31 January 2006

Nani Zaidi......

Bado najiuliza sijui kwa nini MtiMkubwa anaogopa kufungua blogu yake, majuzi amenitumia waraka huu ili wote tujadili kihoja hiki cha wabunge...haya endelea hapo chini.

"Kuna wakati nikikaa nikawaza mambo ya Watanzania nashindwa kupata jibu. Leo nimefikwa na jambo ambalo nimeshindwa kupata jibu. Kwa wale wenye nafasi naomba msomee habari hiyo hapo chini halafu mnisaididie majibu: Maswali niliyojiuliza "..Kati ya mbunge na daktari nani anastahili kulipwa mshahara mkubwa?..Halafu Mheshimiwa Kimiti anaposema "..madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote.." Kama ni kweli?

Wabunge wataka kukata ’keki’ zaidi ya taifa

2006-01-26 08:38:24
Na Mashaka Mgeta

Baadhi ya Wabunge wamechachamaa na kuitaka serikali iwaongezee mishahara, posho na marupurupu ili kuwawezesha kuwatumikia wapiga kura wao kwa ufanisi zaidi.

Lakini kwa upande mwingine wametaka madai hayo hayo yasiandikwe au kutangazwa katika vyombo vya habari, kwa maelezo kuwa zitachochea hisia mbaya na kuwafanya wasikubalike kwa wapiga kura wao.

Wabunge hao walitoa mapendekezo hayo jana walipokuwa wakichangia mada kuhusu masharti ya Mbunge iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo katika semina ya mafunzo inayoendelea jijini Dar es Salaam.

Hata hivyo, Bw. Luhanjo aliwaonya wabunge dhidi ya madai yao hayo na kuwataka wazingatie maslahi yanayokidhi matakwa ya usawa kwa wananchi wote katika kugawana pato la taifa linalotokana na vyanzo mbalimbali zikiwemo shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi.

Alisema hatua ya kudai maslahi bora zaidi kuliko ya watumishi wengine, ni sawa na kuonyesha ubinafsi aliouita kuwa ’collective selfishness’.

Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Bw. Paul Kimiti alisema madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote.

Bw. Kimiti aliwaonya wabunge wasilichukulie mzaha dai hilo wala kulionea aibu kwa kuwa ni miongoni mwa masuala nyeti yanayowahusu.

Mbunge huyo wa siku nyingi, alisema suala la kudai maslahi bora kwa wabunge liliwahi kufanyika pia mwaka 1980 ambapo Spika wa sasa, Bw. Samwel Sitta, Naibu Spika, Bi Anna Makinda na yeye (Kimiti) walikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa kwenye kundi la kudai maslahi hayo.

Hata hivyo alisema madai hayo yalitoweka baada ya wajumbe kadhaa wa kundi hilo ’kutunukiwa’ Uwaziri katika serikali ya awamu ya pili.

Bw. Kimiti alisema madai hayo ni muhimu kwa wabunge kwa vile Wakuu wa Mikoa wanapata kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya shughuli za hamasa zenye mwelekeo wa kisiasa kwa wananchi.

Kwa mujibu wa Bw. Kimiti, hivi sasa wabunge wanapata mshahara wa Sh milioni 1.2 na kiasi kingine cha takribani Sh milioni moja kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha huduma jimboni, fedha ambazo hazihusiani na posho na marupurupu mengine wanayoyapata kwenye vikao vya bunge, vikao vya mabaraza ya madiwani na wanapokuwa safarini.

Naye Naibu Waziri wa Elimu Bw. Ludovic Mwananzila alisema hatua ya wananchi kulalamika wakati wabunge wanapodai ongezeko hilo inatokana na uelewa wao mdogo walionao kuhusu wajibu wa Mbunge.

Bw. Mwananzila alisema uelewa kama huo unachochewa na waandishi wa habari wanapoandika ama kutangaza habari zinazohusu madai ya ongezeko la maslahi ya wabunge, na hivyo kuwafanya (wabunge) wasikubalike kwa wapiga kura.

Alisema kutokana na hali hiyo, habari zinazohusu madai ya wabunge kutaka ongezeko la mishahara, posho na marupurupu hazipaswi kuwafikia waandishi wa habari wala kutangazwa au kuandikwa kwenye vyombo vya habari.

