22 October 2006

Wangari Muta Maathai.


Wangari Muta Maathai, mwanamke mwafrika wa kwanza kushinda Nishani ya amani ya Nobel tangu kuanzishwa kwake mwaka 1900.

Mwaka 2004, niliposikia mwanamazingira mama mpanda miti, Wangari Maathai ndiye mshindi wa nishani ya Amani ya nobel, nilishindwa kabisa kuelewa ni kwa kigezo gani aliweza kuchaguliwa kuwa mshindi wa tuzo hii ambayo ni moja wapo ya tuzo ya zaidi ulimwenguni. Nilijiuliza "Miti na Amani" wapi na wapi? na kutokana na swali hilo nilianza kumfuatilia kwa makini zaidi mama huyu na ndipo nilipogundua uwezo mkubwa wa akili alionao mama huyu.

Mama Wangari Muta Maathai alizaliwa 01/04/1940 katika kijiji cha Tetu kilichopo Nyeri nchini Kenya. Baba yake bwana Muta Wanjugu na mama yake Lydia Wanjiru Muta ambao walikuwa wakulima, walimpeleka Wangari shule baada ya kaka mkubwa wa Wangari Nderitu kushauri kwamba dada yake ni lazima asome kitu ambacho katika miaka hiyo kilikuwa ni nadra sana, ni watoto wachache sana wa kike walipelekwa shule katika miaka hiyo.

Hivyo alianza shule ya msingi Itithe mwaka 1948 hadi 1951 darasa la kwanza hadi la nne. Akafuatia shule ya Mtakatifu Cecilia mwaka 1952 hadi 1955 darasa la tano hadi la nane. Alimaliza elimu ya msingi na kujiunga na sekondari ya wasichana ya Loreto kidato cha kwanza hadi cha nne kati ya mwaka 1956 na 1959. Baada ya hapo alibahatika kupata ufadhili wa kwenda nchini Marekani kwa ajili ya masomo ya juu zaidi, huko alijiunga na chuo cha Mtakatifu Scholastica cha Kansas kwa Shahada yake ya kwanza katika baiolojia ikiwa ni mwaka 1960 hadi 1964, mwaka huo huo 1964 alijiunga na chuo kikuu cha Pittsburgh kwa shahada ya pili ambapo alimaliza mwaka 1965. Mwaka 1966 alirudi nyumbani Kenya na kupata kazi katika Chuo kikuu cha Nairobi kama mtafiti msaidizi.

Mwaka 1969 alifunga ndoa na mfanyabiashara na mwanasiasa Bwana Mwangi Mathai, ambapo walibarikiwa kupata watoto watatu, Wanjira, Weweru na Muta. Kuwa na familia yake mwenyewe haikumfanya Wangari kuacha kujiendeleza kimasomo, kwani mwaka 1971 Waangari alipata PhD na inasemeka kwamba alikuwa ni mwanamke wa kwanza kutoka Afrika mashariki na kati kufikia kiwango hicho cha elimu. Na mwaka 1977 alikuwa Profesa.

MWANZO WA KUWA MWANAMAZINGIRA NA KUINGIA KATIKA SIASA.

Mwaka 1974 Bwana Mwangi Mathai muwewe na Waangari aliamua kugombea ubunge katika jimbo la Langata, Wangari akiwa mkewe ilibidi awe bega kwa bega na mumewe katika kampeni. Bwana Mwangi kama ilivyo kawaida ya wanasiasa aliwaahidi mambo mengi wananchi wake ikiwa ni pamoja na kutatua tatizo la ajira. Wangari alisikiliza kwa makini malalamiko ya wananchi na hakuyachukulia mzaha. Kwa bahati nzuri Bwana Mwangi alishinda kiti cha ubunge, na ni hapo Wangari aliona umefika wakati wa kuyatekeleza yale waliyokuwa wakiahidi. Akaamua kuunda kampuni binafsi iliyoitwa ENVIROCARE malengo yake ikiwa ni kutaka kutengeneza ajira kwa wananchi, lakini kwa bahati mbaya kampuni haikuendelea kutokana na ukosefu wa fedha za kutosha. Wakati huo huo Wangari alikuwa ameshaanza kujihusisha na harakati za ukombozi wa mwanamke na tayari alikuwa mwenyekiti wa baraza la Taifa la wanawake Kenya, akiwa kiongozi katika baraza hilo aliendelea kupata malalamiko juu ya shida wanazozipata wanawake katika maisha yao ya kila siku, kwamba hawana maji, kuni wala chakula chao na cha mifugo yao na huwalazimu kutembea mwendo mrefu ili kuvipata hivyo.

Wangari aliyatizama yale malalamiko na kuona kuwa ni matokeo ya ugonjwa mbaya uliyoikumba Kenya na nchi nyingi za Afrika. Ugonjwa wa kuharibu na kutokujali kabisa mazingira, miti kukatwa ovyo bila kupandwa mingine ndio aligundua kuwa na chanzo shida zote wanazozipata wananchi wa Kenya. Hivyo akaja na wazo la kuanzisha mradi wa kupanda miti kwani miti huilinda ardhi mmomonyoko wa udongo, huifadhi vyanzo vya maji, hutoa chakula, mbao za kujengea, kuni na huweza kuwa chanzo kipato na mambo mengine mengi.

Hivyo tarehe 05/06/1977 ambayo pia ilikuwa ni siku ya mazingira duniani, Wangari alizindua rasmi kampeni ya upandaji miti Kenya, yeye na wenziye walianza kwa kupanda miti saba katika bustani ya Kamukunji Nairobi. Na kuanzia hapo Jumuiya vuguvugu ya ukanda wa kijani ilizaliwa (The Green Belt Movement).

