28 October 2005

Uchaguzi wahailishwa....

Kutokana na kifo cha mgombea mwenza wa chama cha CHADEMA, Bwana Jumbe Rajab Jumbe uchaguzi wa Tanzania umehailishwa kutoka 30 oktoba hadi 18 disemba. Soma hapa na hapa upate habari zaidi. Poleni CHADEMA, poleni wananchi. Kifooo kifooo kifo hakina huruma!!

27 October 2005

Mchina amtwanga ''hedi'' mbantu na kuzirai.

Jamanieee! sasa watanzania tumezidi, inakuwaje mgeni anayekujia nyumbani akutawale wewe mwenye nyumba??!! na wewe mwenye nyumba unakubali tu ni wogaaa au utumwa?

"MtiMkubwa" Fidelis Tungaraza, amenipatia habari hii niilete kwenu wasomaji ili kwa pamoja tuweze kujadili tatizo letu ni nini hasa, ameanza kwa kuhoji hivi
Mimi nilifikiri kizazi cha wale watanganyika waliombeba Dr Livingstone tena akiwa kafa kilikwisha! La hasha! Kumbe wajukuu zao bado tupo na tunaendeleza waliyoyafanya! Nilipokuwa chuo cha sanaa Bagamoyo, nilikuwa nikienda kanisani na kutazama pale mahala aliposimama wale watanganyika waliombeba mfu Dr Livingstone na kuwaambia wazungu wenziye kwamba "..Bwana amefariki.." Nilikuwa sipati majibu kwamba: Wale watanganyika walikuwa na utu sana??, Au walifanya vile kwa sababu walikuwa wanataka walipwe mishahara, marupurupu, mafao na pensioni zao kwa kukileta kidhibiti cha maiti?? Au walimpenda sana hayati Dr Livingstone? Au walikuwa wafanya kazi watiifu na waaminifu kwa mwajiri wao? Au walikuwa kama waswahili wasemavyo mafala?? Au walikuwa wapumbavu kupindukia?? Au kama uchawi upo walikuwa wamelogwa??

Siku zilizopita nilikarahishwa na habari kama hii kwenye gazeti la Dar Leo, (www.bsctimes.com). Habari hiyo ilikuwa na kichwa cha habari "ASKARI WA KIINGEREZA WAUA CHANGUDOA". Habari hiyo niliituma kwa baadhi yetu na na kwa Mheshimiwa Waziri Omar Mapurina Balozi Abdulkadir Shareef ili kwamba ichukuliwe hatua. Sijui kama kuna hatua iliyochukuliwa. Leo nimekumbana tena na habari za kabila hiyo hiyo yenye kichwa cha habari. MCHINA AMTWANGA AMTWANGA 'HEDI' MBANTU NA KUZIRAI. Kuna tusi limeniijia lakini nalihifadhi, hivi ingekuwa MBANTU KAMPIGA 'HEDI' MCHINA NA KUZIRAI ndani ya mitaa ya Beijing huyo Mbantu angekuwa hai mpaka saa hizi?? Leo imenipasa kusema kwamba wajukuu wa wale Watanganyika bado tupo, baada ya kukumbana na taarifa hii kwenye gazeti la Nipashe. Hebu jisomee mwenyewe hapa.

21 October 2005

Hakutaka mchezo Nyerere!

Kipindi kama hiki miaka sita iliyopita Tanzania ilikuwa bado katika maombolezo ya kuondokewa na hayati baba wa taifa Mwalimu Nyerere. Ni katika kipindi hiki habari nyingi za mwalimu zilianza kutoka wazi wazi, za ndani na nje ya familia.

Habari ambayo ilinivutia kuliko zote ni hii ya mtoto wake wa kiume. Kwanza kabisa habari hii nilihakikishiwa ni ya kweli kabisa......., kwamba mmoja kati ya watoto wake wa kiume alikuwa akisoma katika sekondari moja huko mjini Mbeya, (inasemekana mwalimu aliwasomesha watoto wake katika shule hizi hizi za kawaida tulizokwenda mimi na wewe). Sasa huko shuleni huyo mtoto akawa anataka kuleta zile za mimi mtoto wa Nyerere, utundu na kutokusikia(si unajua tena utoto!. Basi siku moja yeye na wenzie wawili waliamua kutoroka usiku kwenda kujivinjari mjini, wakiwa huko wakakamatwa na mwalimu wao duh! hawana la kusema wala la kujitetea. Alichofanya mwalimu yule ni kumtaarifu mkuu wa shule, naye mkuu wa shule usiku ule ule akapiga kengele wanafunzi wote washuke kuja kufanya "lokoo", basi lokoo ilipopita wenyewe kweli hawakuwepo wengine wakatawanyika kwenda kulala huku wakisubiri kusikia kesho yake itakuwaje? maana na mtoto wa Nyerere alikuwemo, atarudishwa kama wengine ambavyo huwatokea au??

