Winnie Madikizela Mandela.
Duniani kuna watu machachari, tena kuna watu majasiri na wenye misimamo wanaoweza kudhamiria jambo na kujitoa muhanga kwa lolote hadi jambo lake lifanikiwe.
Winnie Mandela ni miongoni mwa watu wa aina hiyo. Mama huyu ambaye nchini kwake amepewa jina la 'Mama wa Taifa' anajulikana duniani kote kwa jinsi alivyoweza kupigania uhuru wa nchi yake hadi kupatikana hata baada ya mumewe Rolihlahla Nelson Mandela kutiwa garezani kwa miaka 27.
Winnie alizaliwa tarehe 26/09/1936, katika kijiji cha Bizana mkoani Transkei Afrika kusini akiwa ni mtoto wa 4 kati ya 8 wa bwana Columbus Mazingi Madikizela na bibi Gertrude Nomathamsanqa Mzaidume.
Baba yake alikuwa ni mwalimu na baadaye waziri wa kilimo na misitu katika serikali ya Transkei wakati huo ikiongozwa na Kaizer Matanzima. Mama yake alikuwa alikuwa ni mwalimu wa sayansi kimu. Familia yao ilikuwa ni yenye furaha hadi Winnie alipofikisha umri wa miaka saba ambapo mmoja wa dada zake alifariki. Msiba huu ulimsononesha na kumfadhaisha sana mama yake kiasi kwamba mwaka uliofuatia naye alifariki dunia. Akiwa na miaka minane na huzuni ya kuondokewa na mama yake, Winnie alikata shauri kwamba yeye ni lazima atakakuwa mwanamke jasiri.
Maisha mapya yalianza kwa Winnie, na sasa alikuwa karibu zaidi na baba yake. Baba yake alitumia muda mwingi kumfundisha historia ya Afrika kusini na utawala wa kibaguzi uliopo, anasema kila wakati alipokuwa akijisomea vitabu baba yake alikuwa akimuainishia habari za kweli na zisizo za kweli ambazo makaburu walikuwa wakiziandika katika vitabu hivyo. Hivyo basi Winnie katika umri wake mdogo alianza kuelewa kwamba nchi yao ina tatizo ingawa hakujua vizuri ni kwa kiwango gani.
Baada ya muda mfupi alianza shule ya msingi hapo hapo kijijini kwao Bizana na baadaye sekondari ya Shawbury. Akiwa sekondari mwaka 1952 alianza kusikia habari za Mandela na harakati zake, Winnie damu ya ukombozi ikaaanza kumuingia akashawishi wanafunzi wenzie kuanza kutumia kauli alizokuwa akizitumia bwana Mandela katika mikutano yake, inasemekana ilibaki kidogo shule ile ifungiwe.
Winnie alimaliza masomo yake ya sekondari na kubahatika kupata ufadhili wa kuendelea na masomo ya juu katika chuo cha Jan Hofmeyer Johannesburg, chuo hiki kilikuwa mahususi kwa masomo ya Ustawi wa jamii. Alimaliza mwaka 1955 na kupata diploma ya mediko sosho weka (Medical social worker). Baada ya hapo alijiunga na chuo kikuu cha Witwatersrand hapo hapo Johannesburg safari hii akisomea Siasa na uhusiano wa kimataifa.
Alipohitimu chuo kikuu alibahatika kupata kazi katika hospitali ya Baragwanath kama mwana ustawi jamii (social worker). Winnie alikuwa ni mwafrika wa kwanza kwa wanaume na wanawake kufanya kazi ya ustawi wa jamii hospitalini hapo. Na ni kutokana na kufanya kazi hospitalini hapo ndipo alipoamua kwamba atakuwa mwanasiasa. Anasema kulikuwa na tofauti kubwa sana katika utolewaji wa huduma kwa wagonjwa wazungu na wagonjwa waafrika, wagonjwa waafrika hawakupewa kipaumbele hata kidogo jambo hili lilimkera sana Winnie. Akiwa bado mfanyakazi wa hapo hospitalini, alipata zoezi la kufanya utafiti kujua takwimu ya vifo vinavyotokea wakati kina mama wanapojifungua. Matokeo yalikuwa kwamba katika kila wazazi waafrika 1000, kuna vifo 10, na hakuna vifo kwa wazazi weupe na kama vipo basi havikutokana na huduma mbaya na duni aliyopata wakati wakijifungua. Vifo hivi kumi kwa waafrika vilitokana na huduma mbaya walizokuwa wakipatiwa waafrika.
