27 May 2006

Graca Simbine Machel.


Kuna nchi nyingi sana za Afrika ambazo unaweza kuzungumzia historia zake bila kutaja wake wa viongozi waasisi wa mataifa hayo na bado historia ikakamilika. Kwa nchi ya Msumbiji kitu hicho hakipo!. Hauwezi kuelezea historia ya Msumbiji bila kumuhusisha bibi Graca Machel ambaye ni mjane wa Rais wa kwanza wa Msumbiji Ndugu Samora Machel(Mzee wa kombati)

Graca Simbine ni mwanamke mwenye hulka ya upole lakini ni mwenye akili nyingi na makini sana katika utekelezaji wa mambo yake. Ni mtu asiyekurupuka wala kuyumbishwa na mikumbo ya kijamii. Kwa ufupi ni mtu anayefanya jambo kutokana na imani yake inavyomuongoza.

Mwanamke huyu wa shoka alizaliwa tarehe 17-10-1946 katika eneo la pwani ya ukanda wa Gaza nchini Msumbiji. Akiwa ni mtoto wa mwisho kati ya watoto sita wa mzee Simbine na bibi Nelly ni yeye peke yake ambaye hakubahatika kumuona baba yake kwani alizaliwa majuma matatu baada ya baba yake kufariki. Mzee Simbine ambaye alikuwa akifanya kazi katika misheni ya Methodist hapo kijijini, aliacha maagizo kabla ya kufa kwake kwamba mkewe na watoto wake wakubwa ni lazima wahakikishe mdogo wao (Graca) anakwenda shule hadi masomo ya juu. Alipofikisha miaka 6, dada yake mkubwa aliyekuwa mwalimu alimchukua na kumuingiza shule, anasema dada yake alikuwa ni kama mama yake wa pili kwa jinsi alivyomlea vizuri na kuhakikisha anafanya vizuri katika masomo yake, na kutokana na usimamizi mzuri wa dada yake aliweza kufaulu masomo yake ya msingi na kupewa nafasi na misheni ya Methodist kwenda kusoma sekondari. Anasema akiwa sekondari ndipo alipoanza kubaini ubaguzi uliopo kati ya weusi na weupe kwani darasani kwao alikuwa mweusi peke yake kwa hiyo aliona jinsi alivyokuwa akibaguliwa na kutengwa na weupe. Lakini kama nilivyosema hapo awali kwamba yeye si mtu wa kuyumbishwa hilo la kubaguliwa halikumfanya kushindwa kuzingatia masomo yake na mara nyingi anasema jambo moja lilikuwa likimfariji kwamba hata kama alikuwa akibaguliwa lakini alijua Msumbiji ni ya kwake na si yao na wao wako kwake, hivyo alifanya masomo yake vizuri na kufanikiwa kupata tena ufadhili wa kwenda chuo kikuu cha Lisbon Ureno kusomea Lugha hiyo ilikuwa mwaka 1968.

Akiwa Lisbon alikutana na watu wengi wenye fikra mbalimbali za kimapinduzi, akasikia pia habari za FRELIMO chama ambacho kilikuwa kinapigania ukombozi wa Msumbiji. Graca akajiunga kwa siri katika chama cha FRELIMO, lakini haikupita muda mrefu serikali ya kikoloni ikagundua anachokifanya Graca na hivyo ikaandaa adhabu ya kwenda gerezani pindi Graca atakaporejea Msumbiji. Graca kwa kulijua hilo ikabidi asimalize masomo yake na kukimbilia nchini Uswisi. Mwaka 1973 akiwa bado ulaya akaamua kujiweka wazi kama mwanasiasa na mpigania uhuru wa nchi yake na mwaka uliofuata 1974 chama cha FRELIMO kilimrudisha Afrika lakini nchini Tanzania ambapo ilimpatia kazi ya kuwa mkuu wa shule ya sekondari ya FRELIMO iliyokuwa Bagamoyo, shule hii siku hizi hujulikana kama shule ya sekondari ya Kaole. Chama cha FRELIMO kilikuwa na shule nyingi za sekondari katika nchi huru za Afrika nia ikiwa ni kuwapatia elimu wananchi wake huku harakati za ukombozi zikiendelea. Akiwa Tanzania alijifunza pia mafunzo ya kijeshi ya kujilinda na ni katika kipindi hiki ndipo alipoweza kukutana na mzee wa kombati Samora Machel. Graca na Samora walianza kama marafiki wa kawaida lakini baadaye urafiki ukazidi na kuwa wapenzi wakati huo ikiwa ni miaka mitatu tu imepita tangu Samora afiwe na mkewe wa kwanza Josina Machel.

Harakati za FRELIMO ziliendelea vizuri kwani mwaka uliofuatia tarehe 25-06-1975 Msumbiji ilijipatia uhuru wake kutoka wa Wareno, mwaka huo huo Graca alifunga ndoa na Samora machel.

