16 December 2005

Kuhusu neno "Blog" kwa kiswahili.

Kwanza kabisa labda nianze hivi..."Jambo haliwi jambo hadi uliamuru kuwa jambo ndipo hugeuka kuwa jambo". Kwa kipindi sasa wanablogu tumekuwa tukijitahidi kutafuta neno blog kwa kiswahili ili kuendelea kuikuza lugha yetu. Lakini kwa bahati mbaya mbio hizi zimekuwa zikizorotazorota kutokana na sababu mbalimbali. Pamoja na sababu zote zinazozorotesha upatikanaji wa neno blog katika kiswahili, nimekuja kugungua kwamba iliyo kubwa kabisa ni hii.." Tumejifunga wenyewe"...kwamba tunatafuta maneno ambayo yapo tayari, na tena yanayoendana na maana halisi ya neno blog. Sikatai kwamba ni njia isiyofaa, lakini tukumbuke kwamba ..Fasihi yoyote huzaliwa, hukua, na hufa. Na kama ni hivyo basi kwa nini wanablogu tusizae neno letu wenyewe na sisi ndio tukaliamuru hilo neno kuwa na maana ya Blog kwa kiswahili, ila katika uzazi huo tuzingatie Kanuni za lugha, kwamba ni lazima liweze kutamkika vizuri katika nafsi ya kwanza, ya pili na ya tatu, na katika nyakati zote, wakati uliopo, uliopita na ujao.
Mfano neno NGWANGA. Hili neno halina maana yoyote, lakini kuanzia sasa ninaliamuru liwe na maana ya blog. Neno hili limetimia katika nafsi na nyakati za kiswahili.

Mfano... Ninaenda kungwanga.
.........Unaenda kungwanga.
.........Anaenda kungwanga.

Najua wasomaji bado mnasitasita, lakini hebu fikirieni majina ya vitu vilivyopo hapa ulimwenguni, je yanahusiana na maana ya vitu vyenyewe?? hapa ukubali usikubali jibu ni hapana. Na kama jibu lingekuwa ndiyo, basi vitu vyoote hapa duniani vingekuwa na jina moja.

Hakukuwa na ulazima wowote wa NYUMBA kuitwa nyumba, au kinu kuitwa kinu, au dunia kuitwa dunia au kitabu kuitwa kitabu. Ni watu walikaa na kuamua hiki kiitwe hivi na hiki vile. Na kama tunavyojua fikra hujenga taswira, baada ya neno Nyumba kuanza kutumika kuwakilisha jengo basi taswira nayo ikajengeka akilini..Nyumba ni jengo. Na ukienda kwa waingereza wenyewe jengo ni HOUSE.

Kwa hiyo kwa mtazamo wangu naona tusiendelee kupoteza muda, tupeane zoezi la kila mwanablogu kuleta maneno mawili mapya kabisa, halafu tutapiga kura na kuchagua moja.
Na kumaliza mchezo. Tukifanikiwa kulitekeleza hili tutakuwa na faraja kubwa kwani tutakuwa tumefanikiwa kuumba na kutia pumzi. Msangi Mkubwa ameianzisha tena mada hii, msome na usome maoni ya wengine.

17 Comments:

At Saturday, 17 December 2005 at 21:34:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

Kwanza kabisa nimependa sana hoja uliyoijenga kwamba jina la kitu halina uhusiano wowote na kitu chenyewe. Inamaanisha kuwa wazungumzaji wa kiswahili tukaamua mvua iitwe mawingu na mawingu yaitwe mvua hakuna jambo litakaloharibika. Neno "kiti" halina uhusiano wowote na kitu ambacho tunakiita "kiti." Ni makubaliano tu ya kijamii. Kama ulivyosema, majina/maneno ni sisi tumeyaunda na tukaamua yatumike namna fulani. Huu ni mwanzo mzuri maana wanaweza kuwepo watu wanaoamini kuwa maneno yameshushwa.

Tuje kwenye Ngangwa. Neno hili bado halijaniingia vizuri. Huenda ni kwasababu ni jipya kwangu. Huwezi kujua kesho nitafikiria nini. Naomba wanablogu wote tuweke neno hili kwenye blogu zetu na kuweka viungo kupeleka watu mahali hapa ulipojadili. Wakilipokea wengine, nami nitalipokea bila kusita. Hebu tulijadili, hapa na pia kwenye blogu zetu.

Asante kwa kudaka hoja ya Jeff. Jeff kafanya vizuri sana kutukumbusha jambo ambalo tuliliweka kando siku nyingi.

 
At Sunday, 18 December 2005 at 09:21:00 GMT, Blogger mwandani said...

Hoja nzuri Mija.
Masuala mengine ni uamuzi tu.

Naonelea vyema kama hoja zote hizi zingekusanywa pamoja ili iwe rahisi kuendeleza mjadala baada ya kusoma hoja ya mwana-"ngwangwa" aliyepita na mwingine akaongeza yake, hoja baada ya hoja.

