16 March 2007

Miriam Makeba

Miriam Makeba ni mwanamuziki mashuhuri sana na mwanaharakati kutoka Afrika kusini. Alizaliwa 04-03-1932 Johannesburg. Baba yake Caswell Mpambane Makeba alikuwa ni kabila la xhosa na Mama yake Christina Nomkomendelo Jele alikuwa ni mswazi.

Miriam ni mtoto wa sita na wa mwisho kwa mama yake, na wa kwanza na wa mwisho kwa baba yake. Mama yake aliolewa na Makeba baada ya ndoa yake ya kwanza na bwana Mahlangu kuvunjika wakiwa tayari na watoto watano ambao ni, Joseph, Hilda, Mizpah, Ethel na mmoja aliyefariki akiwa mchanga.

Familia yao ilikuwa ni masikini sana. Baba yake ambaye alikuwa ni mwalimu kitaaluma hakuwa na kazi yoyote, kwani katika kipindi hicho cha utawala wa kikaburu ilikuwa ni ngumu sana kwa mwalimu mwafrika kupata shule ya kufundisha. Mama yake alikuwa anafanya kazi za ndani kwa wazungu na wakati mwingine kuuza pombe ya kienyeji(umqombothi) ili kuihudumia familia. Wakati huo ilikuwa ni kinyume cha sheria kwa mwafrika kunywa au kutengeneza pombe ya aina yoyote ile lakini hata hivyo ilikuwa ikitengenezwa na kunywewa kwa kificho. Kutokana na hali hiyo polisi wa kizungu walikuwa wakivamia mara kwa mara makazi ya waafrika ili kuwakamata wasiotii amri hiyo ya kunywa na kutengeneza pombe. Ilikuwa ni pale Miriam alipofikisha umri wa siku 18 tu tangu azaliwe, polisi walivamia maeneo ya waafrika na kufanikiwa kumkamata mama Miriam akiuza pombe, bila huruma wala kujali kwamba ana mtoto mchanga walimbeba hadi mahakamani na kuhukumiwa adhabu ya kifungo cha miezi sita jela. Hakuwa na jinsi ya kumuacha Miriam, alimbeba Miriamu wake na kwa pamoja kukaa jela kwa miezi sita. Hivyo basi Miriam akiwa katika umri mdogo kabisa aliweza kuionja jela.

Walipotoka Jela walikuta baba (Makeba) amepata kazi katika kituo cha kuuza mafuta cha Shell, hivyo maisha yao yakawa na nafuu. Maisha yaliendelea vizuri hadi mwaka 1938 ambapo Mzee Makeba alifariki dunia, Miriam akiwa na umri wa miaka 6. Taabu ikarudi palepale, na kwa vile kipato cha mama yao hakikuweza kutimiza mahitaji ya watoto wote sita, ikabidi ahamishie watoto wake kijijini kwa bibi yao aliyeitwa MaVilakazi, (huyu ni mama mzazi wa mama yake na Miriam). Na yeye akabaki mjini kwa ajili ya kazi. Miriam anasema kuanzia hapo ilikuwa si rahisi kuonana na mama yake, muda mwingi alikuwa kazini mjini na kwa vile Miriam alikuwa bado ni mdogo na anayehitaji uwepo wa mama yake zaidi, ilibidi awe anafunga safari ya mjini kila mwisho wa juma baada ya masomo kwenda kumuona mama yake aliyekuwa akikaa kwa wazungu aliokuwa akiwafanyia kazi.



