Nani Zaidi......
Bado najiuliza sijui kwa nini MtiMkubwa anaogopa kufungua blogu yake, majuzi amenitumia waraka huu ili wote tujadili kihoja hiki cha wabunge...haya endelea hapo chini.
"Kuna wakati nikikaa nikawaza mambo ya Watanzania nashindwa kupata jibu. Leo nimefikwa na jambo ambalo nimeshindwa kupata jibu. Kwa wale wenye nafasi naomba msomee habari hiyo hapo chini halafu mnisaididie majibu: Maswali niliyojiuliza "..Kati ya mbunge na daktari nani anastahili kulipwa mshahara mkubwa?..Halafu Mheshimiwa Kimiti anaposema "..madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote.." Kama ni kweli?
Wabunge wataka kukata ’keki’ zaidi ya taifa
2006-01-26 08:38:24
Na Mashaka Mgeta
Baadhi ya Wabunge wamechachamaa na kuitaka serikali iwaongezee mishahara, posho na marupurupu ili kuwawezesha kuwatumikia wapiga kura wao kwa ufanisi zaidi.
Lakini kwa upande mwingine wametaka madai hayo hayo yasiandikwe au kutangazwa katika vyombo vya habari, kwa maelezo kuwa zitachochea hisia mbaya na kuwafanya wasikubalike kwa wapiga kura wao.
Wabunge hao walitoa mapendekezo hayo jana walipokuwa wakichangia mada kuhusu masharti ya Mbunge iliyotolewa na Katibu Mkuu Kiongozi, Bw. Philemon Luhanjo katika semina ya mafunzo inayoendelea jijini Dar es Salaam.
Hata hivyo, Bw. Luhanjo aliwaonya wabunge dhidi ya madai yao hayo na kuwataka wazingatie maslahi yanayokidhi matakwa ya usawa kwa wananchi wote katika kugawana pato la taifa linalotokana na vyanzo mbalimbali zikiwemo shughuli za uzalishaji mali zinazofanywa na wananchi.
Alisema hatua ya kudai maslahi bora zaidi kuliko ya watumishi wengine, ni sawa na kuonyesha ubinafsi aliouita kuwa ’collective selfishness’.
Akichangia mada hiyo, Mbunge wa Sumbawanga Mjini, Bw. Paul Kimiti alisema madai yao yanatokana na ukweli kuwa wabunge wana majukumu mengi na makubwa ya kuwahudumia watu kuliko watumishi wengine wote.
Bw. Kimiti aliwaonya wabunge wasilichukulie mzaha dai hilo wala kulionea aibu kwa kuwa ni miongoni mwa masuala nyeti yanayowahusu.
Mbunge huyo wa siku nyingi, alisema suala la kudai maslahi bora kwa wabunge liliwahi kufanyika pia mwaka 1980 ambapo Spika wa sasa, Bw. Samwel Sitta, Naibu Spika, Bi Anna Makinda na yeye (Kimiti) walikuwa miongoni mwa wabunge waliokuwa kwenye kundi la kudai maslahi hayo.
Hata hivyo alisema madai hayo yalitoweka baada ya wajumbe kadhaa wa kundi hilo ’kutunukiwa’ Uwaziri katika serikali ya awamu ya pili.
Bw. Kimiti alisema madai hayo ni muhimu kwa wabunge kwa vile Wakuu wa Mikoa wanapata kiasi kikubwa cha fedha kwa ajili ya shughuli za hamasa zenye mwelekeo wa kisiasa kwa wananchi.
Kwa mujibu wa Bw. Kimiti, hivi sasa wabunge wanapata mshahara wa Sh milioni 1.2 na kiasi kingine cha takribani Sh milioni moja kila mwezi kwa ajili ya kufanikisha huduma jimboni, fedha ambazo hazihusiani na posho na marupurupu mengine wanayoyapata kwenye vikao vya bunge, vikao vya mabaraza ya madiwani na wanapokuwa safarini.
Naye Naibu Waziri wa Elimu Bw. Ludovic Mwananzila alisema hatua ya wananchi kulalamika wakati wabunge wanapodai ongezeko hilo inatokana na uelewa wao mdogo walionao kuhusu wajibu wa Mbunge.
Bw. Mwananzila alisema uelewa kama huo unachochewa na waandishi wa habari wanapoandika ama kutangaza habari zinazohusu madai ya ongezeko la maslahi ya wabunge, na hivyo kuwafanya (wabunge) wasikubalike kwa wapiga kura.
Alisema kutokana na hali hiyo, habari zinazohusu madai ya wabunge kutaka ongezeko la mishahara, posho na marupurupu hazipaswi kuwafikia waandishi wa habari wala kutangazwa au kuandikwa kwenye vyombo vya habari.
Pia Bw. Mwananzila aliiomba serikali kutoa waraka maalum wenye lengo la kuwashawishi wananchi waamini kuwa posho za wabunge ni kwa ajili ya matumizi kama vile ya kununua mafuta ya magari yao na siyo vinginevyo.
Naye Mbunge wa Iramba Mashariki, Bw. Mgana Msindai alisema alisema ongezeko hilo ni muhimu kwa vile litakuwa linakidhi mahitaji yao.
Bw. Msindai aliyataja baadhi ya mahitaji hayo kuwa ni kulala kwenye hoteli zinazostahili wanapokuwa kwenye misafara ya Mawaziri wanaposafiri ndani ama nje ya nchi na kuwa na magari yenye hadhi isiyopungua Sh milioni 50.
Kwa upande wake, Mbunge wa Bahi Bw. William Kusila alisema wabunge ni hazina ya ufumbuzi wa matatizo ya wananchi hivyo wanapaswa kupata ongezeko la mishahara, posho na marupurupu.
Katika kuchangia hoja hiyo, Bw. Kusila aliwahimiza wabunge wapya kuunga mkono madai ya kuongezewa posho, mishahara na marupurupu ili wamudu kuwahudumia wapiga kura wao vinginevyo wasitarajie kuchaguliwa tena.
Bw. Kusila alisema watu wanaopinga hoja za madai ya ongezeko hilo wana kile alichokiita ’wivu wa jumla’ na kwamba hawana mapenzi mema na wabunge.
Naye Mbunge wa Rufiji, Profesa Idrissa Mtulia alisema wabunge na familia zao, wanastahili kutibiwa kwenye hospitali zenye hadhi ili kupata huduma mapema na hivyo kuwa na wakati mzuri wa kurejea kwa wapiga kura wao.
Hata hivyo, mbali na kuwataka wafikirie kuhusu haki ya mgawanyo sawa wa pato la taifa, Bw. Luhanjo aliwahakikishia wabunge hao kuwa, pamoja na mambo mengine serikali itazifanyia kazi hoja zao.