24 January 2006

Hadi lini Wachina wataendelea hivi?..MtiMkubwa ahoji...

Watanzania wenzangu,

Miezi kadhaa iliyopita niliwatumieni taarifa niliyoinukuu kutoka katika gazeti la Nipashe iliyokuwa na kichwa cha habari "..Mchina Amtwanga Hedi Mbongo na Kuzirai.." Leo swahiba wangu Dennis Londo kanitumia habari nyingine kama hiyo lakini sasa ni ya mauaji.

Habari kamili hiyo hapo chini:


Mchina mbaroni kwa mauaji ya mfanyakazi mwenzake Mtanzania Ni katika mradi wa maji ya Ziwa Victoria Na Anthony Komanya, ShinyangaMCHINA anashikiliwa na polisi mkoani Shinyanga kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mfanyakazi mwenzake Mtanzania.Raia huyo China, Yuan Yan Bin (42), mfanyakazi wa Shirika la China Civil Construction Corporation, anatuhumiwa kusababisha kifo cha mfanyakazi mwenzake kwa kumgonga na gari kwa makusudi Jumanne iliyopita, akimtuhumu kwa wizi wa dizeli.Kaimu Kamanda wa polisi mkoani wa Shinyanga , Karibueli Shoo, amemtaja aliyefariki kwa kugongwa na gari kuwa ni Benson Msengi (28) aliyekuwa ameajiriwa na shirika hilo, akiwa dereva wa tingatinga la uchimbaji.Shoo alisema Yan Bin, ambaye hivi sasa amelazwa katika hospitali ya mkoa akiongezewa maji kwa njia ya dripu, atafikishwa mahakamani baada ya upelelezi kukamilika.Habari kutoka kwenye eneo la tukio zilizotolewa na baadhi ya wafanzakazi wa shirika hilo walioshuhudia tukio hilo, zinadai kuwa raia huyo wa China, akiwa na wafanyakazi wengine, siku hiyo walimshambulia Msengi kwa kumpiga nondo baada ya kumtuhumu kuiba dizeli.Mmoja wa wafanyakazi ambaye amekwishatoa maelezo polisi, lakini hakutaka jina lake litajwe, alidai na yeye alishambuliwa na watu hao alipojaribu kumsaidia marehemu wasiendelee kumtesa.Alidai baada ya kumpiga sana, Wachina hao walimfunga marehemu kamba mikono kwa nyuma, wakamtupa kwenye gari Nissan ‘pickup’ na kuelekea kwenye kambi kuu, karibu na mjini Shinyanga.Mwingine anayesemekana kushuhudia tukio siku hiyo ni katibu wa mkoa wa chama cha wafanyakazi katika shirika la STAMICO, Simon Kafula, ambaye alikuwa hapo kambini kwa masuala ya wafanyakazi.Kafula anadai aliona Yan Bin alivyoendesha na kumgonga kwa makusudi marehemu akiwa bado amefungwa kamba walipowasili kwenye kambi hiyo ya Lubaga.Polisi jana ilithibitisha pia kwamba Kafula amekwishatoa maelezo kituo cha polisi mjini hapa.Baadhi ya wafanyakazi, wakielezea chanzo cha tukio, wamedai siku hiyo wakiwa kwenye Mlima wa Old Shinyanga, panapojengwa tanki kuu la maji ya mradi wa kufikisha maji Shinyanga, walionekana watu wawili kwa mbali wakiwa na madumu ndipo inadaiwa Yan Bin aliagiza wafanyakazi, akiwemo Msengi, kuwakimbilia watu hao.Hata hivyo, watu hao walifanikiwa kutoweka wakiacha madumu mawili matupu nyuma ambayo wafanyakazi hao, akiwemo Msengi, waliyapeleka kwa Yan Bin.Mmoja wafanyakazi hao alidai Msengi alipokwenda kukabidhi funguo za tingatinga kwa Yan Bin ili aende kupata chakula cha mchana ndipo alipoanza kushambuliwa.Inadaiwa Yan Bin alianza kumshambulia kwa kumpiga na nondo sehemu mbalimbali za mwili na kuungwa mkono na Wachina wenzake wapatao sita ambao walimshambulia kwa kutumia mipini ya sepetu na koreo.Inasemekana mmoja wa wafanyakazi alijaribu kumsaidia marehemu, lakini akajikuta anashambuliwa na Wachina hao na kufukuzwa asitoe msaada mpaka walipomweka ndani ya gari na hatimaye kufariki dunia

5 Comments:

At Tuesday, 24 January 2006 at 18:25:00 GMT, Blogger boniphace said...