Upande wa pili kwa bibi MaVilakazi, familia ilikuwa ni kubwa ya wajukuu 21,(watoto wengine ni wa kaka na dada za mama yake na Miriam). na yenye kipato kidogo, siku nyingine walikula na siku nyingine walilala njaa, lakini maisha yalikuwa yakienda. Miriam anasema kwamba pamoja na hali ile duni pale kwa bibi yake, bibi yake hakuwa na mzaha kabisa na kanisani, kila jumapili ni lazima kwenda kusali utake usitake. Miriam hakupenda sana kutokana na vile bibi yao alivyokuwa akitunza hela na vitu vingi vizuri kwa ajili ya kutoa sadaka wakati nyumbani wanalala na njaa. Wakati mwingine Padri wao aliwapita njiani wakati wa mvua wakinyeshewa bila kutoa hata lifti kwa gari ambalo limenunuliwa kwa sadaka zao. Miriam anasema kitu kimoja kilichomfanya asiache kwenda kanisani kilikuwa ni uimbaji tu, alipenda sana kuimba, na kanisani waliimba sana. Baada ya miaka kupita, mama yake alianza kuchoka na kuugua ugua, lakini alishindwa kuacha kazi kwa vile alikuwa akimsomesha Miriam ambaye ndio alikuwa ameanza chuo, Miriam naye alikuwa amechoka na maisha duni waliyokuwa wakiishi, maisha ya kuvaa 'kauka nikuvae' hali hii pamoja na kuona mama yake akiugua kila mara ikamfanya kufikia uamuzi wa kuacha shule na kutafuta kazi. Alipata kazi yake ya kwanza ya kuangalia mtoto katika familia ya kigiriki, alihamia pale na ulipofika mwisho wa mwezi wa kwanza alilipwa mshahara wake vizuri, mwezi uliofuatia akaambiwa asubiri kidogo kwa vile mwajiri wake alikuwa na matatizo kidogo, mwezi wa tatu mke wa mwajiri wake akamsingizia ameiba vitu ndani kwa hiyo hakuna mshahara. Miriam akaona huu ni uendawazimu, akaamua kuacha kazi. Akapata kazi nyingine kwa wazungu hii nayo ni ya kuangalia mtoto, anasema mambo yalienda vizuri hadi siku moja wakati wa likizo ambapo walisafiri, wakiwa huko wakafikia hoteli ya ufukweni. Hivyo wakati wa jua wao walikuwa wakijianika mchangani na Miriam akapewa kazi ya kukusanya shells kwa ajili ya kazi za sanaa za yule mzungu alizokuwa akizifanya. Siku ya kuondoka ilipofika bila sababu maalumu Miriam akaambiwa apande treni arudi, na wao wakarudi na gari walilojia. Katika ukusanyaji wake zile sheli aliweza kujaza ndoo mbili, hizi nazo aliambiwa arudi nazo kwa treni. Kwa hiyo yeye, mabegi yake na ndoo mbili zilizojaa shells tena katika daraja la tatu la treni!! hakuwa na la kufanya akapanda na kuanza safari ya kurudi, wakiwa njiani wakaambiwa inabidi wabadili treni wakatelemka na kusubiri nyingine. Ilipokuja akaanza kupandisha begi lake la nguo, akachukua ndoo ya kwanza ya shells, alipotaka kuchukua ya pili treni ikaanza kuondoka, haraka haraka akarukia ndani ya treni bila ndoo ya pili. Akaitizama ile ndoo iliyobakia akasema 'katu siiachi hii treni kwa ajili ya hiyo ndoo ya shells, sina hela nyingine ya nauli na hii treni ikiniacha ndiyo itakuwa mbaya zaidi'. Treni ikazidi kukaza mwendo na yeye akazidi kuitizama ile ndoo inavyobakia. Kufika Johannesburg alikuwa akitetemeka kwa hofu, alijiuliza atamwambia nini mwajiri wake kuhusu ndoo ya pili? baada ya kufikiri akaamua hatorudi tena kazini, hivyo akaachana na kazi ile nakuamua kurudi nyumbani.




Huku nyumbani hali ya mama yake ilizidi kuwa mbaya, miguu yake ilianza kuvimba hadi kushindwa kutembea, walimpeleka karibu kila hospitali bila mafanikio. Hivyo wakaamua kumpeleka kwa mganga wa kienyeji 'isangoma', kule wakaambiwa kwamba kuumwa kwake si bure, mizimu ya kwao imemchagua awe mganga wa kienyeji 'isangoma' ili aweze kuwasiliana nao moja kwa moja na kuwaeleza watu mambo yaliyopita, kutabiri yajayo na pia kutibu wengine. Na kama anataka kupona maradhi yanayomsumbua ni lazima akubaliane na hilo, wote walifurahi na kukubali kwani wanasema kuchaguliwa na mizimu ilikuwa ni kama zawadi. Baada ya kukubali alitakiwa kufuata mchakato wa Ukutwasa. Ukutwasa ni mchakato au hatua za kumfanya mtu kupokea nguvu za mizimu hadi kuweza kuponya wengine (Mganga). Aliondoka na kwenda Swaziland ambako ukutwasa wake ulikuwa unafanyikia. Kutokuwepo kwa mama yake nyumbani kulimfanya yeye kuchukua majukumu ya mama yake, kama kuilisha na kuiangalia familia kwa ujumla. Kwa jukumu hili ilibidi atafute kazi tena na safari hii akaamua kuwa dobi. Wakati huo kulikuwa na wafanyakazi wengi wageni waliokuwa wakifanya kazi nchini, na hao ndio walikuwa wateja wake, kila jumatatu alikwenda kukusanya nguo zao chafu na ijumaa kuwarudishia safi. Haya ndiyo yakawa maisha ya Miriam.




