23 June 2005

Malengo katika maisha.

Mafanikio yoyote yale ya binadamu huletwa na malengo thabiti yanayoambatana na ufuatiliaji wa kina. Kuwa na malengo katika maisha yetu ni jambo la muhimu sana kwani malengo ndo humfikisha mtu pale alipodhamiria kufika. Ninaamini kila mtu ana malengo yake katika maisha, lakini watu wachache tu ndo huyatimiza malengo yao. Nimekuwa nikijiuliza ni kwa nini watu wengi hawayafikii malengo yao, na nimekuja pata jibu kwamba watu hushindwa kuyafuatilia malengo malengo yao, ni rahisi sana kupanga jambo lakini ni ngumu sana kulifanya hilojambo litokee, hii ni kwa sababu ya kutokutaka kusumbuka wala kutumia muda mwingi katika jambo fulani. Hivi ndivyo tulio wengi tunavyoishi.

Leo nitaongelea jinsi ya kufuatilia malengo ili kuyafikia malengo.
Kwanza kabisa ni kujua jinsi ya kuutumia muda wako wa siku nzima, tangu unapoamka hadi utakapolala, panga ratiba nzuri na usiruhusu vitu visivyo na maana kukuingilia katikati, mfano tuseme leo umepanga utapalilia bustani yako yote, basi badala ya kufanya hivyo mara moja wewe utashika jembe utalima kidogo, utasema ngoja nikanywe maji ndani ukiingia ndani unakuta kakipindi kazuri kwenye luninga, unasema ngoja nitizame kidogo hako kanakugharimu dakika kumi, unapotaka kurudi bustanini unaona ngoja umpigie simu shoga yako kumweleza uliyoyaona kwenye luninga, hiyo inachukua robo saa maana zinazuka na stori zingine za nani kafanya nini na mambo mengine meeengi, ukija kutahamaki ni saa saba mchana labda unatakiwa uandae chakula kwa wanao na mambo mengine, hapo upaliliaji inabidi usitishwe hadi kesho bila sababu yoyote ya maana, ule muda wa kesho ambao ungeutumia kwa mambo mengine unajikuta unautumia kutimiza mambo ya jana yake na si ajabu siku hiyo tena ikapita bila kufanya lolote na kujikuta unamaliza wiki nzima bila kufanya lolote la msingi. Mambo haya madogo madogo ndio hutufanya tushindwe kufikia malengo yetu makubwa ya maisha yetu.
Kuwa na malengo katika maisha haikusaidii tu kufanikiwa katika maisha yako bali pia kuepuka mikumbo. Mara nyingi watu wengi hujikuta katika kundi la kufuata mkumbo kutokana na kushindwa kujiwekea malengo binafsi ya yeye kama yeye, utakuta mtu anafanya jambo fulani kutokana na kumuona mtu fulani anafanya jambo hilo kwa mafanikio, kwa mfano hili suala la sanaa ya muziki kwa vijana, utashangaa siku hizi kila mtoto anasema anataka kama Juma Necha au Jeidii, ukimuuliza kwa nini atasema kwa vile anaimba vizuri na amekuwa maarufu , jamani tuelewe kila mtu ameumbwa kwa ajili ya kutimiza jambo fulani hapa duniani, Juma necha amekuwa Juma Necha kwa sababu alikaa akatafakari yeye binafsi anataka nini, anaweza nini na je anayapenda hayo anayoyataka nakuyaweza? alipopata jibu ndio, hapo akaanza utekelezaji na hii ndio sababu kubwa ya mafanikio yake...'kufanya jambo analolisikia rohoni ni lake'.

Hivyo ndugu zangu tuanze kujirekebisha sasa kwa kuanza kusikiliza nafsi zetu zinasema nini, halafu kuweka malengo kwa hayo tunayoyapata katika nafsi zetu na lamuhimu zaidi ni kufuatilia utekelezaji ili kuyatimiza malengo hayo. Kama tukifanya hivi wengi wetu tutafika mbali na vipaji vingi vitaibuka.

06 June 2005

Maria Mutola mwanariadha kutoka msumbiji anayetingisha dunia.

Katika harakati zangu za kuwasakanya wanawake wa shoka, nimebahatika kukumbana na huyu dada Maria Mutola. Dada huyu ambaye ni mwanariadha tishio ulimwenguni alizaliwa katika kitongoji cha chamanculo jijini Maputo tarehe 27, mwezi wa kumi mwaka 1972.

