22 January 2006

Siti binti Saadi.


Kama isivyowezekana kutenganisha kalamu na wino, basi ndivyo isivyowezekana kumtenganisha Siti binti Saadi na muziki wa Taarabu.

Siti binti Saadi alizaliwa katika kijiji cha FumbaTanzania visiwani 'Zanzibari' mwaka 1880. Alipozaliwa alipewa jina la 'Mtumwa' hii ni kwa vile alizaliwa katika kipindi cha utumwa wa kiarabu. Jina la Siti alipewa na mkabaila mmoja wa kiarabu likiwa linamaanisha 'Lady' kwa kiingereza.

Baba yake bwana Saadi alikuwa ni Mnyamwezi kutoka Tabora na mama yake alikuwa ni Mzigua toka Tanga, lakini wote wawili walizaliwa Zanzibari. Hali ya maisha ya familia yao ilikuwa ni duni sana na walijishughulisha zaidi katika shughuli za kilimo na ufinyanzi kazi ambazo Siti alijifunza na kuzimudu vizuri pia.

Kama waswahili wasemavyo 'kuzaliwa masikini si kufa masikini' Siti alibarikiwa kuwa na kipaji cha pekee cha uimbaji. Kipaji hiki kilimsaidia sana tangu siku za awali za maisha yake kwani alitumia uimbaji wake kuuza vyungu vya mama yake alivyokuwa akimsaidia kuvitembeza. Siti alipoimba sauti yake iliweza kupaa na kusafiri kwa umbali wa maili nyingi na hii ndio ilikuwa ishara ya watu kujua kwamba vyungu vya kina Mtumwa vinapita leo. Alifananishwa kuwa na mapafu yenye nguvu kama ya simba kutokana na alivyoweza kupaza sauti yake mbali na bila kuachia pumzi.

Kutokana na wakati huo elimu kwa watoto wa kike kutotiliwa mkazo, Siti hakuwahi kwenda shule wala kuhudhuria mafunzo ya Koran (madrasa). Hivyo mnamo mwaka 1911 aliona ni bora ahamie mjini ili kubooresha maisha yake zaidi. Ujio wake wa mjini ulikuwa wa neema kwani alikutana na bwana mmoja wa kundi la 'mziki wa Taarabu la "Nadi Ikhwani Safaa" aliyeitwa Muhsin Ali. Katika kipindi hicho hilo ndilo lilikuwa kundi pekee la muziki wa taarabu lililoanzishwa na Sultani mpenda starehe na anasa bwana Seyyid Barghash Said. Kundi hili lilikuwa ni la wanaume peke yake , wanawake hawakuruhusiwa kujiunga na vikundi vya muziki kwa vile ilikuwa ikichukuliwa kama ni uhuni. Bwana Muhsin alikiona kipaji cha pekee cha Siti na hivyo akajitolea kumfundisha kuimba kwa kufuata vyombo vya muziki na lugha ya kiarabu. Baada ya hapo alikwenda kumtambulisha kwa wanamuziki wenzie wa "Nadi Ikhwani Safaa" ambao bila kusita wakaanza kufanya naye maonyesho mbalimbali katika jamii. Walipata mialiko mingi hasa kutoka kwa Sultani na matajiri wengine wa Kiarabu, pia katika maharusi na sherehe zingine mbalimbali, inasemekana ulifika wakati ambapo sherehe ilishindwa kufana kama Siti binti Saadi hakuwepo kutumbuiza. Siti alikuwa ni moto wa kuotea mbali na jina lake lilivuma kwa haraka sana hadi nje ya mipaka ya nchi na bara la Afrika. Na punde Siti alianza kufananishwa na 'Umm Kulthum', mwimbaji mahiri wa kike aliyetamba wakati huo kutoka Misri.

Kama nilivyosema moto wa Siti ulikuwa si wa kuusogelea karibu, mwaka 1928 kampuni ya kurekodi muziki ya 'Culumbia and His Master's voice' yenye makazi yake Mumbai India ilisikia umaarufu wa Siti binti Saadi na hivyo ikamwalika yeye pamoja na kundi lake kwenda kurekodi kwa lugha ya Kiswahili ili kujaribu kama muziki wake utauzika. Kampuni ile haikuweza kuamini jinsi muziki ule ulivyouzika kwa kasi kubwa kwani wastani wa santuri 900 ziliweza kuuzika katika kipindi cha miaka miwili ya mwanzo, na hadi kufikia 1931 santuri 72,000 zilikuwa zimeuzwa. Kutokana na kusambaa kwa santuri hizi, umaarufu wa Siti ulizidi mara dufu watu kutoka sehemu mbalimbali za dunia walikuwa wakija Zanzibari kuja kumwona. Mambo yalizidi kuwa mazuri kwa Siti hadi ikafikia hatua kampuni ya kurekodi ya Columbia kuamua kujenga studio ya kurekodi muziki palepale Zanzibar maalumu kwa ajili ya Siti binti Saadi.

Hatua hiyo ya hadi kujengewa studio iliwaumiza wengi wenye wivu, hivyo wakaanza kumtungia nyimbo za kumkejeli ili kumshusha na hasa walitumia kigezo kwamba hana uzuri wa sura, nyimbo nyingi ziliimbwa lakini huu ndio uliovuma sana:-
  • Siti binti Saadi kawa mtu lini,
  • Kaja mjini na kaniki chini,
  • Kama si sauti angekula nini?

Na yeye kwa kujua hila za wabaya wake, akaona isiwe taabu akajibu shambulio namna hii:-

  • Si hoja uzuri,
  • Na sura jamali,
  • Kuwa mtukufu,
  • Na jadi kebeli,
  • Hasara ya mtu,
  • Kukosa akili.

