01 October 2007

Malkia Nzinga Mbande wa Angola.


Nikiwa katika harakati ya kukusanya habari za wanawake waliotia fora duniani, nimeona niirudishe habari hii niliyoiandika hapo nyuma 2005 wakati nikianza kublogu hii ni kuwapa fursa wale ambao hawakuweza kuisoma nao wapate kumfahamu mama huyu, haya endelea...

Kama ukibahatika sasa hivi kukutana na Mreno, wewe jifanye kama unamchokoza juu ya wanawake wa afrika kwamba hawana lolote na hawawezi lolote, uone atakavyokushangaa, na bila shaka atakutupia swali kwamba unaishi dunia gani wewe?

Wasomaji msishangae, kwani aisifiae mvua...imemnyea. Hii yote imetokana na mwanamke mmoja jasiri, shupavu, mwenye akili sana na asiyetaka kuonewa wala kudharauliwa, si mwingine ni Malkia Nzinga Mbande. Mwanamama huyu aliyezaliwa mwaka 1583 na kufa 1663, alikuwa ni mtoto wa chifu na aliishi kipindi ambacho biashara ya utumwa ndio ilikuwa imepamba moto kwelikweli, kwa bahati mbaya baba yake alifariki na hivyo kaka yake mkubwa bwana Ngola Ngoli Mbandi akarithishwa madaraka ya baba yake. Mm! kaka huyu bila shaka aliguna kwa kujua kabisa kasheshe analotakiwa alikabili la kuwazuia wareno kuingia nchini kwao, lakini afanyeje na yeye ndio mwanaume na kama inavyojulikana kwa wengi mwanaume anaweza kila kitu na daima si mwoga, ikabidi ayavae madaraka huku akijua kabisa yeye ubavu wa kukabiliana na wareno hana na ni
mwoga kufa.

Dada yake, Nzinga baada ya kuona kaka yake anasua-sua ikabidi amwambie, kaka ni lazima uchukue hatua juu watu hawa na kuwazuia kuingia kututawala, lakini kwa vile kaka yake alikuwa mwoga ikabidi amwombe dada yake amsaidie, mara moja bila kuchelewa mwana mama Nzinga akaanza kuchukua hatua za utekelezaji na akafanikiwa kuwashawishi wareno katika kuandika mkataba wa makubaliano ya amani.

Tarehe ikapangwa ya kuweka saini makubaliano hayo, Kaka mtu kwa woga akakataa kwenda hivyo ikabidi Nzinga amwakilishe, akaenda na watumishi kadhaa lakini walipofika ndani ya ukumbi Nzinga akagundua kwamba hakuwekewa kiti yeye kama kiongozi wa nchi yake isipokuwa gavana wakireno peke yake, mwanamama akaona dharau gani hii? mara moja akapiga kofi na mmoja wa watumishi wake akaja mbele yake na kuinama magoti na mikono chini, Nzinga akakaa juu yake, kwa hiyo suala la gavana kukaa kwenye kiti peke yake likawa ngoma droo. Gavana akamtizama yule mama bila kummaliza na kubaki na aibu ya kuzidiwa maarifa tena na mwanamke, bila shaka alibaki akijiambia duh! kumbe wanawake nao wamo!!!

Nzinga baada ya kugundua kwamba kaka yake si kiongozi mzuri na hawezi kila kitu, alimfunga na kujitangaza kwamba yeye ndiye atakayeshika nchi kinyume na desturi ya nchi yao kwamba mwanamke haruhusiwi kushika wadhifa wowote wa uongozi katika serikali, minong'ono ya hapa na pale ilitokea lakini haikufika mbali kwani Nzinga alithibitisha ujasiri wake kwa vitendo. Na ni hapo ndipo umalkia wake ulipoanzia.

