisiwe kama zilivyotokea).

 
At Thursday 9 February 2006 at 08:58:00 GMT, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

kweli ni kali...na limeonyesha picha halisi za watanzania aka Wabongo...

1. kwanza kupenda kujionea wenyewe...kukimbilia eneo la tukio ili kukuza reference frame na cha kusimulia kibarazani jioni....unajua waTZ hata ikitokea ajali wanashangilia? au wakisikia bunduki wanakimbilia eneo la tukio??

2. kukubali na kukiri bila kuelezwa na yeyote kuwa lazima mswahili kakwapua.....

3. kuamini kuwa sheria huweza kuvunjwa na raia wa kigeni ...yaani raia wa kigeni yu juu ya sheria....udhaifu huu ukaonekana hadi kwenye ngazi za juu za mambo ya nje......

4. kiburi kinachojengeka miongoni mwa wachina kuwa ukitaka kuua, nenda Tanzania....(lakini sijui naye yule jamaa aliyemkanyaga na kreni mchina aliyekuwa anawafuatilia kuwa wameiba diseli kesi yake ilienda kuamuliwa ubalozini?)

sasa ni nani alaumiwe kwa matukio ya ukwapuaji miongoni mwa watanzania katika makampuni ya kigeni?

a.ni tabia ya kuzaliwa (asili - urithi wetu)?

b.ni mikataba mibovu inayofanyika miongoni mwa wakubwa na kutoa bora ajira na sio ajira bora??? hivyo inaishia kuonyesha uchumi unakua?

c. ni katabia ka uvivu na uzembe miongoni mwetu kama watanzania na hivyo kukimbikia njia mkato?

 
At Thursday 9 February 2006 at 11:23:00 GMT, Blogger Kaka Poli said...

Hili igizo limenipa mwanga anuai juu ya matukio kama haya yaliyo ya kweli lakini ili mimi na wewe tuelewe kimantiki kaka ameliweka katika mtindo wa igizo na mimi ninaomba kuliweka igizo hili kama lilivyo kwanza kwenye blgou yangu kwa sababu inasomwa na wafanyakazi wenzangu haoa kituo cha sheria na haki za binadamu na wanaharakati kadhaa wa haki za binadamu ndani na nje ya Tanzania. pili Nitaomba nilitume kwa barua pepe kwa watu wote ninaowafahamu.

 
At Thursday 9 February 2006 at 16:17:00 GMT, Blogger NNYAMUNDU said...

SEHEMU YA 1
Hii yaonesha Sisi watanzania atupendani au kwamba UTU umetuishia kabisa.
SEHEMU YA 2
Wajinga si kwa kupenda mabaya tu hata kwa kutokana mazuri.
SEHEMU YA 3
Bado hatujajitambua kama tunastahili heshima popote pale kama watu na kama Taifa(HATUNA UTAIFA)
SEHEMU YA 4
Wachache wetu wanajitambua kama binadamu na wana UTU;lakini jamii haitaki kuwapa nguvu ya kutimiza FIKRA zao na hasa hasa vyombo vya dola au nisema Watu waotuongoza kama kweli au neno linatumika kimakosa --viongozi!(Viongozi wenye uzalendo)na wanapewa vyeo tofauti na AKILI ZAO,NGUVU ZAO , UTU WAO NA WAMAWAZO YAO.

naomba soma.SISI WAVIVU? http://bhalezee.blogspot.com

 
At Wednesday 22 February 2006 at 19:32:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Mkulu MtiMkubwa Tungaraza, Ujumbe huu kiboko, natumaini nitakapoongea nawe, itabidi tulizungumzie hili kwa kirefu.
Dennis Londo

 
At Tuesday 28 November 2006 at 23:45:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Kweli, inavutia; inasikitisha na inafikirisha. Matukio ya kweli ya aina hii ni mengi. Si ajabu Mti Mkubwa alishuhudia mojawapo, likampa hamasa na kwa ubunifu wake akatupatia igizi hili. Ashukuriwe!

Hao tunaowazungumzia - walioishiwa utaifa na uzalendo - ndio hao hao wanaojivunia miaka 45 ya uhuru. Uhuru wa kuwa hivyo!

Na wakubwa wetu, watawala wanaojiita viongozi, wanahusika sana katika kuua tunu hizo. Sasa tumebaki kusikia neno 'uzalendo' likitumika kwenye michezo na sanaa. Hivi ni kwa kuwa tunaongozwa na wasanii?

 

Post a Comment

<< Home