27 April 2006

Eti siku ya mtu kuzaliwa ni ya nani?..mama au mtoto?


Pichani juu ni mimi na kaka yangu na chini ni mzaa chema.

Hapo kipindi cha nyuma nilipata kuzua mjadala na mshairi maarufu wa kikundi cha Parapanda Mgunga mwa Mnyenyelwa juu ya hasa ni nani mwenye haki ya kuiita siku yake, je ni mama au mwana? kwa mujibu wa Mgunga anasema siku ya mtu kuzaliwa ni haki ya mama na kama ni sherehe au pongezi zote anayetakiwa kupewa ni mama. Hili nimelikumbuka leo kwa vile ni siku yangu ya kuzaliwa..., haya wewe unasemaje? ni nani anayetakiwa kupewa pongezi katika siku za kuzaliwa?

"Unapokuwa mwanamke mweusi duniani..." Hotuba aliyotoa Winnie Mandela Chicago Marekani.


Mwezi uliopita Winnie Mandela kwa heshima zote alialikwa na jamaa wa V-103'Expo huko nchini Marekani (Chicago) kuhutubia juu ya Nafasi ya mwanamke mweusi duniani, Winnie aliandaa hotuba nzuri sana lakini tofauti na matarajio yake watu waliacha kumsikiliza na kwenda kuangalia maonyesho mbalimbali yaliyokuwa yakiendelea katika ukumbi huo na yeye kutokana na utovu ule wa nidhamu akaamua kukatisha hotuba.

Ni hotuba nzuri na sana nimeona niwawekee hapa ili wote tuisome. Mwandani asante kwa kuniletea habari hii nimeona si bora kuifaidi peke yangu.

14 April 2006

Bibi Mohamed!..Mwanamke wa kwanza nchini kushika madaraka ya uwaziri. Hongera MtiMkubwa kwa kutegua.




Kwanza niwashukuru wachangiaji wa mada hii, na pia tumpigie makofi ya pongezi MTIMKUBWA Tungaraza kwa kutegua kitendawili hiki mapemaaa! Huyu jamaa ana kumbukumbu za karne. Pia ninamshukuru bwana Michuzi kwa kuibua mjadala mwingine juu ya kina mama na uongozi katika vyombo vya habari, binafsi nilikuwa bado sijaanza kuifuatilia nyanja ya Habari na nafasi ya wanawake katika kuviongoza vyombo hivyo..."Raha ya blogu jamani".

Haya, Bibi Titi Mohamed alikuwa si mwanamke wa kwanza tu kushika nafasi ya uwaziri nchini, bali pia ni mwanamke wa kwanza aliyejitolea kupigania uhuru wa Tanganyika hadi ukapatikana bila kukata tamaa pamoja na kwamba alikubwa na misukosuko mingi. Hapa kuna habari kamili ya jinsi alivyojiunga na harakati hizi za ukombozi. Habari hii aliitoa yeye mwenyewe miaka michache kabla ya kufariki kwake. Na hapa kuna orodha kamili ya mawaziri wanawake wa Tanganyika na Tanzania.

Shujaa Bibi Titi alifariki 5/11/2000 katika hospitali ya NETCARE Johannesburg Afrika Kusini.

09 April 2006

Unamfahamu mwanamke wa kwanza kuingia katika baraza la mawaziri la tanzania?


Pengine kuna haja ya kuwajua mashujaa wetu wa kwanza kabisa waliojitolea kwa mioyo yao yote kuipigania nchi yetu. Wako wengi ingawa leo hii wanasikika wachache tu. Swali langu au tuite mtego wangu wa leo ni kumtaja mwanamke wa kwanza kuingia katika baraza la mawaziri Tanzania wakati huo ikiwa ni Tanganyika na je ni ipi nafasi yake leo katika Tanzania yetu, je anaenziwa kama kina Karume na Nyerere hadi kupewa siku za mapumziko? Kumbuka enzi hizo hadi uweze kushika nafasi ya uwaziri ni lazima harakati zako za kupigania uhuru zilikuwa na za kiwango cha juu.

JE MWANAMKE HUYU NI NANI?