Damija tutaacha lini ubaguzi wa rangi katika habari zetu. Kwa kuwa tunanyanyaswa basi na sisi tunaona suluhisho ni kujumuika na harakati zinazohamasisha rangi, utaifa, ukabila nk. Kwani akitajwa jina huyo kwa kuua haitoshi. Nini implication ya MCHINA AUA MTANZANIA? Mbona hawaandiki POLISI MTANZANIA AUA MTANZANIA MWENZAKE?

FIKRA hizi zanikumbusha kukosekana kwa Mwalimu Nyerere. Kumbuka namna alivyokuwa akipinga fikra za Afrika Kusini Waafrika kuchukia wazungu huku wao pia wakiuana? Tubadilike hasa tunaoufahamu ulimwengu katika kuhamasisha katika maandishi yetu habari hizi. Kwani Wachina ndio wameumbwa kutoua au waafrika ndio wameumbwa kuua? Ni tafakari na falsafa yake inachukua wakati kuipatia jawabu sawia.

 
At Thursday, 26 January 2006 at 04:28:00 GMT, Blogger Jeff Msangi said...

Damija,
Niliisoma habari hii nikasikia uchungu wa ajabu.Nikawa kama natazama ile filamu ya Time To Kill.Nikaona kama niliyoyaona kwenye Sarafina pale yule jamaa alikamatishwa mbwa.Majuzi nimetoka kuangalia documentary moja inaitwa Darwin's Nightmare,inahusu kanda ya ziwa Victoria na biashara ya samaki.Kuna mzungu alimuua dada yetu mmoja anaitwa Eliza ambaye alikuwa ni changudoa.Hivi visa vinazidi kuwa vingi na sioni hatua zozote za maana zikichukuliwa.Hivi vyombo vya usalama viko wapi?

 
At Thursday, 26 January 2006 at 15:51:00 GMT, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

pengine huko kwao msamiati wizi haupo, na mwizi ni msaliti huuwawa.....wanatafsiri hivyo hivyo na huku kwetu....wataalamu wa mambo ya wachina watatuelimisha!

 
At Monday, 6 February 2006 at 09:39:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Mayo wane Mija!

Ngoja nikutengenezee onyesho la hilo tukio lilivyokuwa:

SEHEMU YA KWANZA:
Mchina mfupi, mdogo kwa umbo, na sura yake kama paka anaonekana anamkimbiza Mtanzania. Mtanzania anakimbia kwa mbio zake zote huku anageukageuka nyuma kuangalia kama atadakwa. Mchina anaongeza kasi. Mtanzania maskini wa MUNGU kasi inapungua kadri anavyozidi kukimbia. Hatimaye Mchina anamkamata Mtanzania.
Wakati huo huo wa kumkimbiza Watanzania wengine wanakimbilia nyuma. Siyo kwamba wanakimbilia kumdhibiti Mchina isipokuwa wanakimbilia kuona kibano atakachopewa Mtanzania na Mchina.

SEHEMU YA PILI:
Mchina kamkamata mwizi wake (Mtanzania). Wote wawili wanahema kwa nguvu kwa sababu ya kukimbia. Mchina anamkunja shati Mtanzania. Watanzania wengine wamefika kwenye tukio wanasubiri kuona cha mtema kuni atakachokipata Mtanzania mwenzao. Mchina anaanza shughuli ya kumuadabisha Mtanzania kwa vibao. Kwa kila kibao anachopokea Mtanzania analia "..mama!.." "..ang'i!.." "..mama!.."
Wakati huo Watanzania wengine wanashabikia "..Kula eeeh.." "..kula eeeh.." "..k...mae wallai Wachina siyo mchezo cheki anavyopiga kunfuu.." Mchina anaona anaumiza mkono wake kwa sababu jamaa ni sugu sana anachukua chuma anaanza kumbonda nalo kichwani kama anaua nyoka. Mtanzania damu zinamchuruzika kwa majeraha. Watanzania wengine wanaacha kuangalia wengine wanaangalia huku wakisema "..Mchina akikasirika hatari.." "..hawa jamaa huwa hawaongei lakini 'usiwauzi'..Maanake wakikasirika jasho litakutoka.." Mchina anaendelea kubonda kichwa na nondo. Paa la uso linapasuka. Mtanzania sasa halii tena bali anaguna tu kila pigo la nondo likitua "..mmgh.." Pigo jingine "..mmmgh.." na jingine tena "..mmgh.." na jingine tena "..mmgh.." na jingine tena hakuna sauti inayotoka Mtanzania kishapoteza fahamu. Mikono, viatu na nguo za Mchina vimetapakaa damu ya Mtanzania. Mchina anamuangalia mtuhumiwa wake anaridhika na kisago alichompa.

