17 July 2005

...labda Yesu amepotea...!!!!

Majuzi, mwanangu Shija,(mtoto wa dada yangu)mwenye umri wa miaka tisa aliniacha hoi, ilikuwa ni jioni, mvua kubwa iliyoambatana na radi kali za mwanga na kuunguruma ilikuwa ikinyesha. Shija alikuwa kimya akiangalia dirishani, nilidhani kwamba anaangalia jinsi mvua inavyonyesha kumbe alikuwa na fikra zake, akaamua kutoa duku duku lake...

Shija: (akiniita) Mam'dogo Mija....

Mija: Unasemaje?

Shija: Labda Yesu amepotea mbinguni...

Mija: (Kwa mshtuko na ka mshangao kidogo) Hee! kwa nini unafikiri hivyo??

Shija: Kwa ajili ya hizi zinazopiga (radi)...Labda yesu amepotea sasa wanamtafuta...

Mwanangu huyu aliniacha mdomo wazi, nikabaki daa! huku nikifikiria nianzie wapi kumpa somo. Lakini pia nilijifunza kwamba si kila mtu huwa na fikra moja juu ya jambo fulani ambalo liko wazi na linalojieleza. Na vile vile niligungua kwamba kama unataka kupata mtazamo mpya juu ya jambo fulani, basi waulize watoto kwani wenyewe husema hasa lile wanalolifikiria kuwa ndilo, lakini watu wazima mara nyingi husema yale ambayo wanadhani watu watafurahi kuyasikia, hata sijui ni kwanini watu wazima tuko hivi?? Hili jambo nitalizungumzia hivi karibuni...ngoja nikikimbilie kitanda.

07 July 2005

KUMZOEA MUNGU.

Sijui kama na wenzangu mmeliona hili. Mimi huliita kumzoea Mungu, suala hili ni kwa wakristo waliookoka, nimekuja kugundua kwamba walokole walio wengi humuogopa Mungu katika siku za awali za wokovu wao, lakini kadiri siku zinavyoendelea watu hawa hujisahau na huanza kumzoea Mungu kwa kurudia matendo yao ya zamani lakini wakiwa chini ya kivuli cha wokovu kwa maana ya kusali sana lakini bila kuwa makini kwamba matendo nayo yalitakiwa yabadilike.

Nina vielelezo vingi ambavyo vimekuwa vikinitatanisha, mfano mmojawapo ni ukosefu wa upendo wa dhati na kujaa kwa dharau kwa walokole dhidi ya wale wasiookoka. Binafsi naunga mkono kabisa suala zima la wokovu, lakini vile vijitabia vya walokole nasema vinahitaji kukemewa kwa jina la Yesu, utakuta familia hizi zina wakataza watoto wao kufanya urafiki na watoto wa imani zingine kwa kusema kwamba wataharibika tabia, na si kwa watoto wao tu, bali hata wao wenyewe utakuta urafiki wao ni wa wenyewe kwa wenyewe, hata kutembeleana ni kwa wao kwa wao, ukiuliza utaambiwa wale ni watu wa mataifa, kweli sikatai ni watu wa mataifa lakini je? tunategemea watu hawa wa mataifa watayaachaje mataifa hayo bila ya kujichanganya nao na kupata kujua wokovu ni kitu gani? Yesu mwenyewe enzi zake hakushughulika kabisa na wale waliokwisha kuwa wake, kila siku alijichanganya na wale wa vijiweni ili nao wapate kumjua na ndio sababu alisema 'wenye afya hawahitaji daktari bali wagonjwa' hii ni baada ya walokole wa enzi hizo pia kumshangaa kwamba ni kwa nini anajichanganya na vibaka na walevi na wazinzi.....mlokole wa sasa hivi aunde urafiki na mzinzi ....dhubutuu!! hawajui tu hiyo ni dhambi tosha ya kumbagua badala ya kumsogeza karibu ili na yeye abadilishe tabia.

Tabia nyingine ya kumzoea Mungu ni kwa waumini hawa kugeuza makanisa uwanja wa maonyesho ya mavazi, simaanishi kwamba kanisani usipendeze la hasha! pendeza lakini usifikie hatua kwamba huendi kusali eti kwa sababu sina nguo nzuri ya kuvaa, kina fulani watanicheka...na ni kweli kuna walokole ambao kazi yao ni kuangalia fulani kavaa nini leo.... fulani hajui kuvaa, jamani huku kama si kumzoea Mungu ni nini? haogopwi tena, watu wanafanya yale wanayojisikia kufanya, alimradi kivuli cha wokovu kiko mbele yao.

Utakuta mchungaji haamini kama watu wengine wasiookoka wanajua kusalisha, kipindi fulani mchungaji fulani alikuja nyumbani kwetu kututembelea, saa ya chakula ikafika tukamwambia mmoja wetu asalishe kabla ya kula, mchungaji akadakiza kwani na nyie mnajua kusali!! tulibaki na butwaa... kwamba kumbe hata kusali kuna utaalamu wake??

Ni mengi mno niliyoyaona kama kugombea madaraka, vinyongo, uzinzi baada ya mazoezi ya kwaya...Mungu alisema wa kwanza atakuwa wa mwisho na wa mwisho wa kwanza, tujiangalie sana. Ni lazima tujifunze kuishi kwa kujitathmini, kila siku kabla ya kulala ni vizuri ukajiuliza matendo niliyoyafanya leo yamemsaidia yeyote kubadili tabia yake kuwa nzuri au la? binafsi nina tabia ya kujiuliza kwamba..hiki kitu ninachokifanya angekuwa Yesu angefanya? jibu nilipatalo ndo hunifanya niendelee au niache kufanya jambo nilifanyalo.

Hivyo basi kila mara tujue Shetani yuko nasi na hasa ukiokoka, hivyo tuwe makini sana.