08 May 2006

Da' Mija na wanawake wa shoka yafunga mwaka!!

Shukrani hoi hoi na vifijo vimuendeee ndugu Ndesanjo Macha popote pale alipo kwani kama si yeye leo hii nisingekuwa naandika haya ninayo yaandika. Ndesanjo ndiye aliyenikurupua huko nilikokuwa na kusisitiza kwamba ni lazima nifungue blogu, nilikwepa kwepa lakini wapi jamaa alikuwa na mimi tu mwishowe nikaona ngoja nikate shauri na leo hii nayaona matunda yake. Sio siri ufahamu wangu sasa umeongezeka-ongezeka.

Labda niwapeni kisa kizima cha Ndesanjo kunibabatiza. Nilikuwa katika harakati zangu mtandaoni mara nikakutana na blogu ya Jikomboe, kuangalia vizuri naona Ndesanjo Macha..nikajiuliza huyu mtu huwa namsikia sikia ngoja nione anafanya nini na humu mtandaoni, basi nikaanza kumfuatilia na kwa kweli makala zake zilinitia nguvu sana nikajisemea peke yangu..'haiwezekani huyu mtu lazima nimjue zaidi'.. basi siku moja nikaona nimtupie kaji-swali ambako kanaonyesha niko kinyume na yeye yaani kama mpinzani wake nione atajibu nini!.. mara nyingi mimi nikiona mtu anafanya vitu vizuri hupenda kujua na anapokoselewa hupokeaje hali hiyo? Wee! nilipata jibu hilo mwenyewe nilitulia bahati mbaya nimesahau hata jibu lenyewe labda kama Ndesanjo unalikumbuka. Basi kuanzia hapo Ndesanjo akajua huyu mtu yuko kinyume na mimi kwa hiyo akawa amekaa mkao tayari tayari, mimi sina hili wala lile siku moja nikatoa maoni katika habari fulani ya "Nimtume nani" nikamwambia labda umetumwa wewe kwani Mungu haangalii mtu fulani ili kumtuma". Sasa hapa nikamchanganya kidogo kwamba huyu Da'Mija yuko upande upi? yuko upande wangu au ananidhihaki?... akanipiga swali Kwani wewe kwako Mungu ni nini au ni kitu gani?? Duh! nikaona haya tena mengine...kaka yangu hapa hakunielewa lakini na mimi sikufanya ajizi nikamuelewesha Mungu ni nini, ni nani kwa jinsi nilivyokuwa nikimuelewa. Baada ya maelezo hayo ndiyo akasema wewe binti ni lazima ufungue blogu yako. Basi nikaona huyu Ndesanjo lazima atakuwa ametumwa na kwangu mimi pia. Hivyo nikafungua blogu yangu. Hadi sasa hivi ingawa sina data kamili, lakini ninaamini huyu bwana ndiyo ameweza kushawishi watu wengi zaidi kufungua blogu zao. Ubarikiwe Ndesanjo, tubarikiwe wanablogu wote.

13 Comments:

At Monday, 8 May 2006 at 09:58:00 BST, Anonymous Anonymous said...

hongera !

 
At Monday, 8 May 2006 at 12:55:00 BST, Blogger MICHUZI BLOG said...

da mija!

si wewe peke yako uliyeambukizwa ugonjwa hatari na usiotibika wa kublogu. mie pia yalinikuta septemba mwaka jana nilipokuwa helsinki ambako niligongana na kuhani mkuu wa blogu za kiswahili ndesanjo macha ambaye hakuchelewa kunimwagia virusi vya maradhi haya. uzuri maradhi haya hayaui kama ukimwi bali yanakuunganisha na watu dunia nzima, nami namshukuru kwa hilo. na kwa kweli nakuwa kama nna deni endapo kama sijapoti japo picha moja kwa siku. nakushukuru ndesanjo kwa hilo.

da mija na wengineo, natembelea brazil kuanzia tarehe 13 mei hadi 20. kama kuna bloga naomba tuwasiliane

 
At Monday, 8 May 2006 at 14:30:00 BST, Blogger mwandani said...

Hongera kutimiza mwaka. Kadhalika kaugonjwa niliambukizwa na huyo huyo Macha, nilidhani katuma barua pepe tuseme habari za zamani - kumbe kiungo cha jikomboe, nilipoingia kwenye blogu hiyo basi ndiyo nikawa nishapata maradhi.

Tena hongera.

 
At Monday, 8 May 2006 at 16:12:00 BST, Blogger boniphace said...

