19 November 2006

Shabiki na Ushabiki!

Wasomaji wapendwa, habari hii chini inawajia kwa hisani ya mwanablogu MtiMkubwa.....

Naam,

Hakuna kitu kibaya kama unazi, ushabiki, au umaamuma. Ushabiki unaweza kuwa wa kidini, kiitikadi, kikabila, kirangi, kimichezo, kitaaluma au hata kumshabikia mtu binafsi. Shabiki akiamua kushabikia jambo analoshabikia hata wakitumwa malaika, mitume na manabii kumsilimu hasilimiki.

Siku chache zilizopita nilikutana na shabiki mmoja. Huyo shabiki alipoanza ushabiki wake nilifikiri alikuwa anatania kwa sababu sijawahi kukutana na mtu anayemshabikia mtu kwa namna ya yule shabiki. Sina jinsi ya kumuelezea shabiki mwenyewe lakini ni kijana anayetokea mikoa ya kanda ya ziwa, tena ana lafudhi kali ya kanda ya ziwa, na aliyebahatika kupata ajira serikalini. Tulikuwa tunazungumzia operesheni bomoa bomoa ya RC Kandoro, ndipo huyo shabiki alipoingilia mazungumzo na kusema "..Hiyo yote ni mipango ya JK..Unajua ameunda Wizara ya Mazingira iri kumekishua kwamba jiji rinakuwa safi..Yeye mwenyewe yuko Marekani rakini huku nyuma kaacha maagizo akirudi Wamachinga wawe wameshaondoka.." Miye na jamaa yangu mwingine tukageuka kumsikiliza shabiki. Alipoona tumeonyesha nia ya kumsikiliza ikawa tumefungulia ushabiki "..JK bwana ni mjanja sana. Unajua kamreta huyu kocha iri Tanzania iende woridikapu. Na huo ni mmoja wa mipango yake ya muda mrefu..Na utaona Tanzania itafika woridikapu.." Jamaa yangu akamuuliza "..Tanzania itafika woldikapu kwa sababu ya JK?.." Yule kijana akajibu "..Usifanye mchezo na JK, nyie turieni mtaona..Unajua JK amekwenda Marekani kwenye jenero asembri rakini pia kaenda kuonana na Bush..Yaani Bush anamuadimaya sana JK katika viongozi wote wa Afrika..." Jamaa yangu akaniambia "..Unasikia insaidi storizi hizo?.." Nikamjibu "..Nazisikia.." Yule kijana kusikia hivyo moto ukazidi kumpanda "..Kwa mikakati ya JK bai dhe endi ofu dhisi manthi yaani Septemba umeme utakuwa umerudi nchi nzima..Yaani jamaa anachapa kazi siyo mchezo endi hi izi so krozi tu dhe pipo kwa hiyo anayajua matatizo ya Watanzania kwa karibu zaidi anraiki Mkapa..Mkapa arikubarika inteneshinari rakini rokari hakuwa karibu na wananchi..JK ameshaanza kurudisha njia za kuu uchumi mikononi mwa wananchi, ATC tayari imesharudi harafu sasa hivi anashugurikia mikataba ya madini, yaani kwa kweri katika kipindi kifupi amefanya mambo mengi sana tena makubwa.." Jamaa yangu akamwambia "..Aisee.." Hapo shabiki ndiyo akazidi kupamba moto "..Ingekuwa JK ndiye ariyekuwepo madarakani wakati ure Baba wa Taifa asingefariki.." Niliposikia hivyo ikabidi niingilie mazungumzo "..Hebu tuache ushabiki hapa na tuzungumze yaliyo kweli..Ni kweli kuwepo kwa JK madarakani kunaweza kurefusha au kufupisha maisha ya mtu au watu.." Kabla sijamaliza hoja yangu yule shabiki akarukia "..Na ndiyo maana awamu ya ine sera yao ni Maisha bora kwa Watanzania wote..JK anataka kira Mtanzania awe na maisha bora..Ndiyo maana hapati usingizi kwa kufikiri jinsi gani atawapatia Watanzania maisha bora..Yaani kwa kweri tunaomjua kwa karibu tunaerewa anavyohangaika kuwatafutia Watanzania maisha bora.." Jamaa yangu akamwambia "..Ndiyo hatamu na maana ya uRais kulinda masilahi ya wananchi wake.." Shabiki akajibu "..Rakini siyo maraisi wote wanakumbuka hiro na hapo ndipo JK anapochukua pointi kurinda masirahi ya wananchi..JK bwanaa..Yaani wee acha tu..Baadhi ya watu hawamuerewi kwa hiyo wanamkritisaizi widhiauti eni graundis..Aripoteuwa kabineti wapinzani wakamkritisaizi eti baraza kubwa sana.. Yeye ariunda kebineti kubwa iri kuzidisha efishensi..Sasa hivi ware wariomkritisaizi wameshushuka baada ya kuona jinsi kabineti inavyochapa kazi..Ini Tanzanian histori kabineti hii ni drimu timu..Hakuna kabineti iriyowahi kuundwa kama hii ya sasa hivi, yaani kira ariyepewa wizara inamfiti..Teri mi huu izi ini dhe rongi ministri?! Shemeji yangu Dokta Migiro fits pafektri weri in foreni afeazi.. Mama Meghji -fainansi, bajeti aliyoisoma hata Kenya na Uganda wameomba kopi..Msabaha kwenye madini na nishati humo ndiyo mwake kabisa, unajua mambo ya madini ni grobo biznesi na Msabaha ni mtu dipromasia kwa hiyo atayauza madini kiurahisi na kwa bei nzuri tu...Mramba wizara ya miundombinu, jamaa ni rongi eksipiriensid na JK kamuweka pare makusudi kwa sababu pare panatakiwa mtu mwenye rongi eksipiriensi.." Jamaa yangu akamwambia "..Ahaaa hili baraza kiboko.." Shabiki akarukia "..Harafu ormosti dhe whori kabine au thrii kota ni niyuu fesiz tena ni vijana vijana na akina mama kawapa wizara nyeti zote isipokuwa urinzi..Hapo ndipo anapothibitisha Nguvu mpya, Ari mpya, na Kasi mpya JK bwana ni kiboko..Nyie bwana JK izi dhe prezidenti..Halafu amekubarika na wananchi, ukiangaria historia ya Tanzania ni viongozi wanne tu wariokubarika na Wananchi; Hayati Baba wa Taifa, Hayati Sokoine, Agostini Murema, na JK! Bati Murema disapointedi dhe masizi kwa hiyo femu yake inawitha siku hadi siku.." Wakati anaendelea kutupiga darasa kilongalonga chake kikamuita akasogea pembeni kuongea, alipomaliza akarudi kutuomba radhi kwamba ameitwa ofisini, akaondoka. Miye na Jamaa yangu tukaondoka tukiwa ndani ya gari jamaa yangu akaniambia hayo ndiyo maoni ya wengi.

