23 June 2005

Malengo katika maisha.

Mafanikio yoyote yale ya binadamu huletwa na malengo thabiti yanayoambatana na ufuatiliaji wa kina. Kuwa na malengo katika maisha yetu ni jambo la muhimu sana kwani malengo ndo humfikisha mtu pale alipodhamiria kufika. Ninaamini kila mtu ana malengo yake katika maisha, lakini watu wachache tu ndo huyatimiza malengo yao. Nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini watu wengi hawayafikii malengo yao, na nimekuja pata jibu kwamba watu hushindwa kuyafuatilia malengo malengo yao, ni rahisi sana kupanga jambo lakini ni ngumu sana kulifanya hilojambo litokee, hii ni kwa sababu ya kutokutaka kusumbuka wala kutumia muda mwingi katika jambo fulani. Hivi ndivyo tulio wengi tunavyoishi.

Leo nitaongelea jinsi ya kufuatilia malengo ili kuyafikia malengo.
Kwanza kabisa ni kujua jinsi ya kuutumia muda wako wa siku nzima, tangu unapoamka hadi utakapolala, panga ratiba nzuri na usiruhusu vitu visivyo na maana kukuingilia katikati, mfano tuseme leo umepanga utapalilia bustani yako yote, basi badala ya kufanya hivyo mara moja wewe utashika jembe utalima kidogo, utasema ngoja nikanywe maji ndani ukiingia ndani unakuta kakipindi kazuri kwenye luninga, unasema ngoja nitizame kidogo hako kanakugharimu dakika kumi, unapotaka kurudi bustanini unaona ngoja umpigie simu shoga yako kumweleza uliyoyaona kwenye luninga, hiyo inachukua robo saa maana zinazuka na stori zingine za nani kafanya nini na mambo mengine meeengi, ukija kutahamaki ni saa saba mchana labda unatakiwa uandae chakula kwa wanao na mambo mengine, hapo upaliliaji inabidi usitishwe hadi kesho bila sababu yoyote ya maana, ule muda wa kesho ambao ungeutumia kwa mambo mengine unajikuta unautumia kutimiza mambo ya jana yake na si ajabu siku hiyo tena ikapita bila kufanya lolote na kujikuta unamaliza wiki nzima bila kufanya lolote la msingi. Mambo haya madogo madogo ndio hutufanya tushindwe kufikia malengo yetu makubwa ya maisha yetu.
Kuwa na malengo katika maisha haikusaidii tu kufanikiwa katika maisha yako bali pia kuepuka mikumbo. Mara nyingi watu wengi hujikuta katika kundi la kufuata mkumbo kutokana na kushindwa kujiwekea malengo binafsi ya yeye kama yeye, utakuta mtu anafanya jambo fulani kutokana na kumuona mtu fulani anafanya jambo hilo kwa mafanikio, kwa mfano hili suala la sanaa ya muziki kwa vijana, utashangaa siku hizi kila mtoto anasema anataka kama Juma Necha au Jeidii, ukimuuliza kwa nini atasema kwa vile anaimba vizuri na amekuwa maarufu , jamani tuelewe kila mtu ameumbwa kwa ajili ya kutimiza jambo fulani hapa duniani, Juma necha amekuwa Juma Necha kwa sababu alikaa akatafakari yeye binafsi anataka nini, anaweza nini na je anayapenda hayo anayoyataka nakuyaweza? alipopata jibu ndio, hapo akaanza utekelezaji na hii ndio sababu kubwa ya mafanikio yake...'kufanya jambo analolisikia rohoni ni lake'.

Hivyo ndugu zangu tuanze kujirekebisha sasa kwa kuanza kusikiliza nafsi zetu zinasema nini, halafu kuweka malengo kwa hayo tunayoyapata katika nafsi zetu na lamuhimu zaidi ni kufuatilia utekelezaji ili kuyatimiza malengo hayo. Kama tukifanya hivi wengi wetu tutafika mbali na vipaji vingi vitaibuka.

2 Comments:

At Monday 27 June 2005 at 09:30:00 BST, Blogger mwandani said...

Si utani.

 
At Tuesday 5 July 2005 at 22:59:00 BST, Anonymous Anonymous said...

ulichosema, sema tena na tena.

 

Post a Comment

<< Home