14 November 2005

Anna Kajumulo Tibaijuka, Mwanamke Mtanzania.
Anna Tibaijuka, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia makazi duniani UN-HABITAT. Tangu kuanzishwa kwa shirika la umoja wa mataifa mwaka 1945, hakuna mwanamke mwafrika aliyewahi kushika wadhifa wa juu kama huu alioushika yeye sasa hivi.

Historia yake fupi inaanzia nchini Tanzania, mkoani Kagera, kijijini Kangaviyo ambako ndiko alikozaliwa. Alizaliwa wakati ambao watoto wa kike walikuwa hawathaminiwi kabisa, kabisa katika jamii, na katika familia yao walizaliwa watoto kumi, kati yao wanawake nane na wanaume wawili. Hivyo familia yao haikuwa na wakati mzuri, ilionekana ni familia iliyopata hasara....wanawake wanane???!!!...duh! lakini anasema kwa bahati nzuri baba yake alikuwa ni mtu mwenye mtazamo mwingine, na hakukubaliana na jamii kwamba watoto wa kike na hasara, alidiriki kuwaambia wanajamii kuwa siku hizi kuna kitu kinachoitwa elimu, na wasichana wangu ni lazima waende shule kama wavulana...ni lazima waendelee. Hivyo Anna alikwenda shule hadi hapo hapo kijijini kwao na baadaye alipata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Alipomaliza chuo kikuu cha Dar er salaam aliolewa na kupata watoto wanne, baadaye mumewe alipata uhamisho wa kikazi nchini Sweden, hivyo wakahamia huko yeye akiwa kama mama wa nyumbani. Lakini anasema mumewe hakuona vizuri kwa Anna kukaa tu nyumbani, hivyo alimshauri ajiunge na masomo ya juu. Anna akajiunga na chuo kikuu cha Uppsala nchini Swedeni ambako alihitimu mwaka 1984 na kupata shahada ya udaktari ya uchumi na kilimo. Baadaye alirudi Tanzania na kufundisha chuo kikuu cha Dar es salaam huku akijiendeleza hadi kuwa Profesa wa uchumi. Zaidi ya kufundisha chuo kikuu ameshafanya kazi na UNCTAD kwa miaka mitano.

Mwaka 2000, Katibu mkuu wa shirika la umoja wa mataifa Koffi Annan, alimteua mwanamama huyu kushika wadhifa huu alionao hadi leo.
Kutokana na wadhifa huu na uwezo wake wa kiutendaji kazi ameweza kushiriki katika midahalo mingi duniani. Pia ameshawahi kushiriki katika kipindi cha HardTalk cha BBC. Na hivi majuzi ameteuliwa na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kuwa mjumbe wa Tume ihusuyo Afrika iliyoundwa na Bwana Blair inayoshirikisha wajumbe 17 watanzania wakiwa ni wawili Rais Mkapa na Tibaijuka. Hotuba ya Rais Mkapa juu ya tume hiyo hii hapa.

Anna Tibaijuka ni mwanamke mwenye akili, kujiamini na mwenye kuweza kufuata malengo yake hata kama mambo mengine yataingilia kati. Mwanamke kama huyu ni ajabu sana hajulikani vilivyo nchini kwake, bali huko ulimwenguni, mwanamke kama huyu alitakiwa kutumiwa vilivyo nchini mwake kwanza kabla ya huko ulimwenguni, bado najiuliza ni kwa nini hajawahi kushika nyadhifa za juu serikalini kama uwaziri na vinginevyo. Nina hakika hata uwezo wa kuingoza nchi anao lakini sijui inakuwaje watu kama hawa wanakuwa hawaonekani. Ninaamini iko siku. Kwa kupata undani wake zaidi kong'oli hapa na hapa

7 Comments:

At Monday, 14 November 2005 at 16:44:00 GMT, Blogger Indya Nkya said...

Huyu mama acha kabisa. Ni mchapa kazi kwelikwli. Nimeshawahi kufanya naye kazi mwaka 1997 alivyokuwa kiongozi wa utafiti kuhusu kuandaa mpango wa kahawa kwa millenium ya tatu nchini Tanzania. Nilimvulia kofia. mama anachapa kazi na anajua anachofanya.

 
At Thursday, 17 November 2005 at 11:25:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Bibie,

Naona halahala zako za wanawake wa shoka zinarejea mkondoni.

Huyu uliyetuletea leo ni mwanamke wa shoka hasa. Nimemuona kwenye midaharo mitatu ya BBC; Hardtalk. Talking Point, na ule wa Global Debate sikuwa na budi kukubali kwamba ni mwanamke wa shoka. Mzao wa mwanamke/binadamu wa namna yake ni adimu sana.

Tafadhali nakuomba uendelee kutuongezea dozi mpaka tudate.

Nakutakia kila la kheri na mafanikio.

Watakabahu, ni miye kijana mwenziyo,

F MtiMkubwa Tungaraza.

 
At Thursday, 17 November 2005 at 21:43:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Mija si kwamba sio maarufu, kwa wale wafurukutwa wa maendeleo nyumbani jina la mama Tibaijuka sio geni, kwani BAWATA ilipokuja juu ilinyanyua sana jina la huyu mama. Tatizo la nyumbani ni wachache sana wanaoweza kufuatilia vitu vya msingi kama hivyo.
Bongo ukitaka ujulikane inabidi uwe kiongozi wa Simba,Yanga,FAT na upuuzi mwingine.Kama kwenye siasa ukitaka kufahamika basi uwe kiongozi wa CUF,CHADEMA au CCM hapo utawaka na kumeremeta katika kila kona ya mitaa ya walalahoi, katika vijiwe vya wakereketwa na wafurukutwa. Lakini yote haya yana mwisho, na tusubirie huo mwisho kama utakuwa wa heri.
Dennis Londo

 
At Sunday, 27 November 2005 at 15:54:00 GMT, Blogger Ndesanjo Macha said...