Tangu akiwa shule hadi kipindi hiki anachofanya kazi za udobi, Miriam alikuwa na mpenzi wake chotara aliyeitwa James Kubayi au Gooli kama alivyojulikana kwa marafiki zake. Urafiki wao ulikuwa mzuri sana na kila mara walikuwa wote, Gooli alikuwa pamoja naye alipoacha shule, alipopata kazi kwa wazungu na hata sasa wakati mama yake alipokuwa Swaziland. Miriam alimpenda na kumuamini sana kiasi kwamba haukupita muda akapata ujauzito, hapo akiwa na umri wa miaka 17 tu. Anasema alikuwa na bahati sana kwani Gooli hakumtelekeza, alimchukua kumuhamishia nyumbani kwao. Familia ya kina Gooli ilikuwa inajiweza kidogo, mama yake alikuwa akipika pombe kama biashara ya ziada. Akiwa katika familia ya wakwe na mimba mambo yalikuwa magumu kidogo kwani Gooli hakuwepo muda mwingi alikuwa anachukua mafunzo ya upolisi katika mji mwingine hivyo alikuja pale kusalimia tu. Muda wa kujifungua ulipofika alipelekwa hospitali na kujifungua mtoto wa kike aliyemwita Sibongile au kwa kifupi Bongi. Alipotoka hospitali maisha hayakuwa rahisi tena, kazi zote za pale kwa mkwewe alitakiwa azifanye yeye, alikuwa akiamka saa 10 alfajiri kumuosha na kumlisha Bongi, kupika chakula cha wengine na kufanya shughuli zote za ndani na bado Bongi akilala alibaki kuhudumia wateja wa pombe hadi usiku wa manane.




Gooli alimaliza mafunzo yake na kurudi nyumbani, lakini alikuwa amebadilika sana tabia, alikuwa mkorofi na mwenye wivu wa kupindukia, alianza tabia ya kumpiga Miriam bila sababu za msingi, Miriam hakuwa na haki ya kusema lolote kwa Gooli, Miriam alianza kusononeka lakini alivumilia, alijua Gooli hampendi tena lakini hakujua ni kwa kiasi gani hadi siku moja alipomfumania na ndugu yake. Miriam alijua amemfumania mumewe kwa hiyo hapo ana nguvu ya kusema lakini badala yake kibano kilimgeukia yeye na kupigwa kipigo cha kifo. Kuanzia hapo alisema imetosha, alimchukua mtoto wake akakodi taksi na kurudi nyumbani kwao bila kuaga. Gooli alimfuata kumrudisha lakini alikuta mama yake amesharudi toka Swazilandi, alimkurupua vibaya sana na toka siku hiyo hakurudi tena na ndiyo ukawa mwisho wa Miriamu na baba mtoto wake kuonana.




Miriam sasa akiishi kwa mama yake, hakuwa na kazi yoyote ya kipato zaidi ya kumsaidia mama yake shughuli za Usangoma. Mama yake akaona hali hii haitamfikisha mahali popote mwanae, akamwambia ni lazima abadilishe kabisa mwelekeo wa maisha yake kwa kutafuta kitu cha kufanya. Miriam akaona ni bora aende mjini akaangalie cha kufanya, akamuacha Bongi na mama yake yeye akaenda mjini Johannesburg.





Johannesburg alifikia kwa binamu yake aliyeitwa Sonti Ngwenya, Sonti alikuwa na mwanaye wa kiume aliyeitwa Zweli ambaye walikuwa karibu rika moja na Miriam. Zweli na baadhi ya marafiki zake walikuwa wameanzisha bendi ya muziki iliyoitwa Cuban Brothers, wote walijua Miriam anaweza kuimba hivyo siku moja wakamuomba kama atataka kujiunga na bendi yao, Miriam akaona hii itakuwa ni kichekesho lakini akakubali kwa vile alikuwa tayari kufanya jambo jipya katika maisha yake. Akiwa Cuban Brothers walifanya maonyesho sehemu mbalimbali kama makanisani, kwenye sherehe za kuchangisha fedha (fundraising) na sehemu nyingine nyingi. Katika kipindi hicho kulikuwa na ukumbi maarufu sana uliojulikana kama Donaldson Community Centre ambao Cuban Brothers mara nyingi walikuwa wakipiga muziki hapo, huu ni ukumbi ambao watu wengi maarufu na wasio maarufu walipenda kwenda. Siku moja wakiwa katika onyesho Miriam alinong'onezwa na mwenziye kwamba Manhattan brothers wako ndani ya nyumba. Manhattan Brothers band kilikuwa ni kikundi cha muziki kinachojulikana sana wakati huo, kila mtu alipenda muziki wake. Baada ya onyesho Miriam alifuatwa na kijana mmoja na kujitambulisha kwa jina la Nathan Mdledle na kuwa ni kiongozi wa kundi la Manhattan Brothers, Miriam hakuamini macho yake kwamba anaongea na Manhattan brother, wakati akishangaa Nathan akamwambia anapenda jinsi anavyoimba, kama hiyo haikutosha, Miriam anasema almanusura aanguke baada ya kuambiwa anaonaje kama anataka kufanya usaili wa kujiunga na Manhattan brothers. Alikwenda kufanya usaili na kushinda hivyo akapata kazi.



