04 May 2006

Boyz 11 men sasa kiboko!!


Haya tena, ahadi ndio zinazidi kumiminwa na uongozi wa awamu ya nne. Hivi majuzi wakati wa sherehe za mei mosi ambapo kitaifa zilifanyikia Shinyanga Ndugu rais ameahidi kushughulikia suala zima la mishahara, sasa sijui ni ya kweli au la! na ni kwa kiwango gani itaongezwa bado sina hakika.. MtiMkubwa kaniletea hii habari hapa ili wote tushuhudie hizi ahadi. Soma habari yenyewe hapo chini...



2006-05-02 16:53:55
Na Mwandishi Wetu, Jijini

Rais Jakaya Kikwete na Waziri wake Mkuu, Bwana Edward Lowassa, marafiki ambao watoto wa mjini waliwahi kuwaita Boyz ll men, wamewadhihirishia Watanzania kwamba hawana mchezo na wamepania kuboresha hali za Watanzania.

Rais Kikwete alidhihirisha hilo jana wakati anahutubia mamia ya wananchi katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani, Mei Mosi, Rais Kikwete, sherehe zilizofanyika kitaifa mkoani Shinyanga katika uwanja wa Kambarage.

Katika hali ambayo inaonyesha Rais amepania kutofanya mambo ya danganya toto katika uongezaji wa mishahara na kuboresha maslahi ya watumishi, alitangaza mikakati kadhaa.

Mosi: Alisema ataunda tume itakayotoa hali halisi ya maslahi ya watumishi iliyopo Serikalini na kwenye mashirika ya umma.

Rais alisema tume hiyo pamoja na mambo mengine, itashughulikia uchambuzi wa mishahara na maslahi ya watumishi hao.

Kwa mtaji huo, ’watemi’ Serikalini na katika mashirika ya umma ambao siku zote wanapigania kuongezwa kwa maslahi yao wenyewe, sasa wataumbuka.
Pia madaraja makubwa ya watumishi walionacho na akina pangu pakavu tia mchuzi, yataondoka.

Na kwa upande mwingine, watumishi wasio na nafasi ambao hali zao zimedhoofu kutokana na maslahi duni, watatamba katika uwanja wa haki na usawa.

Rais Kikwete alisema tume hiyo ataitangaza rasmi wiki ijayo na anataka kabla ya mwaka huu kuisha iwe imemaliza kazi hiyo.

Alisema mara baada ya Tume kumaliza kazi na kumpa mapendekezo, hataweka usiku na badala yake atayashughulikia mara moja na kutoa uamuzi juu ya hatua za kuchukua.

Pili: Rais ametaka Mabaraza ya Kisekta ya mishahara ya Kima cha Chini cha mishahara yaundwe mengi ili kushughulikia maslahi ya kundi hilo.

Kwa mtaji huo, kilio cha muda mrefu cha walalahoi huenda kikapungua.
Kwa muda mrefu, wafanyakazi wa kima cha chini wamekuwa wakilalamika kwamba ’wako jangwani’ kutokana na maslahi duni.

Tatu: Rais alisema suala la ajira amelishikia bango na kwamba mikakati inakamilishwa na muda si mrefu Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana italifahamisha Taifa.

Alisema dhamira ya Serikali ni kuongeza ajira kwa Watanzania na kwamba imedhamiria kuweka mazingira mazuri ambayo yatawezesha kukuza ajira nchini ili Watanzania wanufaike na kupunguza dhiki ya maisha.

Nne: Rais pia alizungumzia suala la kuajiriwa kwa wageni katika nafasi ambazo zingeweza kufanywa na Watanzania.

Alisema Serikali itakuwa makini na yenye ukali kwa ajira za aina hiyo.
Kwa kauli hiyo, malalamiko yaliyozagaa kwamba kuna Ma TX feki wanafanya kazi ambazo hata Wabongo ambao hawakwenda shule wanaweza kuzifanya, yatapungua.

Wananchi mbalimbali walioongea na gazeti hili kuhusu hotuba ya Rais walisema serikali ya awamu hii ni kiboko na kama yote yaliyoahidiwa yatatekelezwa, hali za Watanzania zitainuka.

4 Comments:

At Thursday, 4 May 2006 at 07:33:00 BST, Blogger John Mwaipopo said...

Mija nimekusikia kwa sauti kuu na umakini mkubwa. Isijekuwa ni mbwembwe za siasa na kudhania bado wako kwenye kampeni. Sie yetu macho na bila shaka matumbo. Tumekaza mikanda hata tukaanza kutoboa matundu zaidi mkandani huku wengine wakinunua mikanda mirefu, maana ile waliyokuwa nayo wakati sie akina holoipoloi tunaanza kuikaza haiwatoshi tena. Wasisau matendo hukidhi haja maridhawa kuliko maneno ama debe tupu halivumi ama mkono mtupu haulambwi. Lakini kwa spidi ya kujenga shule (bila walimu) 381 kwa siku 120 si haba watafanikiwa si punde. Wastani wa shule tatu kwa siku moja.

Hapo kwenye madini sichangii kitu maana naogopa mkong'oto.

 
At Friday, 5 May 2006 at 11:07:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Mayo,

Nimekutia ujumbe mwingine wa miujiza ya serikali ya awamu ya nne. Tafadhali ongezea ili wanagazeti tando wapate uhondo zaidi.

 
At Friday, 5 May 2006 at 11:08:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Nilisahau kujitambulisha ni mimi MtiMkubwa.

 
At Saturday, 6 May 2006 at 22:47:00 BST, Blogger Jeff Msangi said...

Bado naendelea kuganda kwenye kusisitiza kwamba hotuba ziendane na vitendo..Yapo mengi mazuri katika hotuba zote zilizowahi na zinazotolewa hivi sasa.Swali ni je,yanatekelezeka?

 

Post a Comment

<< Home