14 November 2005

Anna Kajumulo Tibaijuka, Mwanamke Mtanzania.




Anna Tibaijuka, Mkurugenzi mtendaji wa shirika la umoja wa mataifa linaloshughulikia makazi duniani UN-HABITAT. Tangu kuanzishwa kwa shirika la umoja wa mataifa mwaka 1945, hakuna mwanamke mwafrika aliyewahi kushika wadhifa wa juu kama huu alioushika yeye sasa hivi.

Historia yake fupi inaanzia nchini Tanzania, mkoani Kagera, kijijini Kangaviyo ambako ndiko alikozaliwa. Alizaliwa wakati ambao watoto wa kike walikuwa hawathaminiwi kabisa, kabisa katika jamii, na katika familia yao walizaliwa watoto kumi, kati yao wanawake nane na wanaume wawili. Hivyo familia yao haikuwa na wakati mzuri, ilionekana ni familia iliyopata hasara....wanawake wanane???!!!...duh! lakini anasema kwa bahati nzuri baba yake alikuwa ni mtu mwenye mtazamo mwingine, na hakukubaliana na jamii kwamba watoto wa kike na hasara, alidiriki kuwaambia wanajamii kuwa siku hizi kuna kitu kinachoitwa elimu, na wasichana wangu ni lazima waende shule kama wavulana...ni lazima waendelee. Hivyo Anna alikwenda shule hadi hapo hapo kijijini kwao na baadaye alipata nafasi ya kujiunga na chuo kikuu cha Dar es Salaam.

Alipomaliza chuo kikuu cha Dar er salaam aliolewa na kupata watoto wanne, baadaye mumewe alipata uhamisho wa kikazi nchini Sweden, hivyo wakahamia huko yeye akiwa kama mama wa nyumbani. Lakini anasema mumewe hakuona vizuri kwa Anna kukaa tu nyumbani, hivyo alimshauri ajiunge na masomo ya juu. Anna akajiunga na chuo kikuu cha Uppsala nchini Swedeni ambako alihitimu mwaka 1984 na kupata shahada ya udaktari ya uchumi na kilimo. Baadaye alirudi Tanzania na kufundisha chuo kikuu cha Dar es salaam huku akijiendeleza hadi kuwa Profesa wa uchumi. Zaidi ya kufundisha chuo kikuu ameshafanya kazi na UNCTAD kwa miaka mitano.

Mwaka 2000, Katibu mkuu wa shirika la umoja wa mataifa Koffi Annan, alimteua mwanamama huyu kushika wadhifa huu alionao hadi leo.
Kutokana na wadhifa huu na uwezo wake wa kiutendaji kazi ameweza kushiriki katika midahalo mingi duniani. Pia ameshawahi kushiriki katika kipindi cha HardTalk cha BBC. Na hivi majuzi ameteuliwa na waziri mkuu wa Uingereza Tony Blair kuwa mjumbe wa Tume ihusuyo Afrika iliyoundwa na Bwana Blair inayoshirikisha wajumbe 17 watanzania wakiwa ni wawili Rais Mkapa na Tibaijuka. Hotuba ya Rais Mkapa juu ya tume hiyo hii hapa.

Anna Tibaijuka ni mwanamke mwenye akili, kujiamini na mwenye kuweza kufuata malengo yake hata kama mambo mengine yataingilia kati. Mwanamke kama huyu ni ajabu sana hajulikani vilivyo nchini kwake, bali huko ulimwenguni, mwanamke kama huyu alitakiwa kutumiwa vilivyo nchini mwake kwanza kabla ya huko ulimwenguni, bado najiuliza ni kwa nini hajawahi kushika nyadhifa za juu serikalini kama uwaziri na vinginevyo. Nina hakika hata uwezo wa kuingoza nchi anao lakini sijui inakuwaje watu kama hawa wanakuwa hawaonekani. Ninaamini iko siku. Kwa kupata undani wake zaidi kong'oli hapa na hapa

11 November 2005

Ellen Johnson-Sirleaf ....Mwanamke wa shoka.

Naam, Ellen Johnson Sirleaf ameibuka mshindi katika kinyang'anyiro cha kiti cha urais nchini Liberia juma hili. Mwanamama huyu ambaye atakuwa rais wa kwanza mwanamke barani Afrika, alikuwa akichuana na Kijana machachali mwanakandanda wa zamani George Weah. Hongera sana Mama.

01 November 2005

Ugumu wa mwezi mtukufu.

Majuzi nilipata habari hii ya ugumu wa Ramadhani kutoka katika vyanzo vyangu vya habari vilivyoko matawi ya kati. Kwamba kuna huyu mlevi ambaye naye katika mwezi huu hakuwa na namna ya kuukwepa ila kuungana na waumini wengine katika kufunga na kutokugusa pombe kwa mwezi mzima. Jioni moja mlevi huyu alikuwa msikitini akisali, sala yake ilikuwa kama ifuatavyo;

"Ewe Mungu, ifanye Ramadhani kama world cup, ije mara moja katika miaka minne na kila mwaka ije katika nchi nyingine! Amina.

Kwa mtazamo wangu baada ya kuipambanua sala hii ndani nje niligundua kwamba watu wengi sasa hivi hawajui ni kwa nini wanafunga na wanafunga kama sheria na ndio maana huweza hata kuthubutu kuomba ije mara chache, lakini kama wangekuwa wanajua kule kufunga ni kwa manufaa yao wenyewe basi wangeomba hata iongezwe. Hapa nadhani msasa wa haja unahitajika maana kujisahau nako kupo duniani.

Huko Zanzibar Karume kabahatika tena.

Rais Amani Karume wa Tanzania visiwani Zanzibar ameibuka na ushindi wa urais kwa awamu ya pili kwa tiketi ya chama kitukutu cha mapinduzi. Kwa maana hiyo anayo miaka mingine mitano ya kuipeleka tena Zanzibar. Binya hapa upate habari kamili.