Akiwa na Manhattan brothers aliweza kujulikana sana, hii ni kwa sababu kundi hili lilikuwa na kazi nyingi za ndani na nje ya nchi. Anasema Manhattan ilimfungulia milango yake ya mafanikio kwani baada ya kuwa nao makundi mengine mengi yalianza kumfuata ili afanye nao kazi yeye binafsi kama Miriam. Mwaka 1958 alipata bahati nyingine ya kuombwa kujiunga na kikundi cha African Jazz and variety. Hiki kilikuwa ni kikundi kinachozunguka sehemu mbalimbali ndani na nje ya nchi. Mwanzilishi wake alikuwa ni mama wa kiyahudi aliyeitwa Sara Silvia. Mama huyu alisema kuwa atahakikisha African Jazz and variet, inakuwa ni kikundi cha kwanza ambacho waafrika wataruhusikwa kupiga muziki mbele ya wazungu. Na kweli ndivyo ilivyokuwa, kikundi hiki kilikuwa kikifanya onyesho kwa wazungu watupu kila Alhamisi katika ukumbi wa Johannesburg city. Mwaka 1959 akiwa bado na African Jazz, alipata bahati nyingine kubwa ambayo tunaweza kusema ndiyo iliyo mtoa. Mtengeneza filamu mmoja kutoka Marekani aliyeitwa Lionel Rogosin, alimuona Miriam akiimba kwenye shoo za African jazz, alipenda sana uimbaji wake na akamuomba aimbe katika filamu aliyokuwa akiitengeneza COME BACK AFRICA. Miriam alikubali na akaigiza na kuimba katika filamu ile. Baada ya hapo Lionel Rogosin aliondoka na kuwaahidi kuwataarifu atakapomaliza kuitayarisha filamu ile. Huku nyuma mwaka huo huo 1959 februari, bahati nyingine ikaja kwa Miriam, King Kong Jazz Opera ilifunguliwa na Miriam akapata nafasi ya kuimba na kuigiza mle kama Joyce "Queen of Back of the Moon".

KUONDOKA AFRIKA.

Baada ya muda kupita Lionel Rogosin akaleta habari kwamba filamu yake ya COME BACK AFRICA imekamilika na imepokelewa vizuri hivyo ameiingiza katika Tamasha la Filamu la venice Italia(VENICE FILM FESTIVAL) kwa hiyo anamualika Miriamu Makeba kuungana naye katika kuitambulisha film hiyo huko Venice na Ulaya kote.

Anasema hakuamini macho yake kupata nafasi ya kwenda Ulaya, wakati huo kazi yake ilikuwa ikienda vizuri sana alikuwa bado akifanya kazi na King Kong kitu ambacho ni hatua kubwa sana kwake yeye na sasa anapata nafasi ya kwenda Ulaya? Hakuamini macho yake. Haraka aliomba pasipoti, alisumbuliwa sana hadi kuipata kwa sababu makaburu walijua kila kitu kuhusu Miriam na walijua kwamba ameshiriki katika filamu ya come back Africa, hatimaye alipewa na kuondoka bila kuchelewa, ilikuwa ni mwaka 1959.



Safari yake ilianza na alifika London salama na kukutana na mwenyeji wake Lionel Rogosin na mkewe. Akiwa pamoja na wenyeji wake sasa walianza safari ya kuelekea Venice Italy kwa gari. Walifika Venice wakazindua film yao katika tamasha lile na kwa bahati film yao ikawa ni miongozi mwa film zilizopata tuzo, ilishinda Critic Award.