25 June 2006

Yupi anayepaswa kutolewa bungeni?... anayesinzia kikaoni au aliyevalia??


Hapo majuzi nadhani wote tuliipata hii habari ya mbunge Amina Chifupa kutolewa katika kikao cha bunge kutokana na kofia aliyokuwa amevaa ambayo haikuendana na kifungu kimojawapo cha sheria ya bunge, hivi vifungu vya sheria bado vinanichanganya ina maana kuna vifungu vya sheria vinavyoruhusu kusinzia wakati kikao kikiendelea? nauliza hivi kwa sababu sijawahi kuona mbunge akitolewa kikaoni kwa sababu anasinzia ingawa nusu yao huwa wanasinzia. Hivi ni hadi lini watanzania tutakuwa tukiendelea kukemea mambo mepesi mepesi na kumezea mazito?

Haya habari ya Chifupa hiyo hapo chini kama hukubahatika kuisoma.


Mbunge wa CCM wa Viti Maalum, Mheshimiwa Amina Chifupa leo asubuhi amejikuta akitolewa nje ya ukumbi wa Bunge wakati kikao kikiendelea.

Zali lenyewe lilianza hivi:
Kikao kilianza asubuhi kama kawaida, waheshimiwa wakaingia ndani ya ukumbi na kila mmoja kuketi kwenye siti yake.

Dua iliporomoshwa ya kuliombea Bunge na Taifa, kama kawaida na baadaye kipindi cha maswali na majibu kikaanza.

Hata hivyo ilipotimu kama saa 3:22 hivi, Spika wa Bunge, Mheshimiwa Samwel Sitta akasema, ’’ Kabla ya kuendelea namuomba Mheshimiwa Amina Chifupa atoke nje akavue kofia yake,’’.

Baada ya sentesi hiyo, Spika alinyamaza kidogo halafu akaendelea, ’’Ni kwa mujibu wa kanuni za Bunge...Mheshimiwa, unaweza kuvua halafu ukarejea tena...siyo moja kwa moja’’.

Mheshimiwa Amina Chifupa alikuwa amevalia kofia ya pama nyeusi inayomechi na nguo zake.

Baada ya tangazo hilo la Spika, Mheshimiwa Amina Chifupa, alisimama na kutoka nje ya ukumbi.

Hata hivyo Spika amefafanua kuwa suti ya Ulaya ikiwa imekamilika ni ruksa kutinga nayo Bungeni.

Akasema kanuni ya 74 kifungu cha tatu ndiyo inayozungumzia mavazi ya kike Bungeni.

Hata hivyo wakati tunakwenda mitamboni mheshimiwa Chifupa alikuwa tayari amerejea ukumbini akiwa hana kofia hiyo.