Ama kupachika maoni haya kwenye safu ya maoni ya "blogu" ya Jeff iliyozindua mjadala... au la Naona itakuwa vizuri tukiwa na focus.

 
At Sunday, 18 December 2005 at 19:13:00 GMT, Blogger boniphace said...

Damija, usiku niliota neno fulani kisha likanipotea nadhani nitkumbuka upya na kulirejesha hapa. Nashukuru harakati hizi ulizozianzisha hapa kibarazani kwako

Naomba tuendelee kuweka maneno mengine na moja twaweza kulipitisha. Kwanza ni dhamira ya kuwa na neno na hapa nashukuru wengi tunayo.

 
At Monday, 19 December 2005 at 23:21:00 GMT, Blogger Jeff Msangi said...

Samahani kwa kutochangia hoja hii mapema kama ilivyotakiwa.Maji huanza na ubaridi,ukianza kuyachemsha yanafikia mahali pa kuwa vuguvugu kabla ya kuwa ya moto.Kisha kama yakiwa ya moto na hutoyatumia yakiwa ya moto basi hurudi tena kwa kutumia njia hiyo hiyo.Utafiti wa neno hili upo katika hali ya vuguvugu,tusiache.Nimeanza kulikubali hili neno ngwanga.Basi wanablogu wengine nao watoe maneno yao kisha tufanye ule utaratibu wa kura.Nadhani tutafika salama kwa mtindo huu.

 
At Tuesday, 20 December 2005 at 09:57:00 GMT, Blogger Mija Shija Sayi said...

Nimewaeleweni wana Ngwanga wenzangu. Lakini mnaonaje kama tukaweka tarehe ya mwisho ya kuwasilisha haya majina tutakayoyapendekeza? na pia ingekuwa vizuri akawepo msimamizi wa shughuli hii. Mnaonaje hili?

 
At Wednesday, 21 December 2005 at 08:07:00 GMT, Blogger mwandani said...

Wazo swafi Mija. Tusisuesue.
hii ndio demokrasia. tufanye
twende mbele, kama anavyosema Msangi, tusiwache mambo yakapoa, kama mpira wa kona ukitaka kufunga kwa huwachi mpira upooze. Tuyakusanye yote haya pahala pamoja, na kuamua... huko nyuma Nkya alishauri neno 'bawazi' na nina imani wengine wanayo maneno mengi vichwani.

haya mpira

 
At Wednesday, 21 December 2005 at 10:09:00 GMT, Blogger FOSEWERD Initiatives said...

nakubaliana na kupata jina mbadala la blogu. lakini hili la ngwanga bado halijaingia akilini! tutape jina ambalo linafanana na shughuli yenyewe ya kublogu. mfano kiliitwa kiyoyozi kwakuwa kunayoyoza hewa! mbadala kwa sababu ni badili, network ikawa mtandao! bora mara kumi tungeiita bwabwaja! tuendelee kukuna kichwa tusiweke nukta hadi tupate jina halisi! nina uhakika wale maprofesa wa kiswahili pale mlimani wanalijua kabisa jina mwafaka la blogu. anayewafahamu basi na atuombee msaada.

 
At Wednesday, 21 December 2005 at 12:05:00 GMT, Blogger Mija Shija Sayi said...

Nimepeta lingine tena "DIMBA". Tuendeleeni tutafika.

 
At Wednesday, 21 December 2005 at 12:55:00 GMT, Blogger mloyi said...

Ninafuatilia mjadala kimyakimya lakini dimba lina maana nyingine, sijui kama lina uhusiano na mambo yanayotokea kwenye kitu kilichokuwa kinaitwa blogu.

 
At Wednesday, 21 December 2005 at 13:52:00 GMT, Blogger Indya Nkya said...

Bongo ziendelee kubungwa. Titatohoa maneno mpaka lini? Moto huu na uendelezwe.

 
At Wednesday, 21 December 2005 at 15:38:00 GMT, Blogger Egidio Ndabagoye said...

Bado nachemsha bongo kwa hili

 
At Thursday, 22 December 2005 at 21:37:00 GMT, Blogger Jeff Msangi said...

Nakubaliana na wote,tuendelee kutoa mapendekezo ya maneno mbalimbali na ifikapo mwaka mpya yaani tarehe 1 tuwe na neno jipya.

 
At Thursday, 22 December 2005 at 23:21:00 GMT, Blogger boniphace said...

Waungwana mwaweza kusoma katika maoni ya Jeff ambako huko nimejaribu kufafanua hoja ya mapendekezo yangu ya blog kuitwa Gazeti Tando.

Naomba kuwasilisha hoja

 
At Friday, 23 December 2005 at 01:43:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

Labda kwa kuanza tunaweza kusema kuwa mjadala huu ufanyike hapa kwa Da Mija na pale kwa Jeff. Na ninavyoona mambo yanavyozidi kunoga (tayari tuna bawazi, ngwanga, gazeti tando, na dimba) itabidi demokrasia ya kura ifanyike. Nadhani zoezi zuri sana hili maana tutaanzisha tume yetu ya uchaguzi huku huku mtandaoni...ila hakuna takrima jamani. Wala kugawa fulana, khanga na mchele.