Hepi Birthday. Gazeti Tando lako linabaki na historia yake na heshima mzito sana katika ukurasa wa wanaharakati wa uandishi wa maudhui fulani na kuyasimamia. TUNA IMANI NA WEWE NA TUNATARAJIA MENGI ZAIDI YAKO. Mungu akupe pumzi na abariki kazi hizi za mikono yako ambazo zatufaidisha wengi. Umepewa bure na we toa bure! Huku ndiko kucheza karata yako

 
At Monday, 8 May 2006 at 17:24:00 BST, Blogger Jeff Msangi said...

Hongera sana Damija,blog ni ukombozi wa aina yake.Hongera tena na tena.

 
At Monday, 8 May 2006 at 22:15:00 BST, Blogger John Mwaipopo said...

Hongeeeeeera. Kublogu mwaka mzima sio mchezo. Halafu bethidei zako zinakaribiana. Huyu ndesanjo anastahiki kupelekwa kwa pilato kwa kutapakaza kaugonjwa haka ka kublogu. Nami aliniambukiza yeye.

 
At Tuesday, 9 May 2006 at 11:59:00 BST, Blogger Vempin Media Tanzania said...

Ugonjwa huu nadhani hautibiki na tiba yake atakuwa anaijua nani sijui, bwana kublogu si mchezo, any way happy birthday Mija mwaka mzima si mchezo nadhani tuapiga hatua kwa kasi sana.

 
At Tuesday, 9 May 2006 at 12:37:00 BST, Blogger Egidio Ndabagoye said...

Hongera DaMija!
Blogu sasa hivi hapa Bongo imekuwa gumzo.Habari za uhakika zinahakikishwa kwenye blogu.

Mwaka si mchezo dada huyu jamaa sijui alitumia aina gani ya kirusi kutusambazia haka kaugonjwa.

Haya ndio mapinduzi ya teknolojia

 
At Wednesday, 10 May 2006 at 14:45:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Da Mija,
Umenikumbusha mambo nilikuwa nimesahau. Jamani, mwaka siku hizi unapita kama wiki. Siamini umetimiza mwaka. Nakupongeza sana maana wewe ni kati ya watu ambao wameleta mwamko mkubwa kwenye blogu kutokana na mchango wako kwenye blogu za wengine na makala zako (ambazo huwa nazitumia kuandikia makala za wikipedia) kuhusu wanawake na mambo mengine ya bara letu. NIlipokuwa najaribu kukuvuta nilijua kuwa kuingia kwako kwenye blogu kama mwanamke na pia msanii kutaleta mchango wa aina yake. Na umethibitisha hivyo katika maandiko yako. Na pia tumeweza kuona picha yako na jinsi mungu alivyokujalia!!!!!!!!
Endelea hivyo hivyo...kazi kubwa tunayokupa ni kutuletea Mti Mkubwa...

 
At Wednesday, 10 May 2006 at 16:27:00 BST, Blogger MICHUZI BLOG said...

mti mkubwa? ndesanjo tufafanulie, ama ni signo yenu? anyway, ijumaa napaa kwenda brazil, mji wa brasilia, sijui kuna mabloga huko?

 
At Friday, 12 May 2006 at 05:21:00 BST, Blogger Mija Shija Sayi said...

Ninawashukuru woote kwa kunipa baraka zenu ambazo hasa ndio nguvu yangu ya kuuanza mwaka mwingine wa kublogu.

Ndesanjo, nimewasiliana na Mti kuhusu hili suala la kublogu akaniambia .."vijana tulieni kwani mna haraka ya nini muda utakapowadia mtaniona uwanjani!"...

Michuzi, tunakutakia safari njema na tunaomba utuletee zawadi ya angalau wanablogu wawili wapya maana sina hakika kama huko tunao mabloga.

 
At Thursday, 18 May 2006 at 07:15:00 BST, Blogger Reggy's said...

Nakupongeza kwa dhati Da'mija kwa kjutimiza mwaka. Hata mimi umenikumbusha kuhusu Ndesanjo, kumbe ndiye aliyetumwa na Mungu, amewavua nikiwemo mimi. kwa ufupi tu mimi nilisoma article yake kwenye Gazeti la Mwananchi, nikaona address yake, nikaichukua na kuanza kuitazama ktk internet. kisha nikaona kijisehemu kinachoelekeza namna ya kuanzisha blogu yangu, nikaanza na kumwandikia ndesanjo kwa msaada zaidi, aliitikia ombi na kunitumia maelekezo mengi mazuri hadi nimefika leo hii. Mungu ambariki na awabariki wote.

 
At Monday, 29 May 2006 at 14:51:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Da Mija: basi mwambie Mti Mkubwa kuwa vijana tumetulia. Hatuna papara. Tunamsubiri kiwanjani. Uelewa wake wa historia na uwezo wake mkubwa wa kukumbuka mambo, majina, tarehe, matukio, n.k. tunauhitaji sana (sio tu kwenye maoni bali pia kwenye ukurasa wake mwenyewe).

 

Post a Comment

<< Home