Basi ile kesho yake kila mtu anamtazama mkuu wa shule ataamuaje, mkuu wa shule hata hakuwa na mengi, alichosema ni kwamba wanafunzi hawa watatu wamekosa nidhamu na heshima, wametoroka usiku kinyume na sheria ya shule hivyo wataadhibiwa kwa kurudishwa majumbani kwao na kurudi hapa shuleni baada ya miezi mitatu kila mmoja na mzazi wake.

Wanafunzi ikabidi warudi makwao....kilichotokea huko kwa Nyerere na mwanae haijulikani, ila siku ya kuripoti ilipofika, mzee kifimbo akawasili bila kuchelewa yeye na mwanae. Akakaribishwa na mkuu wa shule ofisini na mazungumzo yalikuwa kama ifuatavyo:-

Mkuu: Ndugu mzazi, kama ulivyosoma barua tuliyokuletea, mwanao ilibidi tumpe adhabu
hii kutokana na utovu wake wa nidhamu, hii ilikuwa ni adhabu ya kwanza, ya
pili ni kupata viboko mbele ya wanafunzi wote ili iwe ni fundisho kwa wengine.

Mwalimu nyerere: (Kwanza alimtizama juu hadi chini yule mwalimu mkuu, kisha
akasimama na kumpa mkono)...Kwa kweli mwalimu wewe ndio hasa watu
ninaowataka mimi....(akiendelea) Unajua huyu aliporudi nyumbani
nilishtuka, nilishangaa na kujiuliza... ni mwalimu gani huyu
mwenye kuweza kuniita mimi shuleni kwa ajili ya mtoto....nikasema
mwalimu huyu ndiye hasa anayejua kazi yake. Wewe kama mwalimu wa
mwanangu mimi kwako ni mzazi na sio Rais, una uwezo wa kuniita
wakati wowote. Na titahakikisha nawawajibisha waalimu wasiojua
kazi kazi zao na kuogopa na kuwanyenyekea watoto wa viongozi wa
nchi.

Baada ya pale kengele iligongwa, wanafunzi wote wakatoka kushuhudia fimbo. Kwa kawaida ilikuwa ni mwalimu mmoja ndiye humchapa mwanafuzi lakini siku hiyo mwalimu mwenyewe aliikamata fimbo. Baada ya hapo ulipita mwezi mmoja yule mwalimu mkuu akapandishwa cheo na kuamia Wizara ya elimu huku Mwalimu Nyerere akisema nataka wawajibikaji kama hawa sio waoga waoga.

Wasomaji hiki kipindi nadhani ndio kilikuwa cha uwazi na ukweli. Kufanya kile ambacho unajua ni haki bila ya kuwa na wasiwasi wa kufukuzwa kazi. Sijui ni kwanini Haki elimu imeundwa baada ya Nyerere.

17 October 2005

MtiMkubwa!!!!!!!

F.T kijana machachali sana, ni yule aliyeleta hoja ya "binadamu ni sawa lakini si sawasawa" nenda hapa utafute aliyosema,kwa wale waliobahatika kukumbana naye watakubaliana nami. Mara yangu ya kwanza kumsikia ilikuwa miaka 12 iliyopita pale chuoni sanaa bagamoyo, ndio kwanza nilikuwa naanza chuo. Basi ile kutua tu, tukapata stori...bwana...bwana ...alikuwepo Fide Tungaraza hapa chuoni....na sisi tuko enhe..., wakuda wakaendelea.... bwana sijui kama tutakujapata msanii kama yule..., jamaa hatari sana yule, kwanza korofi, pili limejaaliwa kichwani, tatu jukwaani kama hakupanda basi watazamaji watatoka wakilalamika.....,iko siku alitoa kituko jukwaani ilibidi mchezo usimame kwa muda kwani wahusika walishindwa kuhimili na wote kuangua kicheko kosa ambalo ni kubwa sana jukwaani (kutoka nje ya husika yako), lakini siku hiyo hata mwalimu alisamehe kosa. Basi hayo ni machache tu ya huyu bwana Tungaraza.