ONYESHO LA TATU
Mchina na wenziye wanachumpa ndani ya gari yao kwenda kunawa na kubadilisha nguo. Watanzania waliokuwepo kwenye tukio wanaondoka wasije wakakutwa na polisi wakatakiwa kutoa ushahidi. "..haroo, yaani yule Mchina arikuwa kakasirika bwana..Maanake arikuwa anampiga kwa nguvu kama nini.." "..Mshikaji tukijikate mandata wasije wakatukuta hapa tukaitwa kwenye ushahidi.." "..Lakini jamaa kajitakia mwenyewe sasa kwa nini aliiba?.." ".unajua mimi nilianza kuwaona tangu wanamkimbiza, nikajua tu leo jamaa ataipata.." "..Hivi arifikiri anaweza kumshinda mbio Mchina..Wachina wanafanya mazoezi ware tangu wadogo.." "..Mimi nirikuwaga nawaonaga wakati wanajenga reri ya tazala, tujamaa tudogo rakini tunabeba mataruma ya reli kama kanabeba rura ya kupigia mistari.."

ONYESHO LA NNE
Mtanzania mmoja mzalendo aliyekereheshwa na kitendo kizima anakwenda kuita polisi baada ya tukio kuisha. Polisi wanakuja na mwandishi wa habari mmoja. Polisi wanampinduapindua maiti. Halafu wanawaamrisha watu "..Hebu sogeeni mbali mnatunyima nafasi.." Polisi mmoja anachapa chapa virungu watu wanasogea mbali kidogo. Wengi wa watazamaji wa tukio ni wanaume vijana na watoto wadogo. Watoto wengine wanamtazama maiti huku macho yamewatoka kama wanatazama sinema ya dracula. Polisi wanampindua marehemu kutoa kitambulisho mfukoni ili kumjua jina lake. Kwa bahati nzuri ana kitambulisho. Wamemtambua jina. Halafu wanampasia mwandishi wa habari kitambulisho. Mwandishi anachukua jina halafu anamrudishia ofisa. Maiti anaokotwa anawekwa nyuma ya Land Rover anapelekwa hospitali. Watanzania wanatawanyika. Eneo la tukio linaachwa na damu halafu polisi wamesahau kuokota nondo iliyotumika kumpigia marehemu. Msamaria mwema anaiokota anaitupa jalalani huku akisema "..Isije ikaua mwingine.."

MWISHO
Mchina anapigiwa simu aende kituoni akatoe maelezo ya tukio. Kituo yupo ofisa upelelezi kesi za jinai. Kiingereza chake siyo kizuri sana kwa hiyo stetimenti ataiandika Kopla Masanja kwa sababu anaongea Kiingereza kizuri zaidi. Mchina anafika kituoni masaa kadhaa baada ya tukio. Stetimenti inaandikwa. Mchina anaambiwa itabidi alale ndani jioni ya leo. Baada ya siku mbili tatu suala linakuwa kati ya Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Ubalozi wa China nchini Tanzania. Kwa sababu za kidiplomasia Mchina anakuwa 'dipotedi' Kesi imekwisha.

Mayo wane, hivi sivyo inavyokuwa? Kama nimekosea kutengeneza onyesho niambieni! Sawa?

F MtiMkubwa Tungaraza.

 
At Saturday, 4 March 2006 at 20:02:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Fide,

Naona bado kipawa cha kutoa hadithi maskani unacho. Hii ni Shekispia material, trajedi, sasa fanya bidii uitoe kwa urefu katika kitabu kama vilie vijitabu vya kijiji chetu ili kitumike mashuleni na kufundisha watu kuwa waamuzi na si mashabiki wa uangamizi.

Babakulu-Dan Nkurlu

 

Post a Comment

<< Home