Bi Kidude.
Ingawa anajulikana zaidi kwa jina la Bi Kidude, lakini jina lake halisi ni Fatuma binti Baraka. Bi Kidude ni msanii mkongwe na mahiri sana katika fani ya muziki, hususani muziki wa mwambao ambao hujulikana kwa jina la Taarabu. Muziki huu ambao asili yake ni Misri umekita sana katika mwambao wa Afrika Mashariki yaani Zanzibar, Mombasa, Lamu na kwingineko.
Fatuma binti Baraka au Bi Kidude, alizaliwa katika kijiji cha Mfagimarigo Tanzania visiwani Zanzibar katika familia ya watoto saba (7), Baba yake Mzee Baraka alikuwa ni mfanya biashara wa nazi zao ambalo ni la kutumainiwa sana Zanzibar. Bi Kidude anasema hafahamu tarehe halisi aliyozaliwa, isipokuwa anachojua ni kwamba alizaliwa wakati rupia ikitumika kama fedha, na vilevile anahakika ni kabla ya vita kuu ya kwanza ya dunia. Wataalamu wa mahesabu baada ya kupata taarifa hizo wakampigia mahesabu na kumkabidhi miaka yake kwamba ni zaidi ya miaka tisini (90).
Bi Kidude anasema uimbaji aliuanza tangu alipokuwa na umri wa miaka kumi (10) na alijifunza kutoka kwa Msanii mkongwe na aliyetamba sana enzi hizo Sitti binti Saad. Anasema wageni wengi kutoka sehemu mbalimbali walikuwa wakifika Zanzibar kuja kumwona Sitti, na kwa vile Bi Kidude na Sitti walikuwa wako karibu basi yeye alikuwa akiwapeleka wageni wale Nyumbani kwa Bi Sitti, wakifika huko wageni walikuwa wakiingia ndani na yeye kubakia nje, kule ndani Bi Sitti alikuwa akiwaimbia wale wageni, na yeye huku nje alikuwa akimsikiliza kwa makini na kumfuatiza jinsi alivyokuwa akiimba. Aliendelea hivyo hadi akawa mahiri sana katika uimbaji.
Alipokuwa na miaka 13, kwa mara ya kwanza alitoroka nyumbani kwao Zanzibar na kukimbilia Tanzania bara, baada ya kulazimishwa kuolewa. Lakini alipokuwa kigoli wa kutosha kuolewa aliolewa ingawa ndoa hiyo nayo haikudumu kutokana na manyanyaso aliyokuwa akiyapata, hivyo aliamua kukimbilia kaskazini mwa Misri ikiwa ni katika miaka ya 1930, huko aling'ara sana katika fani yake ya uimbaji na uchezaji ngoma. Lakini ilipofika miaka ya 1940 aliamua kurudi nyumbani Zanzibar ambako aliendelea na shughuli zake uimbaji.
Bi Kidude hategemei kazi moja tu ya kuimba, pia ni mfanya biashara ya 'Wanja' na 'hina' ambavyo anavitengeneza yeye mwenyewe, pia ni mtaalamu wa matibabu kwa dawa za mitishamba na zaidi ya hayo ni Mwalimu mzuri sana wa 'Unyago' ameanzisha chuo chake mwenyewe na anasema katika wanafunzi wake wote hakuna aliyepata talaka kutoka kwa mumewe.
Watu wanasema 'Utu uzima dawa' Bi Kidude ana upeo mkubwa sana wa akili kwani pamoja na kukulia katika mazingira yaliyogubikwa na tamaduni za kiarabu ambapo mwanamke anatakiwa wakati wote akiwa hadharani ajifunike, Bi Kidude aliliona hili katika upeo mwingine kwamba ni sheria tu ya kitamaduni toka arabuni, hivyo aliamua kuvunja sheria hiyo na kuondoa hijabu mwilini mwake, na sasa hivi anavaa kama Mtanzania na si kama mwarabu. Lakini hakubakia hapo alivunja na miiko mingine zaidi ya kutokunywa na kuvuta, Bi Kidude anakata maji kisawasawa na kuvuta tumbaku na jani, lakini pamoja na yote hayo bado sauti yake iko pale pale.
Amekwisha tembelea nchi nyingi sana ikiwa ni pamoja na Oman, Ufaransa, Hispania, Ufini, Ujerumani na Uingereza.
Amekwisha pata tuzo mbalimbali ikiwa ni pamoja na ile ya Tamasha la filamu ya nchi za Jahazi (ZIFF) mwaka 1999 tuzo ni ya maisha. Pia mwaka jana tuzo ya WOMAX ilienda kwake.
Nyimbo alizowahi kuimba ni pamoja na Muhogo wa jang'ombe, na anaimba kwa kiswahili na Kiarabu. Hakuwahi kupata elimu nyingine zaidi ya Koran.
Kwa mahojiano msikilize hapa.
Mungu azidi kumpa maisha marefu bibi yetu.
11 Comments:
Ahsante sana kwa habari hii juu ya gwiji Bi.Kidude.Watu kama hawa ni lazima tuwaenzi sana kwa sababu wanatusaidia kuandika historia yetu vizuri na sio kama "wageni" wanavyotaka iandikwe.
Taarifa imenielimisha. Ahsante
Kwa mda mfupi niliokaa zanzibar nimefanikiwa kumfahamu sana bibi huyu ila kinachonisikitisha ni wajanja wachache wanaotumia mgongo wake kujipatia mamilion wakijidai wao ni mapromota kumbe wezi tupu!!
makazi anayoishi bibi huyu nathubutu kusema hastahili kuishi ukilinganisha na vipato anavyopaswa kupata katika matamasha mbalimbali ya ndani na nje ya nchi katika bara la ulaya.
FIKRA THABITI,
ndio tanzania ambayo ninaipigia kelele kila kukicha ambayo watu wanaofanya kazi hawali na wasiofanyakazi wanakula. inabidi sasa kuanza kupigia kelele haya mambo!
Da Mija, umefanya jambo la mbolea sana kuandika kuhusu huyu gwiji wa muziki na utamaduni Afrika (sio Tanzania tu). Ukitazama umri wake na mambo anayofanya jukwaani huwezi amini (najua jani na mitishamba mingine anayokula vinamsaidia!). Kazi safi sana hii kutuelimisha juu ya watu wetu. Unatufanya kuwa na kila sababu ya kutukuza utamaduni wetu na kuenzi watu kama hawa.
Makala yako kuhusu Bi Kidude nimeitumia kwenye kamusi elezo huria (wikipedia). Itazame hapa: http://sw.wikipedia.org/wiki/Bi_Kidude
Nashukuru Ka'Ndesanjo! Ngoja niitizame.
Nice stuff
Habari hii imenisisimua. Tuna mengi ya kujifunza kwa bibi Kidude.
Da mija!
mbona hujasema? nasikia huyu huwaga anapuliza na sigara kubwa!
ombi lako nitalifanyia kazi!
cheers!
si kweli, mark! anapuliza embasi na anagida safari, nnao ushahidi wa picha za juzi kwenye sauti za busara. da mija nimependa makala yako.ukitaka picha latesti nambie, nnazo kibao
Post a Comment
<< Home