Mama Anna kweli ni mwelewa wa fani yake na mchapa kazi. Nilimuona mwaka huu akihutubia mkutano mmoja wa masuala ya utandawazi. Alinimaliza sana alipokuwa akitoa uchambuzi kuwa ufugaji wa ng'ombe kwa staili kama ya wamasai hauna nafasi tena katika ulimwengu wa leo. Akatoa nadharia za kiuchumi na kusema kuwa anasema anayosema kwakuwa yeye ni mwanauchumi. Niliandika habari kuhusu uchambuzi wake huo, kuna vyama vinavyotetea haki za wafugaji vimekuja juu kutokana na kauli yake hiyo.
Kwa ufupi, endelea kutuchambulia wanawake kama hawa na tutazame ni yapi mazuri ambayo tunaweza kuiga toka kwao au kuendeleza.

 
At Wednesday, 7 December 2005 at 13:50:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Kofi Annan alimtuma Mama Tibaijuka akakague bomoabomoa ya Harare. Sasa amtume tena aende akague bomoabomoa ya Dar. Akimaliza hapo aende Gaza na West Bank akakague bomoabomoa ya wana wa Israeli.

Bomoabomoa Jijini: Watu waweweseka baada ya kupewa noti

2005-12-07 15:14:05
Na Moshi Lusonzo, Temeke


Bomomoa ya majumba imeanza tena Jijini, na safari hii imewakumba wakazi wa mitaa ya Sandali huko Temeke, ambapo jumla ya nyumba 57 zimesambaratishwa.

Tofauti na bomoa bomoa za nyuma, hii ya Sandali imewafanya watu waweweseke baada ya kupewa vitita vya mamilioni ya Shilingi kama fidia ya mali zao.

Kwa mujibu wa Mratibu wa Mradi wa Uboreshaji wa Makazi yasiyopimwa kwa kushirikisha Jamii, CIUP, Bw. Bakari Saidi tayari wakazi hao wameshaweka vibindoni mwao Sh.milioni 91,pesa ambazo walikabidhiwa na Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bw.Baraka Konisaga mwishoni mwa wiki.

Amesema mitaa iliyohusishwa na mradi huo ni pamoja na Sandali yenyewe, Mopogo na mtaa wa Mwemberadu, ambapo nyumba hizo zilibomolewa ili kupisha ujenzi wa barabara, mifereji ya maji machafu,vizimba vya taka na njia za wapita kwa miguu.

’Kweli wananchi wamefurahishwa na zoezi letu,kila mtu aliyebomolewa nyumba au ukuta wa nyumba amepewa pesa kama fidia ya kuharibiwa mali yake,’ akasema Bw. Bakari.

Hata hivyo, katika zoezi hilo kiwango cha juu cha fidia kilikuwa Sh. milioni nane wakati wengine waliambulia hadi milioni moja.

Kutokana na utaratibu huo, eneo hilo litakuwa na miundo mbinu ya uhakika na kizuri zaidi mitaa hiyo yote itawekewa taa maalum ambazo zitatumika kuweka usalama nyakati za usiku.

Baada ya kukamilika mradi huo, zoezi hilo litahamia mitaa ya Chang’ombe ambako pia nyumba kadhaa zitabomolewa ili kuboresha mazingira ya eneo hilo.

Pamoja na hayo, wakati akikabidhi hundi kwa wakazi wa Sandali Mkuu wa Wilaya ya Temeke Bw. Konisaga aliwataka wananchi hao kuupokea kwa mikono miwili mradi huo japokuwa katika uboreshaji wa miundombinu hiyo ni lazima baadhi ya mali ziathirike.

Akasema Serikali kwa kutambua hilo imeamua kuwafidia wananchi kulingana na thamani ya mali zao.

Pamoja na hayo, amewataka wakazi hao waliopokea hundi za pesa, kuzitumia kwa kupata makazi mbadala na sio vinginevyo.

 
At Tuesday, 13 December 2005 at 10:57:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

People living in Mchikichini quarters in Dar es Salaam ponder their next move yesterday after the Ilala Municipal Council ordered them to vacate the houses to pave the way for the construction of a modern housing estate in the area.

Sijui Kofi Annan atamtuma Mama Tibaijuka kwenda kushubikia hiki kitimtim!

F MtiMkubwa Tungaraza.

 
At Saturday, 31 December 2005 at 16:04:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Kwanza nitoe pongezi kwa Blogger kwa maelezo mazuri yanayomhusu profesa Dr. Anna Tibaijuka. Nilimfahamu profesa Tibaijuka akiwa Ultuna Uppsala kama mwanamke shupavu, mbunifu na mwenye kupenda maendeleo ya nchi yake. Niliposikia tetesi kuwa huenda raisi wetu mpya akamteua mwanamke wa kwanza kuwa waziri mkuu, nilimfikiria sana profesa Tibaijuka. Ombi langu kwa Blogger ni kuwa, "Kwa sababu sio wengi wanaoweza kuyafikia maandishi mazuri uliyoyaandika kuhusu profesa Tibaijuka ninaomba maelezo hayo pia yachapishwe kwenye magazeti ya nyumbani ili wananchi na viongozi wetu ambao hawamfahamu nao waweze kumjua". Nina imani kabisa kuwa viongozi wapya waliochaguliwa watayachukua mawazo uliyoyatoa kuhusu profesa Tibaijuka. Hatimaye kumtumia katika kuiendelea TANZANIA kwa ajili ta watanzania na ulimwengu mzima.

 

Post a Comment

<< Home