Tukikubaliana kuwa mjadala huo ufanyike sehemu hizi mbili (au tunaweza kuamua sehemu moja...labda na hili tupigie kura kati ya hizi blogu mbili?)...wenye blogu hizi watakuwa na wajibu wa kuweka mapendekezo kwenye ukurasa wa mbele kwa ajili ya wale wasiosoma maoni. Mnasemaje?

 
At Friday, 23 December 2005 at 16:58:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

Nadhani itabidi kuwa na ukumbi maalum wa kuweka maneno haya yanayopendekezwa. Ninasema hivi kwakuwa blogu za blogspot.com hazitupi nafasi ya kuweka tuliyoandika katika makundi. Kwahiyo ukiandika kitu kikiingia kwenye rekodi ya uliyoandika siku za nyuma inaweza kuwa vigumu mtu kuipata, hivyo ikawa tabu kufuatilia mjadala. Kwa mfano, ukienda kwa Jeff utaona kuwa alichoandika kuhusu neno jipya la blogu kimeshatokomea. Kiko kwenye rekodi za nyuma, na kupata inaweza kuwa sio rahisi. Sijui kama nimejieleza vizuri. Hapa kwa Da Mija, nadhani ukiandika mambo mengine mawili matatu, sehemu hii uliyoandika kuhusu ngwanda itaingia kwenye rekodi ambako kuipata sio rahisi. Tatizo hili la kutokuwa na makundi ni kati ya matatizo yaliyoko kwenye blogspot.com. Ninaongelea jambo hili kwenye mwongozo mpya ninaoandika kwa wanablogu wapya.

kwahiyo lazima tutafute namna ambayo itatusaidia kuweza kupeleka mjadala huu kwa urahisi.

Gazeti Tando..Kasri kapendekeza hili...hili limenigusa kidogo lakini bado halijaniingia kabisa. Nadhani neno gazeti ndio sijalipenda sana. Lakini bado tujadili.

 
At Tuesday, 27 December 2005 at 12:39:00 GMT, Blogger nyembo said...

asalam waungwana!
mtanisamehe kwa kuwa tabia yangu mara zote ni kuona mambo kinyume zaidi ya fikira za wengine, nimeona Da'Mija umekuwa na wazo zuri sana hapo siendi kinyume nawe, lakini vipi ukatoa msamiati huo "ngwangwa" na zisitumike silabi zingine katika kusaidia herufi "ngw" kwa mfano ngwengwe,ngwingwi,ngwongwo,ngwungwu na kadhalika
kisha kwa wanazuoni mnaoendelea na mjadala huu mbona hakuna mapendekezo ya majina mnayoyataka nyie kila mmoja anamshauri mwana blog aweke neno badala ya blog huku yeye akiwa hana mchango wowote zaidi ya maneno mengi,oooh mimi nafuatilia kimya kimya nini maana yake, lini ukimya ukazalisha hoja katika jamii ya wanazuoni kama nyie,lazima tuzungumze na sasa nanena neno langu kwa maana kila mtu anaishi kwa neno alinenalo kwa mujibu wa biblia kwa nini tusitumie neno kama "DURU" KASIRI, LIPULI,VUGA, DONDOO,maneno haya yana maana nzuri katika historia kwa mfano ikulu ya kiongozi wa wahehe katika Tanzania iliitwa LIPULI hili ni baraza la Mzee Mkwawa alipokuwa anapata habari,kufanya maamuzi na kadhalika neno VUGA lina maana kama hiyo kwa Mtemi Kimweri ambae alikuwa mtawala wa maeneo ya Usambaa mwambao wa Pwani ya bahari ya Hindi.
Dondoo ni habari zinazotolewa kwa hali nyembamba walau si katika hali panuzi kama ilivyo kawaida,na Duru hili Sanjari na kuliandika limekuwa neno rahisi masikioni mwetu kwa wale wanaosikiliza idhaa za kiswahili za uingereza na ujerumani hebu litafsirini
kwa hakika liende sanjari na neno DIRA,MURUA,na sasa nasema niko Tayari kwa neno lolote lakini litakalo kuwa halina ama haliko mbali na Tafsiri ya matumizi ya neno Blog......karibuni

 
At Wednesday, 28 December 2005 at 02:15:00 GMT, Blogger mwandani said...

maneno murua Nyembo. kuna kijibanda cha maoni kuhusu huu mjadala kwenye kona ya juu ya ukurasa wa mbele wa 'lipuli' hii.

Ingekuwa bora kunakili uliyosema hapa na kuyaweka huko pia... au kuchukua kiungo hicho na kupachika kwenye 'ngwangwa' yako.

 

Post a Comment

<< Home