15 May 2005

Mkombozi wa mwanamke ni elimu.

Nakumbuka enzi zetu za Nganza sekondari, ambapo wengi wetu tulikuwa tukiuchezea wakati kwa madai kwamba kuna wanaotusomea. Utakuta mwanafunzi anakacha vipindi vya masomo na kujificha bwenini bila sababu yoyote ukimuuliza atakwambia...achana na mimi mwenzio nasomewa, utakapohoji zaidi atakwambia nyie hangaikeni tu, lakini mjue mwanamke mwisho wake ni kuolewa, kuzaa na kulea wanae sasa kwa nini nijisumbue?

Enzi hizo dhana hii, nilikuwa nikiichukulia juu juu, sikuwahi kabisa kukaa na kuitathmini kiundani nini faida na madhara yake, nina hakika haina faida hata kidogo kwani matokeo yake sasa yanajionyesha waziwazi kabisa, kwa mfano tukiangalia suala la ujasiri na uthubutu wa kufanya jambo kati ya mwanamke na mwanaume, tunaona kwamba kuna tofauti kubwa sana, kama ni nafasi kumi zimetolewa, basi utakuta wanaume saba na wanawake watatu au hata chini ya hapo. Na hii si kwa sababu wanawake wamezaliwa hawawezi bali ni kutokana na mbegu iliyopandwa siku nyingi vichwani mwao kwamba wao ni wa kusomewa hivyo wasubiri tu. Na ni hapa ndipo ninapoona maana ya ule usemi usemao utavuna ulichopanda, wanawake sasa hivi tumebaki tukilalamika kwamba tunaonewa na wanaume,...kwamba kwanini kiuwiano wanaume ndio wameshika nafasi zilizo nyingi na za juu kimadaraka,....lakini hebu tuangalie ule ukweli wanawake wenzangu, hivi hizi nafasi wanapeana tu bila ya kuwa na kitu kichwani??....tukumbuke ule wakati wa kuingiza vitu kichwani tulivyokuwa tukiuchezea, na haya ndio matokeo yake.

Kwa upande wa wanaume, wao nao enzi hizo kwa kujua wanasomea watu, basi walijitahidi kwa kila njia kusoma wakijua kuna majukumu mazito ya kuisimamia familia, na hii ndio imewafanya wawe jasiri na wenye uthubutu, kwa sababu mbegu iliyopandwa kichwani mwao ni ya kupambana. Na bahati mbaya zaidi hata hao waliokuwa wakitusomea wameshtuka, hawataki mambu-mbu-mbu.

Jambo la kujifunza hapa wanawake wenzangu, ni kuanza kushughulika na mizizi na si matunda, ukikata mizizi matunda hayataendelea kuzalika na mti hauna ujanja tena utakufa tu. Na mti ukishakufa tunapanda mpya kwa makini zaidi. Ni lazima tuiweke elimu mbele, ni lazima tujifunze uvumilivu wakati wa kuipata hiyo elimu na hapo ndipo ndipo mambo yatakaposawazika yenyewe bila hata kuyapigia mbiu.

2 Comments:

At Monday, 16 May 2005 at 12:47:00 BST, Anonymous Anonymous said...

umesema.Lakini kuna swali moja, kwanini wanakwake huwa wanalaumu wanaume sana wakati wao kwa wao wanawekeana sana kauzibe?????

 
At Monday, 23 May 2005 at 00:38:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Hoja ya kutazama mizizi kwanza na sio matunda nzuri sana. Na haya mawazo ya kusomewa yanatakiwa kutupwa chooni.

 

Post a Comment

<< Home