23 December 2005

Viti Maalumu ...

Jamani sijui kama na wenzangu mnaliona hili, binafsi ninaona kuna njama za chini kwa chini zinazofanywa na wanaume kuwazima kabisa wanawake katika harakati za ukombozi. Kumkamilishia mtu mahitaji yake ni kumfanya mtu asipambane, na bila mapambano hakuna ushindi, ushindi utabaki kwa yule anayekupigania. Hii tabia ya kutoa viti maalumu kwa wabunge wanawake inatufanya tusiwajibike ipasavyo na kubakia pale pale. Viti hivi vilitakiwa vipiganiwe ili utakapokipata ujue kweli jinsi ya kukifanyia kazi na kukiwajibikia. Hii tabia ya kupewa-pewa ina mambo mengi ambayo wanawake tunatakiwa tuyajue...Kupewa kwa aina yoyote ile kunaendana na kulipa fadhira, kwa hiyo kupewa huku kwa viti maalum tusikuchukulie juu juu, wabunge hawa wajiandae kupangiwa ya kufanya na kuwekewa mipaka ya kufika. Na kama ukitaka kwenda kinyume na mipaka hiyo basi utakumbushwa jinsi ulivyokipata kiti, kwa hiyo itabidi ukubali yaishe.

Sasa wenzangu hali hii kweli itatufikisha tuendako? ..hili nalo ni lazima tulifanyie kazi. Wabunge wenyewe waliotangazwa hawa hapa chini.

2005-12-23 08:32:50
Na Mwandishi wetu.


Tume ya Taifa ya Uchaguzi, imewatangaza rasmi wanawake 64 wa Vyama vya CCM na CHADEMA kuwa wabunge wa viti maalum.
Wabunge 58 miongoni mwa hao ni wa CCM na wengine sita ni wa CHADEMA.

Hata hivyo taarifa ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, ilisema tume imeshindwa kutangaza wabunge maalum kupitia chama cha CUF kwa sababu chama hicho hakijawasilisha majina.

Taarifa hiyo iliwataja wabunge wa viti maalum kupitia CCM kuwa ni Bi Anna Magreth Abdallah, Bi Faida Mohamed Bakari, Bi Martha Jachumbulla, Bi Elizabeth Nkunda Batenga, Bi Zainabu Matitu Vulu na Bi Cynthia Hilda Ngoye.

Wengine ni Bi Esther Kabadi Nyawazwa, Bi Mariam Salum Mfaki, Bi Anastazia James Wambura, Bi Gaudensia Mugosi Kabaka, Bi Sijapata Fadhili Nkayamba, Dk. Aisha Omari Kigoda, Bi. Salome Joseph Mbatia na Dk Lucy Sawere Nkya.

Hali kadhalika Bi Joyce Nhamanilo Machimu, Bi Eliata Ndumpe Switi, Bi Lediana Mafuru Mng’ong’o, Bi Diana Nkumbo Chilolo, Dk Batilda Salha Burian, Bi Asha Mshimba Jecha na Bi Fatma Othman Ali.

Katika orodha hiyo ya wabunge wa CCM pia kuna Bi Devota Mkuwa Likokola, Bi Bahati Ali Abeid, Dk Maua Abeid Daftari, Bi Fatma ABdallah Mikidadi, Bi Janet Bina Kahama, Bi Aziza Sleyum Ally, Dk Asha-Rose Migiro, Bi Shamsa Selengia Mwangunga, Bi Margreth Agnes Mkanga, Bi Zuleikha Yunus Haji na Bi Lucy Thomas Mayenga.

Wengine ni Bi Amina Chifupa Mpakanjia, Bi. Margreth Simwanza Sitta, Bi Felista Aloyce Bura, Bi Halima Mohamed Mamuya, Bi. Rosemary Kasimbi Kirigini, Bi Mwanne Ismail Mchemba, Bi Anna Richard Lupembe, Bi Halima Omari Kimbau, Bi Dorah Herial Mushi na Bi Mwantumu Bakari Mahiza.

Wabunge wengi wa CCM wa viti maalum vya wanawake ni Bi. Riziki Lulida Said, Bi Mariam Reuben Kasembe, Bi Mwanakhamis Kassim Said, Bi. Janeth Mourice Massaburi, Bi Benadetha Kasabogo Mushashu, Bi. Maida Hamadi Abdallah, Bi Mwaka Abdulrahman Mbaraka, Bi Kumbwa Makame Mbaraka, Bi Joyce Martin Masunga, Bi Josephine Johnson Ngenzobuke, Bi Kidawa Hamid Salehe, Bi Martha Moses Mlata, Bi Shally Joseph Raymond, Bi Maria Ibeshi Hewa, Bi Pindi Hazara Chana na Bi Stella Martin Manyanya.

Kwa upande wa CHADEMA waliotangazwa kuwa wabunge wa viti maalum vya wanawake ni Bi Grace Sindato Kiwelu, Bi Maulidah Anna Komu, Bi Mhonga Said Ruhwanya, Bi Lucy Fidelis Owenye, Bi Susana Anselm Jerome Lyimo na Bi Halima James Mdee
Kuhusu wabunge wa CUF Tume ya Taifa ya Uchaguzi imesema imechukua hatua za kukiomba chama hicho kuwasilisha majina.