Pia Bw. Mwananzila aliiomba serikali kutoa waraka maalum wenye lengo la kuwashawishi wananchi waamini kuwa posho za wabunge ni kwa ajili ya matumizi kama vile ya kununua mafuta ya magari yao na siyo vinginevyo.

Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai alisema alisema ongezeko hilo ni muhimu kwa vile litakuwa linakidhi mahitaji yao.

Bw. Msindai aliyataja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni kulala kwenye hoteli zinazostahili wanapokuwa kwenye misafara ya Mawaziri wanaposafiri ndani ama nje ya nchi na kuwa na magari yenye hadhi isiyopungua Sh milioni 50.

Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi Bw. William Kusila alisema wabunge ni hazina ya ufumbuzi wa matatizo ya wananchi hivyo wanapaswa kupata ongezeko la mishahara, posho na marupurupu.

Katika kuchangia hoja hiyo, Bw. Kusila aliwahimiza wabunge wapya kuunga mkono madai ya kuongezewa posho, mishahara na marupurupu ili wamudu kuwahudumia wapiga kura wao vinginevyo wasitarajie kuchaguliwa tena.

Bw. Kusila alisema watu wanaopinga hoja za madai ya ongezeko hilo wana kile alichokiita ’wivu wa jumla’ na kwamba hawana mapenzi mema na wabunge.

Naye Mbunge wa Rufiji, Profesa Idrissa Mtulia alisema wabunge na familia zao, wanastahili kutibiwa kwenye hospitali zenye hadhi ili kupata huduma mapema na hivyo kuwa na wakati mzuri wa kurejea kwa wapiga kura wao.

Hata hivyo, mbali na kuwataka wafikirie kuhusu haki ya mgawanyo sawa wa pato la taifa, Bw. Luhanjo aliwahakikishia wabunge hao kuwa, pamoja na mambo mengine serikali itazifanyia kazi hoja zao.

8 Comments:

At Tuesday, 31 January 2006 at 17:33:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Kwanza tujiulize ni kwa nini wao wenyewe hawakutaka suala hili lifike kwa wananchi?

 
At Wednesday, 1 February 2006 at 10:27:00 GMT, Blogger Bwaya said...

Halafu tujiulize, hivi itakuwaje wakijiuzulu? si hawaridhiki?
si kwamba wanataka kurudisha gharama za takrima kweli?

 
At Wednesday, 1 February 2006 at 19:07:00 GMT, Blogger Boniphace Makene said...

Halafu tukumbuke nini nafasi ya wapiga kura baada ya mbunge kuchaguliwa? Je kuna uwezekano wa wanannchi kutumia nguvu ya umma kuwaondoa katika mtindo wa sasa ambapo mbunge akishashinda anaweza kufanya atakalo?

 
At Thursday, 2 February 2006 at 05:36:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

Makene, umegusa moja ya kasoro za mfumo wetu wa mkumbokrasia tulioa nao. Nguvu ya wananchi kuamua wanataka kuongozwa na nani na hawataki kuongozwa na nani zimebanwa na hiki kipengele cha miaka mitano. Hii inaleta kiburi. Kama wananchi waliomchagua mwakilishi wao hawana uwezo wa kumkataa waliyemchagua ni nini maana ya mfumo ambao unadai kuwa kauli ya umma ndio msingi wa utawala wetu.

 
At Thursday, 2 February 2006 at 17:18:00 GMT, Blogger mloyi said...

Uwezo wa kutenda kazi zaidi au Maslahi zaidi? Sioni tofauti yao na madaktari waliowafukuza kumbe kila mmoja anapata kipato cha chini zaidi? Je? wako sawa? Hapana mmoja ni mtumishi wa umma na mwingine ni mtunga sheria, kumbuka bustani ya wanyama, hivyo akisema aongezewe kipato lazima iwe hivyo. nani wa kupinga? Tungoje kikao kijacho cha bunge tuone kama hawatajiongezea hoyo maslahi kwa kiasi wakitakacho lakini madaktari walitaka kulihujumu taifa.

