21 October 2005

Hakutaka mchezo Nyerere!

Kipindi kama hiki miaka sita iliyopita Tanzania ilikuwa bado katika maombolezo ya kuondokewa na hayati baba wa taifa Mwalimu Nyerere. Ni katika kipindi hiki habari nyingi za mwalimu zilianza kutoka wazi wazi, za ndani na nje ya familia.

Habari ambayo ilinivutia kuliko zote ni hii ya mtoto wake wa kiume. Kwanza kabisa habari hii nilihakikishiwa ni ya kweli kabisa......., kwamba mmoja kati ya watoto wake wa kiume alikuwa akisoma katika sekondari moja huko mjini Mbeya, (inasemekana mwalimu aliwasomesha watoto wake katika shule hizi hizi za kawaida tulizokwenda mimi na wewe). Sasa huko shuleni huyo mtoto akawa anataka kuleta zile za mimi mtoto wa Nyerere, utundu na kutokusikia(si unajua tena utoto!. Basi siku moja yeye na wenzie wawili waliamua kutoroka usiku kwenda kujivinjari mjini, wakiwa huko wakakamatwa na mwalimu wao duh! hawana la kusema wala la kujitetea. Alichofanya mwalimu yule ni kumtaarifu mkuu wa shule, naye mkuu wa shule usiku ule ule akapiga kengele wanafunzi wote washuke kuja kufanya "lokoo", basi lokoo ilipopita wenyewe kweli hawakuwepo wengine wakatawanyika kwenda kulala huku wakisubiri kusikia kesho yake itakuwaje? maana na mtoto wa Nyerere alikuwemo, atarudishwa kama wengine ambavyo huwatokea au??

Basi ile kesho yake kila mtu anamtazama mkuu wa shule ataamuaje, mkuu wa shule hata hakuwa na mengi, alichosema ni kwamba wanafunzi hawa watatu wamekosa nidhamu na heshima, wametoroka usiku kinyume na sheria ya shule hivyo wataadhibiwa kwa kurudishwa majumbani kwao na kurudi hapa shuleni baada ya miezi mitatu kila mmoja na mzazi wake.

Wanafunzi ikabidi warudi makwao....kilichotokea huko kwa Nyerere na mwanae haijulikani, ila siku ya kuripoti ilipofika, mzee kifimbo akawasili bila kuchelewa yeye na mwanae. Akakaribishwa na mkuu wa shule ofisini na mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Mkuu: Ndugu mzazi, kama ulivyosoma barua tuliyokuletea, mwanao ilibidi tumpe adhabu
hii kutokana na utovu wake wa nidhamu, hii ilikuwa ni adhabu ya kwanza, ya
pili ni kupata viboko mbele ya wanafunzi wote ili iwe ni fundisho kwa wengine.

Mwalimu nyerere: (Kwanza alimtizama juu hadi chini yule mwalimu mkuu, kisha
akasimama na kumpa mkono)...Kwa kweli mwalimu wewe ndio hasa watu
ninaowataka mimi....(akiendelea) Unajua huyu aliporudi nyumbani
nilishtuka, nilishangaa na kujiuliza... ni mwalimu gani huyu
mwenye kuweza kuniita mimi shuleni kwa ajili ya mtoto....nikasema
mwalimu huyu ndiye hasa anayejua kazi yake. Wewe kama mwalimu wa
mwanangu mimi kwako ni mzazi na sio Rais, una uwezo wa kuniita
wakati wowote. Na titahakikisha nawawajibisha waalimu wasiojua
kazi kazi zao na kuogopa na kuwanyenyekea watoto wa viongozi wa
nchi.

Baada ya pale kengele iligongwa, wanafunzi wote wakatoka kushuhudia fimbo. Kwa kawaida ilikuwa ni mwalimu mmoja ndiye humchapa mwanafuzi lakini siku hiyo mwalimu mwenyewe aliikamata fimbo. Baada ya hapo ulipita mwezi mmoja yule mwalimu mkuu akapandishwa cheo na kuamia Wizara ya elimu huku Mwalimu Nyerere akisema nataka wawajibikaji kama hawa sio waoga waoga.

Wasomaji hiki kipindi nadhani ndio kilikuwa cha uwazi na ukweli. Kufanya kile ambacho unajua ni haki bila ya kuwa na wasiwasi wa kufukuzwa kazi. Sijui ni kwanini Haki elimu imeundwa baada ya Nyerere.

1 Comments:

At Saturday, 22 October 2005 at 12:13:00 BST, Blogger Indya Nkya said...

Ndiye mwalimu huyu. Nakuambia siku hizi hizo shule ni za walala hoi. Wengine wanakwenda shule za Mtakatifu fulani na academy. Kwa hiyo hakuna hata kiongozi anayejua hizo shule zikoje.

 

Post a Comment

<< Home