Kutokana na elimu yake na uzoefu wake wa kufundisha, na jinsi alivyoweza kuishika vizuri nafasi ya ukuu wa shule ya FRELIMO Bagamoyo, serikali mpya ya Msumbiji iliona haina sababu kumnyima Graca nafasi ya uwaziri wa elimu na utamaduni. Akiwa wanamke pekee na wa kwanza kushika nafasi hiyo kubwa anasema kwanza alipigwa na butwaa na kutetemeka hakujua kama ataweza kuimudu au la!...alijifungia siku kadhaa chumbani kwake akili na kujiuliza kama akikataa si ataonekana mdhaifu? na je akikubali halafu asiimudu si watasema '..unaona matatizo ya kuwapa nafasi wanawake..!!' Lakini baada ya kujufikiria kwa muda alifuta machozi na kuchukua kazi!! Lengo lake likiwa moja, kuhakikisha watoto wote wa Msumbiji wanakwenda shule. Kwa mafanikio makubwa alibadilisha kabisa hali ya elimu ya Msumbiji kiwango cha watoto kwenda shule kiliongezeka mara dufu kutoka watoto 400,000 aliowakuta alipoishika wizara hadi 1,500,000 ikiwa ni asilimia 72 zaidi.

Haya popote penye maendeleo adui hakosi kujitokeza, mwaka 1976 kikundi kidogo cha wananchi wa Msumbiji wakaunda chama cha kuipinga Frelimo kilichojulikana kama RENAMO. Chama hiki kilikuwa kikifadhiliwa na wazungu kutoka Rhodesia(Zimbambwe), Afrika ya kusini na Marekani. Wazungu hawa waliunda na kufadhili RENAMO ili kuiadhibu Msumbiji kwa kuisaidia makazi wafuasi wa ANC. Kazi ya kikundi hiki cha RENAMO ilikuwa ni kufanya uharibifu katika sehemu zote za maendeleo ambapo FRELIMO ilikuwa ikifanya mfano, ilibomoa mashule na hospitali zilizojengwa na FRELIMO, iliharibu reli na mengine mengi, jambo hili lilimtingisha sana Graca ukizingatia wizara yake nayo ilikuwa ni kati ya tageti za RENAMO. Mwaka 1984 Samora Machel alikubali kusaini mkataba na wafadhili RENAMO wa makubaliano ya kuacha kuifadhili RENAMO na FRELIMO kuacha kuipa msaada wa makazi wafuasi wa ANC. Inasemeka kwamba kwa Samora kusaini mkataba ule ni kama alikuwa akisaini mkataba wa kifo chake, kwani miaka miwili baadaye tarehe 19-10-1986 alifariki katika ajali ya ndege inayosemekana ilipangwa na hao hao wazungu wa Afrika ya kusini. Samora alikuwa akirudi nyumbani kutoka katika mkutano Lusaka Zambia.

Kifo hiki kwa Graca kilikuwa ni pigo kubwa sana. Hakuamini ilikuwa ni ajali ya kawaida alijua na alisema waliomuua mume wangu ndiyo walewale waliomfunga Nelson Mandela. Maneno haya alimuandikia Winnie Mandela wakati wa msiba kwamba "wanadhani kwa kukata miti mirefu zaidi katika msitu watakuwa wameteketeza msitu wote!! ni wale wale waliomuua mume wangu ndiyo waliomfunga mume wako.."

Kwa miaka mitano mfululizo tangu Samora Macheli afariki, Graca alivaa nguo nyeusi peke yake. Na ilipofika mwaka 1989 alistaafu wadhifa wake wa uwaziri na kujishughulisha na shughuli za maendeleo ya jamii hasa hasa watoto. Mungu si Athumani Mola akaona si vyema Graca kuendelea kuishi peke yake hivyo akamtafutia mwenzi mwingine ambaye pia ni shujaa wa Afrika Bwana Nelson Mandela. Mwaka 1998 Graca alifunga pingu za maisha kwa mara ya pili na Mandela ambaye alitengana na mkewe Winnie Mandela mwaka 1992. Winnie anadai iko siku ataongea juu ya mahusiano ya watu hawa wawili.

Graca alibarikiwa kupata watoto 7, ambapo wawili ni wa kuzaa mwenyewe na watano ni wa wake wawili wa kwanza wa Samora. Hadi leo hii Graca ameweka rekodi ya kuolewa mara mbili na marais wawili mashujaa wa nchi tofauti tena katika ndoa zote akiwa ni mke wa tatu.

4 Comments:

At Monday, 29 May 2006 at 05:59:00 BST, Blogger Mija Shija Sayi said...

Zemarcopolo nimekupata na nimejitahidi kupiga mahesabu nikajikuta nachanganyikiwa, sasa hebu tusaidiane hapa hizo hesabu zako umezipigaje?

Halafu kila nikija kibandani kwako mbona nakuta pamefungwa?..tunaomba utufungulie tuingie.

 
At Monday, 29 May 2006 at 08:31:00 BST, Blogger Simon Kitururu said...

Hivi huyu mama shujaa na Winnie Mandela wanapatana kweli?

 
At Monday, 29 May 2006 at 14:59:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Mija, asante kwa makala hii. Nadhani hakuna ubaya nikitumia baadhi ya nondo hapa kwenye ukurasa wake wa kamusi elzo ya kiswahili.

Nakuunga mkono kuhusu Zemarcopolo.

 
At Tuesday, 30 May 2006 at 05:26:00 BST, Blogger Mija Shija Sayi said...

Kitururu, hao wawili hawapatani!! hiyo ninauhakika.

Ndesanjo jisikie huru kutumia nondo kadiri utakavyoweza.

Zemarcopolo tunakuombea hilo jukumu liishe haraka na salama ili ujiunge na treni yetu.

 

Post a Comment

<< Home