Maria ambaye alizaliwa kuwa mwanamichezo, utotoni mwake alikuwa akilisakata kabumbu kama hana akili nzuri vile. Alikuwa akicheza katika timu za mitaani hadi alipofikia umri wa miaka 14 pale bahati yake ilipomwangukia. Ilikuwa siku moja mwandishi mmoja maarufu wa mashairi nchini humo bwana Jose Craveirinha katika pitapita yake akakutana na Maria ndani ya fani alikuwa akilisakata soka sambamba na wanaume, Craveirinha hakuamini macho yake, ikabidi asimame kwanza ajihakikishie huku akijiuliza...jamani ni macho yangu au, huyu ni mwanaume au mwanamke?? lakini baada ya kuchunguza vizuri akabaini kuwa ni msichana, Pale pale Craveinrinha akagundua uwezekano wa Maria kuwa mwanariadha bora kama angepata mafunzo. Bwana huyu akadhamiria kuongea naye kwa nia ya kumsaidia, walipoongea Maria akasema kama ningebahatika kupata mafunzo na muda wa kutosha wa kufanya mazoezi angeweza siku moja kuitangaza nchi yake duniani.

Bwana huyu baada ya hapo akaona kuna umuhimu wa kumsaidia Maria, akamtafutia shule pamoja na udhamini nchini Marekani kwa mafunzo zaidi ya uanariadha mwaka 1986, nikuanzia hapo ndipo alipoanza kuonyesha mavituz yake, mwaka 1988 aliingia mashindano ya olimpiki Seoul, ambapo hapa hakufanya vizuri sana, 1992 Barcelona nafasi ya 5, 1996 Atlanta akaondoka na medali ya bronze, 2000 Sedney ndio akawamaliza kabisaa akaondoka na medali ya dhahabu. Hadi leo hii Maria Mutola anaheshima kubwa duniani na nchini kwake, mwaka 2003 aliteuliwa kuwa Balozi wa umoja wa mataifa kwa vijana. Kwa kumjua zaidi mtizame hapa akiwa na vijana wake wa kazi.

01 June 2005

Kujitambua nguzo ya ukombozi wa mwanamke.

Mara nyingi nimekuwa nikijiuliza, hivi ni kwanini watu wengine wanafanikiwa maishani mwao na wengine hawafanikiwi, zamani nilikuwa nafikiri kwamba Mungu huandikia watu hivyo, kwamba huyu ni wa kukosa na huyu ni wakupata, dhana ambayo haina ukweli wowote. Ukweli ni kwamba kupata au kukosa kwa mtu kunatokana na yeye mwenyewe kwa ufupi ni mtu mwenyewe ndiye anayechagua apate au akose, najua utajiuliza ni kwa vipi mtu achague kukosa? basi mtu huyo kidogo zitakuwa zimeruka....laa hasha!! utakuta mtu mzima na akili zake lakini ndio kachagua kukosa. Kwa vipi basi?? ....Kwa kutojitambua.

Kujitambua ni nguzo kubwa, muhimu na ya kwanza katika maisha ya binadamu. Sina hakika kama wengi wetu hujiuliza, je mimi ni nani?, ninapenda na sipendi nini?, ninaweza na siwezi nini?, nina malengo gani katika maisha yangu, nina wajibu gani katika maisha yangu kwa watu wengine n.k. Maswali haya au mambo haya ndio humuamulia mtu kuwa wa namna gani, au wa tabia gani, kwani mwelekeo wa maisha ya mtu hutokana na yeye anawaza nini hasi au chanya.

Tukirudi katika suala la wanawake kwa nini bado tunapiga danadana pale pale, sababu kubwa ni hii ya kutojitambua wenyewe, tunaiachia jamii ituambie sisi ni kina nani, tunaweza nini, hatuwezi nini, tunapenda nini hatupendi nini, wajibu wetu ni upi na upi si wajibu wetu na mengine meeengi, tumekingwa na wingu la giza na sisi tukalikubali, kitu muhimu kina mama tunatakiwa tukitambue ni kwamba hakuna mtu anayeweza kumtambua mtu mwingine zaidi ya yeye mwenyewe anavyojitambua, wewe ndio unajua unawaza nini sasa hivi, unaumwa au huumwi, unasikia njaa au husikii. Hivyo tuache kabisa tabia ya kusubiri kuambiwa wewe sasa hivi unasikia njaa...kula, au wewe unaumwa kunywa... dawa.

TUJITAMBUE JAMANI NA MATOKEO YAKE TUTAYAONA.