Leo nimekutana na kipande kingine cha habari. Miye nimekiona kama ushabiki wa yule shabiki wa Kikerewe. Ningelikuwa na namna ningewaomba viongozi wambane huyo tarishi wa Waziri Mkuu wa Malaysia aliyeko nchini Tanzania juu ya mkataba wa IPTL. Halafu pia kumdhibiti asije akatuletea balaa nyingine kubwa zaidi ya IPTL. Ushabiki wenyewe huo hapo chini.

Ziara za JK nje zaanza kuzaa matunda 2006-11-18 10:34:26 Na Joseph Mwendapole

Ziara za Rais Jakaya Kikwete nje ya nchi kutafuta wawekezaji, sasa zimeanza kuzaa matunda kutokana na baadhi ya wawekezaji kuwasili nchini kuangalia mazingira ya uwekezaji. Akizungumza na waandishi wa habari jana, Waziri wa Mipango na Uwezeshaji, Dk. Juma Ngasongwa, alisema makampuni mengi yamekuwa yakiandika barua pepe yakionyesha nia ya kuja kuwekeza nchini. Alitaja baadhi ya wawekezaji ambao tayari wamewasili nchini kuwa ni Benki ya Uwekezaji ya Kuwait, ambayo Mkurugenzi wake, Bw. Jassem Zainal yuko nchini kuangalia mazingira ya kuwekeza. Waziri Ngasongwa alimtaja mwingine kuwa ni Naibu Waziri Mkuu wa Malaysia, Bw. Annuary Ibrahim, ambaye ameambatana na wageni hao. Alisema Bw. Ibrahim aliteuliwa na Rais Jakaya Kikwete, kusaidia kampeni zake za kutafuta wawekezaji wa kuja kuwekeza nchini. Dk. Ngasongwa alisema Bw Ibrahim ni rafiki wa kweli aliyekubali ombi la Rais Kikwete kuitangaza Tanzania duniani. ”Kuonyesha kuwa kweli ni rafiki yetu, Bw. Ibrahim leo ametuletea wawekezaji watakaowekeza kwa kiasi kikubwa katika sekta ya fedha,” alisema. Alisema wawekezaji hao bado wanaendelea na mazungumzo na serikali ili kuangalia namna ya kuendesha shughuli zao. ”Wamenihakikishia kuwa, mambo yakienda sawa mwanzoni mwa mwaka ujao wataanzisha benki kubwa ambayo itakopesha watu wengi kwa riba ndogo,” alisema Dk. Ngasongwa. Dk. Ngasongwa alisema Korea imeahidi kujenga daraja la Malagarasi kwa dola milioni 25 za Kimarekani ambazo zitatolewa kwa Tanzania kama mikopo nafuu. Alisema wawekezaji wa kampuni ya Samsung na DAEWOO, imeahidi kuwekeza upande wa teknolojia ya habari na mawasiliano. Alisema serikali ya nchi hiyo pia imekubali kuwekeza katika uzalishaji wa nishati ya umeme. Akizungumzia ziara ya China, Dk. Ngasongwa alisema serikali ya nchi hiyo imeahidi kusaidia kuongeza uzalishaji katika mradi wa Kiwira hadi kufikia Megawat 200 kutoka sita za awali.

04 November 2006

Huyu ni nani?