’Baada ya CUF kuwasilisha majina na taratibu zinazotakiwakuzingatiwa Tume itawatangaza wabunge wa viti maalum kupitia chama cha CUF,’ilisema taarifa.

SOURCE

5 Comments:

At Tuesday 27 December 2005 at 10:07:00 GMT, Blogger Fikrathabiti said...

Dada miza nimependa makala yako ila napenda kutoa wito kwa wanablog wenzangu tuanze harakati za kusafisha nyumba za wanojiita wanaharakati wa haki za wanawake kwani nionavyo mimi wamepoteza muelekeo.

Nilijiuliza sana nilipomuona mama Senkoro akisimama mpweke majukwaani akiwa na visenti finyu akiomba ridhaa ya wananchi huku taasisi hizo kama TAMWA,TGNP zinazotetea maslahi ya wanawake wakikaa kimya bila ya kutoa msaada dhahiri kwa mwanamama huyo.

Au wanataka tuamini kua harakati zao zinawahusu akina mama wa chama tawala tu????Imebidi nihoji hivyo kwani kuna kipindi taasisi hizo zilipokua mstari wa mbele kuwashawishi akina Rose mogiro,Getrude mongela kujitokeza na kuwania kiti hicho!!!!!

Kwanini hali ilibadilika ghafla kwa Senkoro aliyevunja ukimya na uoga hatimaye kujitokeza na kuwatoa kimasomaso akina mama wa nchi yetu.

Dada Mija nadhani mjadala ungeanzia hapa.Nakuomba pia utembelee kibarazani kwangu nilichokibatiza jina la "FIKRATHABITI"

 
At Tuesday 27 December 2005 at 10:28:00 GMT, Blogger Innocent Kasyate said...

Bibie hizi ni harakati za ulaji binafsi tu.Ndio mifumo ya siku hizi hata tukisema sana wameziba masikio.Mimi nimechanganyikiwa, nafikiri tumekwisha.

 
At Tuesday 27 December 2005 at 10:54:00 GMT, Blogger Fikrathabiti said...

Da mija natoa ombi kwako unipe siri ya kuteuliwa tena kwa Grace sindato kwenye viti maalum kwa upande wa CHADEMA.Hivi unajua kua huyo mwanamama ni mkwe wa kigogo mmoja wa chama hicho ambaye pia ni mbunge wa Moshi mjini.Jee uwezo wake ulizingatiwa au ni nguvu za ushawishi alizonazo Mheshimiwa Ndesamburo ndani ya chama hicho?

 
At Wednesday 28 December 2005 at 08:50:00 GMT, Blogger Mija Shija Sayi said...

Nduguzanguni, hizi harakati za ukombozi wa mwanamke sasa zimekuwa ni Mradi. Watu wanapeana madaraka wenyewe kwa wenyewe, Kaka yangu FikraThabiti unajiuliza juu ya Bi Grace Sindato, na mimi hapa najiuliza juu ya Bi Rose Kirigini ambaye nilisoma naye baba yake alikuwa ni Mbunge, haya huyu Amina Chifupa naye baba yake ni mtu wa huko huko, Sikatai kwamba mtoto wa kiongozi basi asiwe kiongozi..laa! hasha... nataka mtoto huyo au mkwe huyo wa kiongozi awe na ari na uwezo wa kuongoza, na ili kiongozi wa namna hiyo umpate basi ni lazima yeye mwenyewe apiganie nafasi hiyo.

Halafu nimekuwa nikijiuliza hivi ni kwa nini hakuna viti maalumu kwa wanaume?..kama viti maalumu vilikuwa na ulazima sana wa kuwepo, basi wanaume nao walitakiwa kuwa navyo maana suala hili la Ubunge alitumii nguvu bali akili. Kuna kitu kimoja tunatakiwa tukijue wakati tukiendesha hizi harakati za usawa wa Mwanaume na Mwanamke, kwamba mwanamke ana nguvu ya akili na mwanaume ana nguvu ya akili na misuli. Kwa hiyo basi katika sekta zinazotumia akili wanawake hatuhitaji upendeleo hapo, ila katika sekta zinazotumia minguvunguvu hapo tunakaribisha upendeleo.

Kuna haja ya kujitambua kabla ya kabla ya kuanza jambo lolote, hii itatufanya tusiwe tunazolewa kiholela-holela.

 
At Wednesday 28 December 2005 at 16:42:00 GMT, Blogger Fikrathabiti said...

Unajua dada mija napenda kurudia kusisitiza hoja yangu ya kuanza kusafisha hizo taasisi za kina mama kwanza ili iwe njia kufikia huko tunapoomba tufike kwenye fursa sawa kwa wote.

Tatizo lililopo ni huu mfumo dume(PATRIACHY) na hali ya kubebana bila kuwapa changamoto za kusimama wao wenyewe.Lakini kiniumacho zaidi ni matumizi mabaya ya rasilimali wazipatazo toka kwa wafadhili.

Mimi kwasasa nipo Zanzibar ila nadhani itakua ni vizuri kama alivyosema brother Ndesanjo tukutane ana kwa ana tupange mikakati thabiti ya hizi harakati na sio kuishia tu blogun.

ALUTA CONTINUE!

 

Post a Comment

<< Home