Turudi katika nilichotaka kukizungumzia leo, ni hili jina lake lingine la "Mti mkubwa". Binafsi ni juma lililopita ndio nimejua kuwa ana jina jipya la Mti mkubwa.
Nililitizama hili jina..., nikamtizama na mtu mwenyewe, nikawa sipati maana hasa ya chanzo chake, nikaona nimwandikie nimuulize...

Mti mkubwa hivi jina hili la Mti mkubwa chanzo chake ni nini hasa??

Jibu alilonipa nimeona nisilifaidi peke yangu, hili hapa chini:

BIBIE JINA LA MTI MKUBWA NILIPEWA KWA SABABU YA WASIFU WAKE:

1. Kuwa na matawi mengi, mtimkubwa mrefu sana kwamba ukifika kileleni kwangu
utaona mengi kwa upeo wa mbali.

2. Nina shina pana hivyo huwezi kunikwea kwa hiyo lazima unipande.

3. Shina hili pana ukitaka kulikata ni lazima uwe na vifaa madhubuti, vinginevyo
utakuwa unajisumbua na kupoteza nguvu zako bure.

4. Shina hili pana huwezi kulifumbata wala kulikumbatia kwa hiyo lishike
unapofikia,
usipofikia paache kama palivyo.

5. Mti mkumbwa una mizizi mirefu huwezi kuning'oa kiurahisi, mizizi yangu
imejikita
kinani sana kwa hiyo siyumbishwi wala kuangushwa na upepo wala vimbunga.

6. Majani mapana ya mtimkubwa mazuri kwa kivuli, watu wengi huja kujipumzisha
chini ya mtimkubwa, mtimkubwa nyumba vijidudu vidogovidogo, majoka ya namna kwa
namna na ndege wenye rangi na sauti nzuri.

7. MtiMkubwa huu hauzai matunda yaliwayo lakini hata ukiyala si sumu hayakuui.

Haya sifa hizo ndio chanzo cha U-MtiMkubwa kwa kaka yetu. Hii sifa ya saba hii, akili yangu inaniambia ni fumbo la imani, tungependa aifafanue kidogo.

Udumu MtiMkubwa, tutajifunza mengi kutokana na sifa hizo.

03 October 2005

Binafsi sikubaliani kabisa na adhabu hii....

Siwatetei na wala sijapendezwa na kitendo walichokifanya wanafunzi hawa mabinti wawili. Lakini tukiangalia kwa jicho la undani adhabu hii ya kufukuzwa shule kwa wanafunzi hawa tena wakiwa wamebakiza juma moja la kufanya mitihani yao ya kuhitimu kidato cha nne, imetolewa bila kuangalia madhara yake kwa watoto hawa hapo baadaye. Kwanza kabisa tumesha poteza labda maprofesa wa kesho, maana huwezi kujua mikakati yao ya maisha walikuwa wameipangaje, pili kitaifa badala ya kubembeleza watoto wasome ili tupate taifa lenye watu waliofunguka fikra, sisi tunawakatiza kwa makosa yanayotokana na utoto wao (nina hakika wako chini ya miaka 20, na hiki ni kipindi kibaya kwa vijana kutaka kujaribu mapenzi hapa na pale) wenzetu wa nchi zingine hawaleti mchezo katika masuala ya elimu, hivi vimakosa vya mpito hutatuliwa kwa njia nyinginezo ambazo pia humjenga mtoto. Tatu huko jamiini wanakokwenda ndio watakuta wameshanyanyapaliwa tayari, ile kufika tu na vidole kila mtu juu yao, hapo tumeshaua tayari kujiamini na kujidhamini, na kutokana na umri wao wataanza kujiona kwamba hawafai na si kitu katika jamii na hapo huwa ni ngoma kumsawazisha mtu.

Sawa, lakini na hao wanaume, watu wazima na wake za watu wamepewa adhabu gani?
Kisa chenyewe hiki hapa.

01 October 2005

Da mija


Foto 92, originally uploaded by mamanganga.

Sema usikike.

Da Mija.