Kwa mara ya kwanza mwaka 1957 Winnie alibahatika kukutana na Nelson Mandela, haijulikani ni wapi hasa walikumbana lakini kwa mujibu wa mwandishi mkongwe na rafiki wa siku nyingi wa familia ya Mandela Profesa Fatma Meer, anasema siku moja alipata simu kutoka kwa Mandela akiwaagiza kwenda stesheni kumchukua mgeni, walipofika walimkuta binti mrembo sana akiwasubiri, wakidhani ni ndugu au jamaa tu wa kawaida wa Mandela walimchukuwa na kumpeleka nyumbani ambako alikaa kwa wiki 2 hivi, hawakujua lolote hadi siku moja Fatma alipomkuta Winnie akitoa na kuangalia picha za Mandela katika mkoba wake ndipo akahisi kwamba kuna jambo linaloendelea kati ya wawili hao.
Mwaka uliofuatia 1958 Winnie alifunga ndoa na Mandela kinyume na matakwa ya Mzee Madikizela. Pingamizi la baba Winnie lilikuwa katika mambo mawili:-
1. Umri- Mandela (40) na Winnie (22) wapi na wapi?
2. Siasa- mandela alikuwa amejikita sana katika siasa, hoja ya Mzee Madikizela
inakuja..saa ngapi ataiangalia familia yake?...hali hii ya kuegemea sana katika
siasa ndiyo iliyofanya ndoa yake ya kwanza na Evelyne Mase Mandela kuvunjika,
kwa hiyo alikuwa na wasiwasi kwamba mwanaye anajiingiza katika matatizo.
Kama nilivyosema hapo awali kwamba Winnie ni kati ya watu wanaoweza kushikilia misimamo yao, basi hata hili la ndoa na Mandela hakuruhusu mtu aligeuze, alikubaliana kabisa na hoja za baba yake na hata alipoolewa alijua kabisa anaolewa na mtu wa aina gani. Muda mfupi baada ya kuoana Winnie alijiunga rasmi na chama cha African National Congress (ANC), na bila kuchelewa akaanza kupiga kampeni ya kuipinga serikali ya kikaburu, mwaka huohuo alikamatwa na kuwekwa jela kwa siku 14 akiwa mjamzito, hii ilikuwa ni mara yake ya kwanza kutumikia kifungo.
Mwaka 1959 walibahatika kupata mtoto wa kwanza wa kike waliyemwita Zenani, na mwaka uliofuatia 1960 walipata mtoto wa pili pia wa kike waliyemwita Zindzi. Mwaka huo huo 1960, chama chao cha ANC kilifutiwa kibali chake na kupigwa marufuku kufanya shughuli zozote za kisiasa. Waliendelea kukiendesha kwa siri na kama haitoshi Mandela akaamua kufunga safari kwenda katika nchi mbalimbali za kiafrika kuwaomba waungane naye katika mapambano ya kutokomeza serikali ya kibaguzi ya Afrika kusini. Bahati mbaya serikali tawala ililigundua hilo na Mandela aliporudi alishtakiwa na kutiwa ndani hiyo ilikuwa mwaka 1962, Mandela akiwa jela huku nyuma Winnie akapatikana na tuhuma za kuendelea kukiendesha chama cha ANC kinyume cha sheria, adhabu yake ilikuwa ni kuwekwa kizuizini katika mji wa Soweto. Mwaka 1964 mandela akapatika na hatia ya kutaka kuipindua serikali ya kikaburu na akahukumiwa kifungo cha maisha jela.
