01 June 2005

Kujitambua nguzo ya ukombozi wa mwanamke.

Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza, hivi ni kwanini watu wengine wanafanikiwa maishani mwao na wengine hawafanikiwi, zamani nilikuwa nafikiri kwamba Mungu huandikia watu hivyo, kwamba huyu ni wa kukosa na huyu ni wakupata, dhana ambayo haina ukweli wowote. Ukweli ni kwamba kupata au kukosa kwa mtu kunatokana na yeye mwenyewe kwa ufupi ni mtu mwenyewe ndiye anayechagua apate au akose, najua utajiuliza ni kwa vipi mtu achague kukosa? basi mtu huyo kidogo zitakuwa zimeruka....laa hasha!! utakuta mtu mzima na akili zake lakini ndio kachagua kukosa. Kwa vipi basi?? ....Kwa kutojitambua.

Kujitambua ni nguzo kubwa, muhimu na ya kwanza katika maisha ya binadamu. Sina hakika kama wengi wetu hujiuliza, je mimi ni nani?, ninapenda na sipendi nini?, ninaweza na siwezi nini?, nina malengo gani katika maisha yangu, nina wajibu gani katika maisha yangu kwa watu wengine n.k. Maswali haya au mambo haya ndio humuamulia mtu kuwa wa namna gani, au wa tabia gani, kwani mwelekeo wa maisha ya mtu hutokana na yeye anawaza nini hasi au chanya.

Tukirudi katika suala la wanawake kwa nini bado tunapiga danadana pale pale, sababu kubwa ni hii ya kutojitambua wenyewe, tunaiachia jamii ituambie sisi ni kina nani, tunaweza nini, hatuwezi nini, tunapenda nini hatupendi nini, wajibu wetu ni upi na upi si wajibu wetu na mengine meeengi, tumekingwa na wingu la giza na sisi tukalikubali, kitu muhimu kina mama tunatakiwa tukitambue ni kwamba hakuna mtu anayeweza kumtambua mtu mwingine zaidi ya yeye mwenyewe anavyojitambua, wewe ndio unajua unawaza nini sasa hivi, unaumwa au huumwi, unasikia njaa au husikii. Hivyo tuache kabisa tabia ya kusubiri kuambiwa wewe sasa hivi unasikia njaa...kula, au wewe unaumwa kunywa... dawa.

TUJITAMBUE JAMANI NA MATOKEO YAKE TUTAYAONA.

0 Comments:

Post a Comment

<< Home