Kwa kujibu shambulio hilo kwa namna yake aliwafunga midomo wale wote waliokuwa wakifuata fuata. Siti pia alikuwa ni mwanamke wa kwanza mwanaharakati katika kipindi chake, alitetea wanawake na wanyonge kwa ujumla, kwani katika kipindi chake watu matajiri walikuwa wakiwaonea masikini na walipofikishwa mbele ya haki waliweza kutoa hongo na kuachiwa huru halafu wewe uliyeshitaki ndiye unayefungwa.

Utunzi wake wa wimbi wa Kijiti ulimpatia sifa kubwa kwani ulikuwa ukielezea kisa cha kweli kilichomkuta mwanamke mmoja mgeni kutoka bara, mwanamke huyu alipofika alikutana na Tajiri mmoja ambaye alijifanya amempenda, hivyo akamchukua na kulala naye halafu baadaye akamuua. Tajiri yule alishitakiwa na bahati nzuri walikuwepo mashahidi wawili walioshuhudia tukio lile, lakini kwa vile ni Tajiri alitoa pesa na kesi ikawageukia wale mashahidi na kufungwa.

Siti akatoa wimbo huu :-

  • Tazameni tazameni,
  • Eti alofanya Kijiti,
  • Kumchukua mgeni,
  • Kumcheza foliti,
  • Kenda naye maguguni,
  • Kamrejesha maiti.

    Siti aliendelea kumwambia katika nyimbo zake kwamba asijethubutu kwenda Dar er Salaam kwa maana watu wenye hasira wanamsubiri na wameapa kwa ajili yake.

    Siti aliendelea na shughuli yake ya muziki hadi uzeeni, muda mfupi kabla ya kifo chake alikutana na mwandishi maarufu na mwanamashairi Shaaban Robert ambaye alimhoji na kuweza kuandika wasifu wake katika kitabu alichokiita " Wasifu wa Siti binti Saadi" wasifu unaosemekana kuwa ndio bora zaidi uliowahi kuandikwa katika fasihi ya Tanzania. Kitabu hiki kinatumika kufundishia shule za sekondari za Tanzania.

    Tarehe 8/7/1950 Siti binti Saadi alifariki dunia na kuacha pengo kubwa katika fani ya Taarabu. Ingawa pengo hilo haliwezi kuzibika lakini kuna watu wengi walioweza kuibuka na umaarufu wa kuimba taarabu kupitia kwake, mfano hai ni Bi Kidude.

    Hata baada ya kifo chake jina lake bado linatumika sana kama kielelezo cha ushujaa wake, Chama cha waandishi wa habari wanawake Tanzania, kimetumia jina lake kulipa jina gazeti la chama chao "Sauti ya Siti". Hadi leo hii Siti hutumika kama kipimo cha kufundishia uimbaji wa Taarabu. Na anakumbukwa katika historia yake ya kuwa mwanamke wa kwanza Afrika mashariki kurekodi muziki katika santuri.

    6 Comments:

    At Tuesday 24 January 2006 at 12:35:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

    Asante Mija. Unajua TAMWA wana jarida linaitwa Sauti ya Siti. Watu wengi wamekuwa wakidhani kuwa jarida hilo limepewa jina kwa heshima ya mke wa Mzee Ruksa Ali Mwinyi, Mama Sitti. Kumbe ni heshima ya huyu kinara wa muziki Afrika. Fikiria kuna wanamuziki wanajitahidi kutafuta namna ya kurekodi muziki wao leo 2006 wakati Siti alirekodi mwaka 1928! Tena Indiaaaaa. nadhani pia watu wengi hawamfahamu Uum Kulthum kwahiyo Siti anapolinganishwa naye inakuwa vigumu kuelewa jinsi gani ilivyo sifa kulinganishwa na huyu "miriam makeba" wa Misri.
    Nitabeba baadhi ya mambo uliyoandika hapa na kuanzisha ukurasa wa Siti kwenye kamusi elezo yetu ya Kiswahili.

     
    At Thursday 26 January 2006 at 15:42:00 GMT, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

    da mija hapa umenikuna kweli!! si ndio huyu aliimba subhakleri mpenzi waonaje hali yako...alikuwa na nani vile salum abdallah?

     
    At Thursday 26 January 2006 at 15:48:00 GMT, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

    kha mija, hebu tuambie yaani ina mana toka wakati huo hakuna tena mwanamuziki wa bongo aliyesaini na makampuni makubwa kama columbia records? kama waliweza wakati huo wa siti ni nini kinawashinda kuja warekodi msondo ngoma? haya ndio mambo ya kuyavalia njuga kwa kasi kuu!! ni ukombozi kwa wasanii......maana hao wakiingia bongo wahindi wetu yatawakuta yaliyomkuta iddi simba alipopambana na illovo sugar!

     
    At Friday 27 January 2006 at 14:12:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

    Nitatumia baadhi ya uliyoandika hapa kwenye ukurasa wa Siti kwenye kamusi elezo ya Kiswahili: http://sw.wikipedia.org

    Poa sana kwa sana.

     
    At Tuesday 7 March 2006 at 18:59:00 GMT, Blogger Chemi Che-Mponda said...

    This comment has been removed by a blog administrator.

     
    At Tuesday 7 March 2006 at 19:03:00 GMT, Blogger Chemi Che-Mponda said...

    Asante Da'Mija Shija Sayi,

    Kumbe na wewe un interest na Bibi Siti.

    Kuna habari zaidi kuhusu Bibi Siti kwenye site yangu:

    http://groups.msn.com/SitiBintiSaad

    Pia, kama kuna mtu ambaye anajua wapi tunaweza kupata cassette/CD au santuri za nyimbo zake, atuelekeze.

    7:59 PM

     

    Post a Comment

    << Home