Makaburu wakidhani kwa hukumu hiyo watakuwa wamezimisha harakati za ukombozi za chama cha ANC, lakini kwa Winnie ndiyo kwanza mapambano yalikuwa yanaanza, cha kwanza alichokifanya ni kuwahamishia watoto wake nchini Swaziland kwa mmoja wa dada zake ili kuepuka usumbufu. Mwaka 1967 akiwa bado kizuizini aliamua kwenda kumtembelea Mandela gerezani Robben Island aliporudi akashtakiwa na kufungwa kwa mwaka mmoja. Alipomaliza muda wake wa gerezani alitoka na kuendelea kukaa kizuizini huku akiwa amezuiliwa kujihusisha na shughuli zozote za siasa.
Sifa au tuseme tabia moja kubwa aliyonayo Winnie ni ukaidi na kutokuogopa lolote, ingawa mwaka mzima wa 1968 aliumalizia gerezani, lakini alipotoka aliendelea na shughuli za ANC na hata kutembelea maeneo aliyokatazwa kufika. Kutokana na hili mwaka 1970 alikamatwa na kutiwa gerezani kwa miezi 9, alipomaliza alitoka lakini akiwa ameongezewa miaka 5 zaidi ya kukaa kizuizini. Mwaka 1974 muda mfupi kabla ya kifungo chake cha nje kuisha alikaidi tena na kuamua kukutana na mwanaharakati mwingine ambaye pia alikuwa kizuizini, kwa hili akahukumiwa tena kwenda gerezani.
Hatimaye baada ya miaka 13 ya kuwekwa kizuizini na gerezani Winnie aliachiwa huru,
lakini mwaka 1976 baada ya machafuko ya Soweto Winnie alifungwa tena kwa miezi 3 na alipotolewa aliwekwa tena kizuizini kwa miaka 8 safari hii akiwa chini ya ulinzi mkali wa polisi.
Miaka ya themanini ilianza, kwa Winnie hii ni miaka ambayo hawezi kuisahau kwa ulahisi kwani ilikuwa ni miaka ya mvurugiko wa maisha yake binafsi, mwaka 1982 mumewe alihamishwa gereza kutoka Robben island kwenda Pollsmoor karibu na Cape Town, mwaka 1985 nyumba yake ya Brandfort ililipuliwa kwa bomu na hivyo kumfanya kuhamia Soweto ili kuepuka vitendo vya kiugaidi. Kwa kipindi chote hiki Winnie alikuwa akiheshimika sana duniani kote kama mwanamke shujaa na jasiri.
Mtizamo huu wa watu juu yake ulianza kubadilika mwishoni mwa miaka ya themanini, ambapo aliamua kuunda timu ya mpira wa miguu ya Mandela (Mandela United Football Team) wachezaji wote wa timu hii walikuwa ni walinzi wake (bodyguards), kwa bahati mbaya timu hii kiutawala ilisahau wajibu wake na kuegemea upande mmoja wa kumlinda na kumzibaziba Winnie katika mambo ya chini chini aliyokuwa akiyafanya. Muda mrefu haukupita habari zikaanza kuvuma kwamba timu inajihusisha na ubadhilifu wa mali ya umma. Timu nayo ikashtuka na kujizatiti zaidi kwa kufukuza na hata kuua mtu yeyote aliyetaka kwenda kinyume nao. Inasemekana vijana wengi walifukuzwa na kuuawa kwa kuchinjwa kama mbuzi au kwa mtindo wa Necklacing, Soma hapa juu ya Necklace, lakini baya zaidi na pengine linalomsumbua Winnie hadi sasa hivi ni lile la kumuua kijana mdogo wa miaka 14 Stompie Seipei mwaka 1989 kwani hili halikuweza kufichika. Stompie Seipei alikuwa ni mmoja wa vijana katika timu ya Mandela, na kutokana na sababu zisizojulikana ilivuma habari kwamba Stompie alijiunga na timu akiwa ni mpelelezi kutoka polisi. Stompie na vijana wengine watatu walikamatwa walipokuwa kanisani na kupelekwa katika nyumba ya Winnie, huko waliteswa sana na baadaye kuchinjwa kama mbuzi. Shughuli ya uchinjaji ilikuwa ikifanywa na kocha wa timu wakati huo bwana Jerry Richardson ambaye sasa hivi anatumikia kifungo cha maisha. Kwa habari zaidi ya jinsi mauaji na mateso yalivyokuwa yakitendeka soma hapa na hapa ambapo bwana Richardson alieleza ukweli wote. Na kwa tukio hili Tume ya usuluhishi (Truth and Reconciliation commission) iliingilia kati na kuanza kuichunguza timu ile kwa undani zaidi, tume iligundua mauaji mengi yaliyofanyika katika timu hiyo, bonyeza hapa ujionee mwenyewe.