Ingawa jambo hili alilolianzisha Wangari ni jema na lina nia nzuri kwa Wananchi lakini si wote walioliunga mkono. Baada ya kusimama na kuonekana hana mzaha kwa kile anachokifanya hasa akiwa mwanamke, upinzani ulianza kujitokeza kuanzia katika familia yake hadi katika serikali tawala kipindi hicho chini ya Rais Daniel Moi.
Kwa upande wa kifamilia, mumewe bwana Mwangi kama ilivyo kawaida ya wanaume wengi wa kiafrika kutaka kutawala wake zao, hapa ilishindikana kabisa kwani alikuta mkewe ni mtu anayesimama na kupigania kile anachokiamini ni kweli. Matokeo ya haya yote bwana Mwangi aliamua kutoa talaka kwa madai kwamba mkewe ni mkaidi mno, msomi mno mwenye mafanikio makubwa na ni kazi kubwa kumthibiti. Ndoa yake ilivunjika miaka ya themanini.

Kwa upande wa serikali, alipata matatizo kwa vile alikuwa na ujasiri wa kudiriki kuisema serikali ya Moi hadharani bila woga kitu ambacho kilimsababishia kutiwa gerezani mara kadha wa kadha, kupigwa hadi kupoteza fahamu na askari. Lakini katika mambo hayo yote linalokumbukwa zaidi ni lile la miaka ya tisini, ambapo serikali ilitaka kutumia eneo la bustani ya kupumzikia ya Uhuru Park ya Nairobi kujenga jengo la ghorofa 62 ikiambatana na sanamu yake yenye urefu wa futi 60 vyote hivi vikikadiriwa kugharimu dola za kimarekani milioni 200, ambazo nazo ni za kukopwa katika mashirika ya kigeni. Kwa hali moja au nyingine wako ambao hawakulipenda wazo hili lakini kutokana na kukosa ujasiri wa kumkosoa Rais Moi hakuna aliyediriki kupinga. Wangari mwanamke wa shoka alisema hakijengwi kitu hapa. Alikuwa na sababu kuu mbili:
1. Sababu ya kimazingira - kwamba ni kwanini litumike eneo la kupumzikia watu
kujenga ghorofa hilo? ..akaendelea kwamba "Tembo na Vifaru wanatengewa sehemu
za kupumzikia, kwa nini na binadamu wasiwe na sehemu ya kupumzikia?

2. Sababu za kiuchumi - kwamba inakuwaje nchi kama Kenya ambayo watu wake wanakufa
kwa njaa na wakati huo huo inakabiriwa na madeni makubwa, bado inataka kukopa
fedha zote hizo kwa ajili ya jengo moja tu la fahari?.

Msimamo wa Wangari ulifanya mashirika yaliyokuwa yamekubali kutoa fedha hizo kubadili mawazo yao na wazo la kujenga jengo la fahari na sanamu ya Moi kuishia hapo. Kutokana na hili Rais Moi alikasirika sana hadi kuifunga ofisi ya Green belt Movement, ingawa baadaye ilifunguliwa. Na kuanzia hapo alimbatiza jina la 'Mad Woman'. Pamoja na hayo yote bibi Wangari hakukata tamaa kufanya kile alichoamini kuwa anatakiwa kukifanya na hakujua ni kwa kiasi gani kumbe dunia ilikuwa ikimuunga mkono hadi mwaka 2004 ambapo alishangazwa kwa kuchaguliwa kwake kuwa mshindi wa Nishani kubwa ya Amani duniani.

UHUSIANO KATI YA UTUNZAJI WA MAZINGIRA NA AMANI DUNIANI.

Kama nilivyosema hapo awali kwamba mimi pia sikuelewa uhusiano uliopo kati ya upandaji wa miti na amani duniani, kuna watu wengi ambao pia hili liliwatatiza na kupelekea watu wengi kutaka kujua uhusiano uliopo. Na Bibi Wangari alijibu kama ifuatavyo....
Vita vyote vilivyopo duniani leo ni vita vya kugombea mali asili kama ardhi yenye rutuba, maji, mafuta, madini n.k na watu wamesahau kwamba hivi vyote vinatokana na utunzaji mzuri wa mazingira ambao hupelekea kutokupungua kwa mali asili, na hivyo kila mmoja kupata za kumtosha, hali ambayo inapunguza migogoro ya kunyang'anyana na kufanyiana hila za kuuana. Kwa hiyo basi kwa kupanda miti tu kunaweza kuhakikisha amani kubwa sana duniani, kwani miti italeta mvua, ardhi itapata rutuba, wafugaji hawatatapatapa kutafuta malisho, kuni zitakuwepo za kutosha, chakula cha kutosha, umeme n.k na ni kwa dhana hii pekee ya Bibi Wangari ya kupenda kushughulika na chanzo cha tatizo ndiyo iliyompelekea kupata Nishani ya Amani ya Nobel mwaka 2004. Na kuanzia hapo dunia ilianza kumtafuta ili kupata zaidi busara zake. Miongoni akiwa ni Oprah Winfrey. Hapa pia kuna hotuba yake aliyoitoa mwaka huu katika chuo cha Connecticut kilichopo Marekani, kwa kweli hotuba hii nimeipenda sana na inatia moyo sana hasa kwa wale tunaopenda kusimama katika ukweli wa lile unaloliamini hata kama hakuna anayekuunga mkono.

Mungu mbariki Mama Wangari Muta Maathai.