Kwa muda wa miaka arobaini ya uongozi wake, wareno walishindwa kuitwaa Angola hadi alipofariki, mwanamama huyu alijulikana na kuogopwa sana na ulaya nzima kwa mbinu zake thabiti za kijeshi, alijulikana kama mwanamke mpiganaji, jasiri na mwenye akili.
Hebu fikiria wareno, pamoja na kuwa na silaha imara na za kisasa ukilinganisha na za Malkia Nzinga, lakini walishindwa kuiteka Angola hadi Malkia Nzinga alipokufa.

Huyu kweli ni mwanamke wa shoka, na nina amini kila mwanamke anaweza kuwa mwanamke wa shoka, pale atakapoamua kufanya jambo kwa moyo na kuondoa uwoga. Hapa duniani kila jambo linawezekana, tatizo liko kwetu sisi wenyewe kutanguliza woga na kutokutaka kusumbuka.

8 Comments:

At Tuesday 2 October 2007 at 13:54:00 BST, Blogger luihamu said...

Da Mija naona kunatatizo kubwa sana tena sana,pili naona huyu mama alikuwa mnyanyasaji na si shujaa kwasababu kitendo cha kumkalia binadamu ni unyanyasaji na si ushujaa.

Hivi Da Mija leo hii uambiwe uiname then mtu akukalie utakubali?then huyo anakukalie tumuite shujaa,does it make any sence?

 
At Wednesday 3 October 2007 at 11:32:00 BST, Blogger Mija Shija Sayi said...

Luihamu hebu angalia mazingira yaliyompelekea kumkalia mtu, je yalikuwa na lengo la udhalilishaji?

 
At Thursday 4 October 2007 at 17:16:00 BST, Blogger luihamu said...

Alitaka usawa lakini akasahau kama kitendo alichofanya hakifai katika jamii.Da Mija unaposema mazingira yanasababisha mtu afanye kitu chochote?ni sawasawa na mvulana kamkuta penzi wake na mwanaume mwingine yeye amuwe kumkatakata mpenzi wake kwa kisingizio cha mazingira au?

 
At Sunday 7 October 2007 at 10:45:00 BST, Blogger Pius Ntwale said...

Da mija, nianze kwa kukupongeza kwa harusi nzuri, ninakutakia maisha mema na baraka za Mungu katika maisha mapya.
wadau tulifurahi kuona zile picha kwa kina michuzi mna mjengwa.Karibu unitembelee si unakumbuka ulinikaribuisha ndani ya ulimwengu wa blogu? nami sikusita kujiunga.
Wikiendi njema

 
At Monday 8 October 2007 at 18:23:00 BST, Anonymous Anonymous said...

wanaoppenda kucheza lottery ya kupata green card kuishi usa imeanza tarehe 3 na web ni hii
http://www.dvlottery.state.gov/

 
At Wednesday 17 October 2007 at 23:58:00 BST, Anonymous Anonymous said...

Damija, unapatikana vipi? Mbona email ya contact hamna?

 
At Sunday 21 October 2007 at 12:51:00 BST, Blogger Mija Shija Sayi said...

Anony hapo juu, samahani kwa kutoweka email yangu, nimeshaiweka nenda kwenye profile.

 
At Wednesday 21 November 2007 at 13:41:00 GMT, Anonymous Anonymous said...

Nimemsikia mwanamke huyu miaka mingi. Kuna mwingine wa Nigeria, alikuwa akiitwa Queen Amina of Zalia. Pia kuna mwanadada aliwahi tawala Russia enzi hizo, alitokea Poland aitwa Catherine The Great. Alitawala Russia na kuipeleka nchi kuzuri sana. Kuna movies hata vitabu vimeandikwa juu yake.

Wanawake wengi sana duniani wamefanya mambo ya ajabu ambayo hadi leo watu wengi wanafikiri ni wanaume ndio waliogundua. Kuna scientist mmoja Marie curie, mshindi wa Nobel nafikiri mbili au 3, amefanya mambo makubwa sana katika ulimwengu wa chemistry na physics.

Asante sana kuelimisha jamii

Mama Malaika
United Kingdom

 

Post a Comment

<< Home