Mwaka 1990 Nelson Mandela aliachiwa huru, mke na mume waliungana bila matatizo hata baada ya Mandela kusikia tuhuma zote za mauaji ya timu ya mpira ya Mandela. Alimuamini mkewe na kumtetea kwa nguvu zake zote. Tatizo lilikuja baada ya Mandela kupata habari kwamba mkewe alikuwa na mahusiano ya kimapenzi na Kijana Dali Mpofu ambaye alikuwa ni mwanasheria binafsi wa Winnie, hapa mzee Madiba alishindwa kumtetea na hata kumsamehe, Mandela na Winnie wakaachana kwa usalama kabisa mwaka 1996 baada ya ndoa yao kudumu kwa miaka 38, kwa habari zaidi ya kuachana kwa Winnie na Mandela soma hapa.
Hilo la ndoa likawa limekwisha, lakini kesi yake ya mauaji iliendelea na ushahidi wote ulionyesha kwamba Winnie ana hatia ya mauaji lakini bado Winnie hakukubali kukiri. Ni askofu Desmond Tutu ndiye aliyefanikiwa kumshawishi akubali makosa yake na kuyakiri hadharani ili kurudisha heshima yake 'alimwambia watu hufanya makosa..na unapokubali na kukiri kosa mara nyingi heshima yako huongezeka'. Winnie kwa kuzingatia hili aliomba msamaha na hata kukumbatiana na mama mzazi wa Stompie Seipei 'Mrs Joyce Seipei. Hebu soma hapa uone jitihada za askofu Desmond Tutu zilivyokuwa.
Tangu kipindi hicho hadi sasa siri nyingi za Winnie zimekuwa zikiendelea kutoka ikiwa ni pamoja na ya wizi wa fedha benki kwa kutumia za kugushi makaratasi yasiyo halali. Soma hapa ulipate na hilo. Lakini pamoja na hayo yote bado Winnie alikumbukwa katika serikali ya Mandela kwa kupewa nafasi ya uwaziri wa utamaduni, ubunge na hata Urais wa African National Congress Women League (ANCWL). Mwaka 2003 Winnie alijiuzuru nyadhifa zake ANC na kuanza kutumikia kifungo cha miaka 5 kwa makosa aliyoyafanya. Soma hapa kwa habari zaidi.
Ndugu wasomaji, labda kwa ufupi ningesema kwamba Winnie Nomzamo Nkosikazi Madikizela Mandela, hajawahi kuishi maisha ya kawaida ambayo mimi na wewe tumeweza kuishi, na kwa kumwangalia tangu alivyoanza mapambano mpaka anavyomaliza mapambano nimeshindwa kabisa nimuweke katika fungu gani maana mazuri kayafanya na mabaya kayafanya. Jamani hebu na nyiye nisaidieni huyu mama.