 
At Thursday, 2 February 2006 at 20:05:00 GMT, Blogger John Mwaipopo said...

Damija: Nimeoa mwanamke mwingine. Kumbe yule wa kwanza alikuwa anatamani pesa zangu tu. Alikuwa hanipendi asilani. Huyu wa sasa anaonyesha atakuwa ananipenda na anaitwa mwaipopo.blogspot.com

Badilisha kiunganishi kwenye links

 
At Monday, 6 February 2006 at 11:22:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Naam,

Waswahili husema "ukistaajabu ya Musa utaona ya Firauni" Tumewastaajabia madaktari kuomba ongezeko la mshahara lakini badala ya kuongezewa mshahara wakafukuzwa kazi. Sasa tunayaona ya Firauni. Ndugu waheshimiwa ile kukutana mara ya kwanza tu walichodai ni nyongeza ya mshahara. Kwa sababu wao ndiyo watunga sheria basi itapita bila kupingwa.

Halafu ukisoma nukuu ya Mheshimiwa Kimiti kwamba wabunge ndiyo watu wenye kazi kubwa kuliko zote. Inawezekana ikawa kweli kwamba ubunge ni kazi kubwa kuliko zote lakini sijui kwa vipimo gani. Kadhalika katika maajabu niliyopata kukutana nayo sijawahi hata siku moja kujua ofisi ya mbunge wa wilaya yangu iko wapi. Pia sijawahi kuhudhuria kikao chochote na mbunge wa wilaya yangu mara tu baada ya kumaliza kampeni zake za kutuomba kura. Kama miongoni mwetu kuna aliyewahi kubahatika kuhudhuria mkutano wa hadhara na mbunge wa wilaya yake naomba atuelezee huo mkutano ulikuwaje. Mbunge wangu ninayemkumbuka ni Mzee Kitwana Kondo. Siyo kwamba namkumbuka kwa sababu alikuwa anatutembelea wananchi wake bali namkumbuka jinsi alivyopelekeshwa na mwanamke wa shoka Mama Martha Weja. Mimi nilikuwa naenda kusikiliza ile kesi pale mahakama kuu ikisimamiwa na Jaji Dan Mapigano. Mzee Kitwana Kondo akiwakilishwa na Wakili Murtaza Lakha na Mama Martha Weja akiwakilishwa na Mawakili Profesa Mgongo Fimbo na Profesa Issa Shivji wa Msaada toka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam. Jamani nyie, kama Tanzania ingekuwa na luninga wakati ule hii kesi ingekuwa ni moja ya maonyesho ya juu (classic) katika historia ya kisiasa na mahakama Tanzania. Nakumbuka Wakili Murtaza Lakha alivyokuwa bingwa wa kucheza sarakasi za maneno kuwasumbua mashahidi wa Mama Martha Weja. Halafu jinsi Profesa Mgongo Fimbo Na Profesa Issa Shivji walivyokuwa wanabomoa kwa upole na usanifu mkubwa hoja za upande wa Mzee Kitwana Kondo na kujenga hoja thabiti za upande wa Mama Martha Weja. Ningependa sana kukutana na Mama Martha Weja ili nizungumze naye. Mayo wane, ukiweza hebu tuletee nyeti za Mama Martha Weja.

Turudi tena kwa Waheshimiwa na mshahara wao. Ili kukata mzizi wa fitina ingekuwa vyema sana kama waheshimiwa wangetueleza kipato halisi wanachokipata kwa mwezi ikiwa ni pamoja na marupurupu, posho, pesa za petroli au dizeli kwa ajili ya magari yao, malipo ya pango, na kiinua mgongo wanachokipata baada ya kumaliza muda wao bungeni. Halafu wajieleze kwa nini hicho wanachokipata hakitoshi na wakiongezewa kiasi gani kilichopunguwa katika wanachokipata sasa kitawatosheleza. Wakifanya hivyo watakuwa wametukata kilomolomo sote tunaojitia kujua.

Naliombea kila la kheri bunge letu tukufu.

F MtiMKubwa Tungaraza.

 
At Wednesday, 22 February 2006 at 19:36:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Ameeen

Dennis Londo

 

Post a Comment

<< Home