07 July 2005

KUMZOEA MUNGU.

Sijui kama na wenzangu mmeliona hili. Mimi huliita kumzoea Mungu, suala hili ni kwa wakristo waliookoka, nimekuja kugundua kwamba walokole walio wengi humuogopa Mungu katika siku za awali za wokovu wao, lakini kadiri siku zinavyoendelea watu hawa hujisahau na huanza kumzoea Mungu kwa kurudia matendo yao ya zamani lakini wakiwa chini ya kivuli cha wokovu kwa maana ya kusali sana lakini bila kuwa makini kwamba matendo nayo yalitakiwa yabadilike.

Nina vielelezo vingi ambavyo vimekuwa vikinitatanisha, mfano mmojawapo ni ukosefu wa upendo wa dhati na kujaa kwa dharau kwa walokole dhidi ya wale wasiookoka. Binafsi naunga mkono kabisa suala zima la wokovu, lakini vile vijitabia vya walokole nasema vinahitaji kukemewa kwa jina la Yesu, utakuta familia hizi zina wakataza watoto wao kufanya urafiki na watoto wa imani zingine kwa kusema kwamba wataharibika tabia, na si kwa watoto wao tu, bali hata wao wenyewe utakuta urafiki wao ni wa wenyewe kwa wenyewe, hata kutembeleana ni kwa wao kwa wao, ukiuliza utaambiwa wale ni watu wa mataifa, kweli sikatai ni watu wa mataifa lakini je? tunategemea watu hawa wa mataifa watayaachaje mataifa hayo bila ya kujichanganya nao na kupata kujua wokovu ni kitu gani? Yesu mwenyewe enzi zake hakushughulika kabisa na wale waliokwisha kuwa wake, kila siku alijichanganya na wale wa vijiweni ili nao wapate kumjua na ndio sababu alisema 'wenye afya hawahitaji daktari bali wagonjwa' hii ni baada ya walokole wa enzi hizo pia kumshangaa kwamba ni kwa nini anajichanganya na vibaka na walevi na wazinzi.....mlokole wa sasa hivi aunde urafiki na mzinzi ....dhubutuu!! hawajui tu hiyo ni dhambi tosha ya kumbagua badala ya kumsogeza karibu ili na yeye abadilishe tabia.

Tabia nyingine ya kumzoea Mungu ni kwa waumini hawa kugeuza makanisa uwanja wa maonyesho ya mavazi, simaanishi kwamba kanisani usipendeze la hasha! pendeza lakini usifikie hatua kwamba huendi kusali eti kwa sababu sina nguo nzuri ya kuvaa, kina fulani watanicheka...na ni kweli kuna walokole ambao kazi yao ni kuangalia fulani kavaa nini leo.... fulani hajui kuvaa, jamani huku kama si kumzoea Mungu ni nini? haogopwi tena, watu wanafanya yale wanayojisikia kufanya, alimradi kivuli cha wokovu kiko mbele yao.

Utakuta mchungaji haamini kama watu wengine wasiookoka wanajua kusalisha, kipindi fulani mchungaji fulani alikuja nyumbani kwetu kututembelea, saa ya chakula ikafika tukamwambia mmoja wetu asalishe kabla ya kula, mchungaji akadakiza kwani na nyie mnajua kusali!! tulibaki na butwaa... kwamba kumbe hata kusali kuna utaalamu wake??

Ni mengi mno niliyoyaona kama kugombea madaraka, vinyongo, uzinzi baada ya mazoezi ya kwaya...Mungu alisema wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho wa kwanza, tujiangalie sana. Ni lazima tujifunze kuishi kwa kujitathmini, kila siku kabla ya kulala ni vizuri ukajiuliza matendo niliyoyafanya leo yamemsaidia yeyote kubadili tabia yake kuwa nzuri au la? binafsi nina tabia ya kujiuliza kwamba..hiki kitu ninachokifanya angekuwa Yesu angefanya? jibu nilipatalo ndo hunifanya niendelee au niache kufanya jambo nilifanyalo.

Hivyo basi kila mara tujue Shetani yuko nasi na hasa ukiokoka, hivyo tuwe makini sana.

3 Comments:

At Sunday 10 July 2005 at 12:03:00 BST, Blogger Indya Nkya said...

Kuna ulokole kama kikundi au kilabu ambacho mwanachama ni lazima uhudhurie, utoe sadaka, unene kwa lugha nakadhalika. Suala si kama unafanya yanoyompendeza mungu na binadamu wenzako, la hasha. Suala ni uanachama. Fanya utafiti na utagundua kuna watu wenye kufanya mambo ya hekima, busara na yanayopendeza bila hata kuwa na dini za kuja achilia mbali uiigizaji wa kilokole.

 
At Monday 11 July 2005 at 11:03:00 BST, Blogger Ndesanjo Macha said...

Sina la kusema zaidi ya kucheka...kumzoea mungu!!

 
At Saturday 16 July 2005 at 17:11:00 BST, Blogger Rama Msangi said...

haya mambo mengine ndugu yangu ni ya kuyaacha kama yalivyo maana hata kusema unaona shida kusema, hivi unajua mimi hata hiki kitu kinaitwa kuokoka sijui maana yake hasa ni nini??

 

Post a Comment

<< Home